Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kodi inapokaba koo la mstaafu

Kodi inapokaba koo la mstaafu

Muktasari:

  • Kama ilivyo kwa Walimwengu walio wengi, mzee wetu Mstaafu anakiri kwamba tokea enzi akiwa shule kichwa chake hakijapata kuwa rafiki na somo la hisabati. Miaka yote akili yake ililiona somo hilo kama kituo cha polisi usichopaswa kuwa na mazoea nacho kama hukuwa na shida au ulazima wa kufanya hivyo. Unakipita mbali na maisha yanasonga.

Kama ilivyo kwa Walimwengu walio wengi, mzee wetu Mstaafu anakiri kwamba tokea enzi akiwa shule kichwa chake hakijapata kuwa rafiki na somo la hisabati. Miaka yote akili yake ililiona somo hilo kama kituo cha polisi usichopaswa kuwa na mazoea nacho kama hukuwa na shida au ulazima wa kufanya hivyo. Unakipita mbali na maisha yanasonga.

Mstaafu wetu anajifariji kwamba katika miaka yake 40 ya kumtumikia kafiri ili apate mradi wake na miaka 62 ya kuwa mkazi mwema wa dunia njema hii, hakupata kufikishwa mahali pa kujutia kukosa kujua somo la hesabu na vitengo vyake vyote alivyokuwa aking’ang’aniwa kufundishwa zaidi ya vile tu vya kutoa, kugawanya na kuzidisha!

Naam, kama zile enzi zake za mafunza na makamasi cha Mwalimu kuingia darasani na kuandika ubaoni “50 + Y = 100” na Mwalimu huyo kumchagua Mstaafu wetu ‘atafute Y’ na fito alizoezekwa zisizo za nchi hii alipomjibu Mwalimu alichoona ni bonge la jibu kuwa “Mwalimu, Y niitafutie wapi, si hiyo hapo hapo ubaoni!”

Naam, kichwa cha Mzee wetu hakikupata kuwa rafiki na somo la hesabu, ugonjwa mbao una waathirika wengi tu wa kutosha, si hapa nchini tu bali duniani kote.

Pamoja na kasoro yake hii, linapokuja suala la kufahamu anachostahili au mgawo anaostahili kwenye fungu fulani la pesa, akili yake inakuwa na kasi ya Bombardier! Humdhulumu!

Ndio maana pamoja na kuwa mstaafu kwa miaka karibuni miaka 15 sasa, bado kwenye ndoto zake za mara kwa mara za jinamizi haachi kujiuliza kama kweli alitendewa haki kwenye kifurushi chake cha ustaafu alichopata, baada ya miaka 40 ya ustaafu uliotukuka na uliokuwa na chembe chembe chache tu za utukutu ambazo atakuja kuzibainisha kadri tunavyosomana hapa.

Kuanzia mshahara wake wa mwanzo kabisa maishani wa Sh280, rejea kwa maneno ili kuweka msisitizo zaidi, shilingi MIA MBILI THEMANINI, sio Alfu Mbili MIA Mbili na Themanini! Hakika Mzee wetu mstaafu amekula chumvi nyingi, kama si kubugia kabisa, amekuwa akikatwa kodi ya kila mwezi ya Sh130, mia Moja Thelathini kwa maneno, kwa msisitizo.

Viwango vya kodi yake alivyoambiwa vinapelekwa kwenye akiba yake ya uzeeni kuanzia huko NPF alikoanzia hadi huku PPF alikomalizia ambako anakiri kwamba mshahara wake ulikuwa umeshagonga kwenye malaki kadhaa ambayo makato yake ya kwenda PPF yalikuwa Sh27,100. Zilizokuwa zinajumlishwa kwenye makato ya mshahara wake na kukatwa kodi!

