Kortini akidaiwa kusafirisha bangi

Mshtakiwa, Peter Luoga akitoka kwenye chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kusomewa shtaka linalomkabili. Picha na Pamela achilongola
Muktasari:
- Dereva Peter Luoga amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na shtaka la kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi kilo 372.41
Dar es Salaam. Dereva Peter Luoga amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na shtaka la kusafirisha kilo 372.41za dawa za kulevya aina ya bangi.
Akisoma hati ya mashtaka Wakili Eva Kassa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate amedai mshtakiwa huyo anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi
Kassa amedai Januari, 30, 2016 maeneo ya Makongo juu jijini Dar es Salaam mshtakiwa huyo alikutwa akisafirisha kilo 372.41 za dawa za kulevya aina ya bangi.
"Upelelezi umekamilika tunasubili kuwasilisha taarifa Mahakama Kuu, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa," amedai Kassa.
Hakimu Kabate amesema Luoga anashtakiwa kwa kesi ya uhujumu uchumi hivyo Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo hivyo upelelezi ukikamilika itahamishiwa kwenye Mahakama zenya mamlaka.
Shauri hilo limeahirishwa hadi Desemba 12, 2023 kwa ajili ya kutajwa na mshtakiwa huyo amerudishwa mahabusu.