Latra kujadili ongezeko nauli za daladala, mabasi

Muktasari:
- Latra kuitisha mkutano kujadili ongezeko la nauli mpya kwa daladala na mabasi ya mikoani baada ya kampuni tatu zinazotoa huduma hiyo kuwasilisha maombi ya kufanya hivyo kufuatia gharama za uendeshaji kuongezeka.
Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhi (Latra) imekusudia kuitisha mkutano wa wadau wa sekta ya usafiri nchini kupokea maoni kuhusu marejeo ya nauli za mabasi ya mikoani na daladala.
Aprili 2022, Latra ilitangaza kupanda kwa viwango vya nauli kwa daladala ilikuwa kuanzia kilomita 0 hadi 10 ilipanda kwa Sh100 wakati kwenye mabasi ya mikoani daraja la kawaida kwa kilomita moja iliongezeka kwa asimilia 11 kutoka Sh36 hadi 41.
Mkutano huo unatarajiwa kufanyika Oktoba 18, mwaka huu Dar es Salaam na shinikizo la kufanya hivyo linatokana na kampuni za Super Feo, Enterprises, ABC Upper Class na Happy Nation kuwasilisha maombi ya kupitiwa upya nauli kutokana na ongezeko la gharama za uendeshaji unaosababishwa na kupanda kwa bei ya mafuta.
Kwa mujibu wa barua iliyotolewa kwa umma na Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano Latra imeonesha kampuni hizo zimetoa mapendekezo tofauti ya kuongeza nauli kutoka ya sasa ya Sh56.88 kwa kilometa 1 kwa kila abiria.
“Super Feo Enterprises kwa daraja la Kati imependekeza Sh101.88 ongezeko kwa kilomita moja Sh45.00 sawa na asilimia 79.11, Kampuni ya ABC daraja la Kati Sh92.84 ongezeko la kilomita moja Sh36.96 ikiwa sawa na asilimia 63.22 na Happy Nation kwa daraja la kati Sh84.06 ongezeko la Sh27.18 sawa na asilimia 47.78,” imesema.
Kupitia barua hiyo imesema sheria ya Mamlaka ya Latra, sura ya 413 na kanuni ya 9(3) ya kanuni za Latra (tozo) za mwaka 2020 (tangazo la Serikali Namba. 82 la Julai 2,2020, Mamlaka inapaswa kutoa fursa kwa kampuni hizo kuwasilisha mapendekezo yao kwa wadau wa usafiri wa abiria kisha kukusanya maoni ya wadau kabla ya kufikia uamuzi.
“Nauli zinazotumika kwa sasa zilitangazwa kwenye Gazeti la Serikali namba 18 la Mei 6, 2022 na mamlaka imeandaa mkutano wa wadau kupokea maoni juu ya mapendekezo ya watoa huduma ya kufanya marejeo ya nauli za mabasi ya masafa marefu,” imesema taarifa hiyo.
Katika mkutano huo, Latra itawasilisha mapendekezo ya vigezo vya mchakato wa kuridhia mapitio ya viwango vya nauli za mabasi yanayotoa huduma mijini (daladala). `Wasilisho litafanywa kwa mujibu wa kanuni ya 13 ya kanuni za tozo za Mwaka 2020.
“Kutokana na umuhimu wa suala hilo wadau wote wa usafiri wa umma na wananchi kwa ujumla tunawaalika kuhudhuria mkutano huu muhimu ili kutoa maoni baada ya kusikiliza mapendekezo yatakayowasiliishwa na kampuni zilizoleta maombi ya kufanya marejeo ya nauli ,” imesema.
Angalizo
Latra imetahadharisha wakati mchakato huu ukiendelea, inawashauri wamiliki wa mabasi na watoa huduma wote wa usafiri wa umma kuendelea kuzingatia masharti ya leseni zao kwa kutojipangia nauli kinyume na Sheria.
“Adhabu ya kutoza nauli isiyo halali ni Sh250,000 kwa mujibu wa kanuni ya 30 ya Kanuni za Leseni za Usafirishaji (Mabasi ya Abiria) za Mwaka 2020, mamlaka haitasita kuchukua hatua stahiki kwa mmiliki au mtoa huduma yeyote atakayekiuka Sheria na Masharti ya Leseni yake,” imesema.