Kimbembe cha ndoto za jinamizi na kumbukizi za mstaafu wetu kinaanzia hapo. Anakumbuka sana kwamba miaka alipostaafu baada ya mwajiri aliyekuwa akimtumikia kumpa ofa ya kupisha teknolojia, akafanya hivyo na tajiri wake akampa kilichoitwa ‘handshake’ (mkono wa heri) ya Sh 23 milioni, ambayo kwa miaka 15 iliyopita ilikuwa si haba, ili akafie mbele na kupisha vijana na teknolojia kuchukua ajira za wahenga.

Kwanza, mwajiri wao aliyekuwa amewaajiri akakata madeni yote waliyokuwa nayo wastaafu wetu, hasa yale ya salary advance ambayo mara nyingi walilazimika kuyachukua kwa ajili ya kusherehekea Eid, Pasaka na Krisimasi mbali na kuwapeleka shule vitegemezi, mwajiri akafyeka yote.

Wastaafu wetu wakaishia kujiuliza kwani kama mwajiri angeamua kuacha kuwakata madeni yao angeingia hasara gani kubwa wakati wao ndio walikuwa wanakwenda kuanza maisha mapya ya kupeleka watoto shule Januari na kusherehekea sikukuu hizo bila salary advance? Mzee wetu na wenzake ndipo wakapata uhakika kuwa ‘muuaji’ si lazima ashike panga ama rungu.

Mzee anakiri tena kuwa hesabu hazijapata kuwa rafiki na kichwa chake lakini kwenye nyaraka zinazohusu pensheni yake akashtuka kuambiwa kuwa kifurushi chake cha pensheni kimekatwa tena shilingi nyingi sana kwa wakati huo 31,000 kama kodi kutoka kwenye pensheni aliyokuwa akikatwa kwenye mshahara wake kwa miaka 40 ya ajira yake iliyotukuka bila utukutu!

Pamoja na kwamba dotcom wake wa nyakati hizi wanaweza kumpiga madongo na kushangaa kwamba mzee anastaafu na kupokea kifurushi cha mafao cha Sh23 milioni lakini badi analalamikia Sh31,000 tu zilizokatwa tena kwenye kifurushi chake cha pensheni

Mstaaafu wetu anakiri kwamba kweli, inawezekana hata yeye mwenyewe kwenye kipindi hicho cha hela, zilikuwa zinatosha si tu kujenga kibanda bali bangaloo kabisa, sasa kwa nini ahoji Sh31,000 zikatwe tena kodi kwenye kifurushi chake mafao wakati kiilishakatwa kodi kwa zaidi ya miaka 40 ya ajira yake kwenye mshahara?

Ni wakati kifurushi cha mafao kilipoanza kuisha na alipoanza kuzisoma upya tena na tena nyaraka zake za kustaafu, ndipo alipoligundua hili na likaanza kuwa sehemu muhimu ya ndoto zake za jinamizi.

Akaanza kupitapita sehemu husika ili kupata ufahamu zaidi ya hili, zaidi ikiwa si kurejeshewa Sh31,000 zake, bali kutaka watakaoliona walifanyie kazi ili ninyi wastaafu watarajiwa mlijue na lisiwasumbue!

Mstaafu wetu anakiri kuwa bado hajaona mantiki ya jumla ya mafao yake ya akiba ya uzeeni kukatwa kodi wakati makato yake ya kuchangia mafao hayo yalikuwa yanakatwa kodi kwenye mshahara wake kwa zaidi ya miaka 40 alipokuwa muajiriwa.

Mstaafu wetu anadhani kuwa itakuwa ni jambo jema iwapo mtaalamu wetu mmoja wa mambo haya akajitokeza na kuliweka sawa hili na likaeleweka kwa mtu kama mstaafu wetu ambaye kichwa chake hakijapata kuwa na urafiki na hisabati.

Haya majibu ya asilimia, credit debit na kadhalika na kadhalika anayopata kutoka kwa wataalamu wasiojua chochote kama yeye yamekuwa yakimchangaya tu na kusababisha ndoto za kumbukizi na jinamizi kuwa sehemu ya ndoto zake miaka 15 baada ya kustaafu. Hili liwekwe sawa kwa Wastaafu watarajiwa wajao. Tusomane Ijumaa ijayo

0754 340606 / 0784 340606