Kizungumkuti usafiri, abiria wakwama Dar

Baadhi ya abiria wakiwa stendi ya Magufuli Mbezi Louis jijini Dar es Salaam ambao wamelazimika kusubiri usafiri wa mchana baada ya kukosa mabasi ya asubuhi.
Muktasari:
- Baadhi ya abiria stendi ya Magufuli Mbezi Louis jijini Dar es Salaam wanaosafiri kwenda mikoani wamelazimika kusubiri usafiri wa mchana baada ya kukosa mabasi ya asubuhi.
Dar es Salaam. Baadhi ya abiria wanaosafiri kwenda mikoani wamekwama katika kituo cha mabasi cha Magufuli kilichopo Mbezi Louis jijini hapa kutokana na ongezeko la wasafiri katika msimu huu wa sikukuu za mwisho wa mwaka.
Mwananchi Digital imefika stendi ya Magufuli Mbezi Louis na kukuta baadhi ya abiria wakiwa wamekosa usafiri huku baadhi yao wakisubiria magari ya mchana.
Abiria anayesafiri kwenda Dodoma, Anna Reuben amesema ameshakata tiketi amasubiri gari inayotoka Dodoma, muda wa kuondoka ni sasa nane mchana.
"Nimefika hapa mapema lakini nikeambiwa magari hakuna nisubiri linaloja ambapo litageuza saa nane," amesema Anna.
Abiria mwingine Abdalh Miraji amesema tangu jana kila anapokata tiketi anaambiwa zimejaa lakini amepata taarifa ya magari yanayoingia mchana na kugeuka hivyo inamlazimu kuondoka nmchana.

Baadhi ya abiria wakiwa stendi ya Magufuli Mbezi Louis jijini Dar es Salaam ambao wamelazimika kusubiri usafiri wa mchana baada ya kukosa mabasi ya asubuhi.
Wakala anayekata tiketi za mabasi yanayofanya safari za Dodoma, Mwanaisha Ally amesema usafiri umeanza kusumbua hasa kwa mikoa ya Kanda ya Kati ikiwemo Morogoro, Dodoma na Singida.
"Unavyooona abiria wengi ni wa Kanda ya kati, lakini usafiri umeanza kusumbua kuna gari tayari tiketi za siku mbili zimejaa, wengi wanasubiri magari yanayokuja na kugeuza," amesema Ally.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Joseph Priscus amesema pamoja na Latra kutangaza kuanza utaratibu wa kusafiri usiku bado haujaanza, isipokuwa muda wa kutoka ni saa 11 alfajiri.
Kila ifikapo mwisho wa mwaka usafiri wa kwenda mikoani umekua ukisumbua hata hivyo Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) imeshatoa mikakati ya kukabiliana na changamoto ya usafiri.
Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na kuongeza mabehewa ya treni pamoja na kutoa vibali vya magari madogo yenye uwezo wa kubeba abiria 30 na kuendelea.
Mikakati mingine iliyotangazwa na Latra ni kuruhusu mabasi kusafiri usiku na mchana msimu huu wa sikukuu ili kupunguza changamoto ya usafiri.
Juhudi za kumpata msemaji wa Latra zinaendelea.