Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Lissu aanza kuvaa ‘bulletproof’ kujilinda na risasi

Muktasari:

  • Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu amesema ameanza kujilinda mwenyewe kwa kuvaa mavazi ya kujikinga na risasi, baada ya kudai kuwapo kwa tishio la uhai wake.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu amesema ameanza kuvaa mavazi ya kujikinga na risasi (bulletproof) ili kulinda usalama wake kutokana na tishio la usalama wake, akidai polisi hawajaonyesha nia ya kumlinda.

Kauli hiyo ya Lissu imekuja siku moja baada ya Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro kuyafananisha madai ya Lissu na uhuru wake wa maoni, huku akisisitiza kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kutekeleza wajibu wake wa kikatiba wa kuhakikisha raia wote wanakuwa salama pamoja na mali zao.

Desemba 16, 2024, kupitia ukurasa wake wa X, Lissu alidai kuwa kuna njama za kumdhuru na kutoa onyo kwa wanaolenga kutekeleza tukio hilo na baadaye kufafanua suala hilo kwenye vyombo vya habari.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 18, wakati akirejesha fomu ya kuwania uenyekiti wa chama hicho, Lissu alisema hajafurahishwa na kauli ya Jeshi la Polisi, na ndio maana ameanza kujilinda mwenyewe.

"Jana nilizungumzia vitisho vilivyotolewa dhidi yangu, na nimeona Jeshi la Polisi wakisema kwamba hawawezi kumlinda mtu binafsi, hata kama mtu huyo aliponea chupuchupu kuuawa kwa kupigwa risasi 16, kwenye majengo ya Serikali, na waliohusika hawajawahi kutafutwa wala kuchukuliwa hatua zozote," amesema.

Lissu ameongeza kuwa, kwa kuwa Jeshi la Polisi limekataa kumlinda au kuchukua hatua kuhusu taarifa anazotoa za tishio la usalama wake, ameamua kuchukua hatua za kujilinda mwenyewe.

"Nimeamua kujilinda mwenyewe, ndio maana nimeamua kuvalia mavazi ya namna hii, bulletproof, kwa kuwa jeshi halitaki kunilinda," alisema.

"Wamesema hadharani kwamba hawatanipa ulinzi kwa sababu jukumu lao ni kulinda raia wote kwa usawa. Lakini, raia wote hawakabiliwi na tishio la maisha yao kwa usawa. Mimi nimeshakaribia kuuawa mara moja kwa kupigwa risasi 16, tishio dhidi yangu haliwezi kuwa sawa na mtu mwingine ambaye hajawahi kushambuliwa," amesema.

Lissu alieleza kuwa kauli ya Kamanda Muliro, kwamba hawezi kutoa ulinzi kwa mtu aliyewahi kushambuliwa, ni ishara kwamba anatakiwa kujitegemea katika kujilinda.

"Uhai ni wa kwangu, ni lazima nijilinde mwenyewe baada ya Jeshi la Polisi, lenye jukumu la kufanya hivyo, kukataa," aliongeza.

Katika hatua nyingine, amezungumzia kuhusu wafuasi waliojitokeza nyumbani kwa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, Mikocheni Dar es Salaam kumtaka agombee uenyekiti, kuwa hali hiyo haimpi hofu.

"Hainipi hofu hata kidogo. Haya makundi yanayoitwa wanachama, wafuasi na wapenzi, hii si mara ya kwanza. Mwaka 2019 ilikuwa hivyo, 2014 ilikuwa hivi hivi. Mwenyekiti huwa analazimishwa kugombea na kushinikizwa na wanachama; kama hiyo ni stahili yake, siwezi kuwa na shida nayo," alisema.

Lissu alirejesha fomu yake leo katika ofisi za makao makuu ya chama hicho zilizopo Mikocheni, Dar es Salaam na kupokelewa na Naibu Katibu Mkuu wa Tanzania Bara, Benson Kigaila.

"Nimeshakabidhi fomu zangu za kugombea nafasi ya mwenyekiti wa Chama Taifa kwa Naibu Katibu Mkuu wa Tanzania Bara, Benson Kigaila na zimeshapokelewa. Kinachofuata ni kusubiri hatua za mbele," amesema Lissu.