Prime
Latra wawageukia wenye malori mfumo wa VTS

Muktasari:
- Awali, mfumo wa VTS ulifungwa kwenye mabasi ya abiria ikiwa ni hatua ya kupunguza ajali za barabarani zinazosababishwa na mwendokasi na uchovu wa madereva
Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), imesema mwaka huu itaanza kufunga mfumo wa kufuatilia mwenendo wa gari (VTS) kwenye malori na kuweka utaratibu mpya wa ratiba kwa madereva wa magari hayo.
Awali, mfumo huo ulifungwa kwenye mabasi ya abiria ikiwa ni hatua ya kupunguza ajali za barabarani zinazosababishwa na mwendokasi na uchovu wa madereva.
Mfumo huo huwezesha mamlaka kumtambua dereva anayeendesha gari husika endapo atasajiliwa na kutumia kitufe cha utambuzi wa dereva (i-button).
Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Februari 2, 2025 Mkurugenzi Latra, Johansen Kahatano amesema katika kupunguza ajali kwa mwaka huu wataanza kufunga VTS kwenye malori na ratiba ya madereva.
“Baada ya mabasi na special hire tunafuata na malori, si kufunga VTS pekee bali na kuweka ratiba za mapumziko ya madereva, utaratibu huo tutauanza mwaka huu,” amesema.
Wakati wa kutoa salamu za mwaka mpya, Rais Samia Suluhu Hassan alisema takwimu za Jeshi la Polisi Tanzania zinaonyesha kati ya Januari hadi Desemba mwaka 2024, jumla ya ajali 1,735 kati ya hizo 1,198 zilisababisha vifo 1,715.
“Hii ni idadi kubwa sana. Ndugu zetu wengine 2,719 walijeruhiwa katika ajali za barabarani. Asilimia 97 ya ajali hizi zimetokana na makosa ya kibinadamu, kubwa kabisa ikiwa ni uzembe wa madereva, uendeshaji hatari na mwendo kasi ambao ni asilimia 73.7 ya ajali zote,” alisema.
Kauli ya Polisi
Mkaguzi wa Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani, Dumu Mwalugenge amesema wamekuwa wakitamani mfumo wa VTS ufungwe kwenye malori kwa kuwa, utasaidia kudhibiti ajali.
“Hii ikifungwa itasaidia Jeshi la Polisi kwa maeneo ambayo hawapo hususani porini, maana ni ngumu polisi kuwepo kila mahali,”amesema Dumu.
Amesema wamekuwa wakitumia kamera zao kwa maeneo machache na imepunguza kidogo kwa madereva kupeana ishara ya uwepo wa askari mahala fulani.
Pia, amesema kwa Desemba 2024 hadi Januari 2025 wameshafungia leseni 56 kwa makosa mbalimbali ikiwamo ulevi na mwendokasi.
Walichokisema madereva
Mwenyekiti wa madereva Tanzania, Schubert Mbakizao amesema mfumo huo walishaukataa muda mrefu kwa sababu hausaidii kupunguza ajali.
“Hili halitosaidia kitu chochote kwenye kupunguza ajali zaidi ya hapo ni kuongeza faini za barabarani kutoka kwa madereva kwani mafuta anayopewa dereva hayamruhusu kukimbia zaidi ya spidi 70,” amesema Mbakizao.
Amesema mfumo huo, hauna tofauti na kamera za polisi za barabarani ambazo hazipunguzi ajali bali zinatoa onyo kwa kumlipisha dereva faini kutokana na mwendo aliotembea.
Amesema ifanywe tathimini ndogo tangu wamefunga mfumo wa VTS hali ikoje, ajali zimepungua au zinaendelea na kusababisha vifo na majeruhi.
Mbakizao amesema ili kudhibiti kuna haja ya kurudi katika mfumo wa zamani wa kudhibiti mwendo (Speed governor) uliokuwa unazuia gari kuendelea na safari baada ya kuzidisha mwendo.
John Michael, dereva wa lori linalosafirisha mizigo ndani ya nchi, amesema mfumo wa VTS na wanaweza kupumzika lakini utawapunguzia safari.
"Kupumzika ni muhimu, lakini mfumo huu unaweza kutufanya tupoteze safari moja au mbili kwa siku, jambo litakalopunguza kipato chetu," amesema John.
David Joram, anayefanya safari Zambia na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), amesema hatua hiyo inayochukuliwa na Latra itaokoa maisha na kupunguza msongo wa kazi.
"Mara nyingi tunalazimika kuendesha saa nyingi ili kufanikisha safari kwa wakati, lakini kama kuna ratiba rasmi, itatusaidia kupata muda wa kupumzika bila kushinikizwa," amesema David.
Amesema makosa mengine ni uzembe tu wa dereva ambao wamejikuta wakiangukia kwenye ajali kwa sababu ya haraka ya kufikisha mzigo aliyobeba.
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori ya Kati na Madogo, Chuki Shaban amesema wapo tayari kwenye ufungwaji wa TVS lakini hilo la ratiba walikubaliana mwisho wa kuendesha gari ni saa 12.
“Japokuwa hatujaambiwa lakini tupo tayari kufungiwa VTS ila katika suala la muda tulishakubaliana mwisho wa kuendesha gari ni saa 12 baada ya hapo dereva apumzike ukiona anaendesha zaidi ha hapo ni ubishi na maamuzi binafsi ya dereva,”amesema Chuki.
Amesema kwa madereva wa malori kuendesha zaidi ya mwendokasi wa 80 ni ngumu kwa sababu wanabeba mizigo mizito, hivyo ni ngumu kuyakimbiza.