Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kituo cha umahiri matibabu ya saratani kujengwa Dodoma

Muktasari:

  • Dira ya Kituo cha Umahiri cha Matibabu ya Saratani Tanzania na Marekani (TRACE) ni kutoa huduma ya saratani ya kiwango cha juu,   inayosaidiwa na utafiti, elimu na uhamasishaji  unaoendeshwa na taarifa na mawasiliano ya kiteknolojia kutumia akili bandia.

Dar es Salaam.  Kituo cha umahiri cha matibabu ya saratani nchini, kinatarajiwa kujengwa jijini Dodoma baada ya Serikali ya Tanzania kutiliana saini ya makubaliano (MoU) na wawekezaji kutoka Marekani (Global Health Catalyst).

Makubaliano hayo yamefanyika jijini Dodoma leo Februari 6, 2024 katika kikao cha wawekezaji wa nje,  wa ndani na wadau wa maendeleo waliokutana kujadili njia sahihi ya kukabiliana na ugonjwa huo pamoja na teknolojia mpya za matibabu zinazohusisha akili bandia.

Akizungumza baada ya majadiliano hayo, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi amesema lengo la Serikali ni kuimarisha upatikanaji wa huduma za saratani.

Amesema uwekezaji huo unatarajiwa kujenga matumaini kwa jamii iliyoathirika na inayotarajia, lengo likiwa ni kuhakikisha kila anayekutana na changamoto hiyo anapata huduma stahiki.

“Maono ya Rais Samia Suluhu Hassan yanalenga mbali kwa kuzingatia maendeleo endelevu. Kuhakikisha matumizi sahihi ya rasilimali fedha na magonjwa yasiyoambukiza, ikiwamo saratani, kama jamii tunapaswa kuwekeza katika tiba na kinga pia,” amesema Dk Mwinyi.

Amesema hatua zilizoanza ni ujenzi wa miundombinu ya afya na mikakati inayolenga upatikanaji wa huduma za afya kwa wote, kuwekeza rasilimali fedha katika tafiti na kuhakikisha upatikanaji bora wa matibabu.

“Watafiti na wataalamu wa tiba tunaweza kubadilisha taswira ya saratani, tuwe na dhamira ya dhati kufanya kazi bila kuchoka katika kukabiliana na ugonjwa huu, zaidi nipongeze Balozi wa Tanzania nchini Marekani kuwezesha mdahalo huu wa pamoja,” amesema.

Awali, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema Serikali ilikuwa ikitafuta fedha kwa ajili ya kununua mashine ya Proton Therapy, yenye thamani ya Dola milioni tano za Marekani (Sh12 bilioni) ambazo zimepatikana katika mdahalo huo.

Amesema fedha hizo zimeweka msingi wa kuhakikisha Tanzania inapata huduma bora za saratani. “Tumekubaliana na Profesa Win Ngwa tutafanya mdahalo mwingine kutafuta kilichobaki. Wameahidi kuwekeza msaada wa kiufundi kuhakikisha tunakuwa na kituo cha umahiri cha matibabu ya saratani.

“Tunaamini tukiwa na kituo hiki tutapunguza gharama ya kupeleka wagonjwa nje, mwaka 2022 tumetumia Sh3.1 bilioni kutibu saratani nje ya nchi kati ya Sh4.8 bilioni za wagonjwa walitibiwa nje, hii inatupa ishara kwamba kituo hiki kitaokoa fedha nyingi,” amesema Ummy.

Amesema hilo limeonekana katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ambayo mwaka 2018 ilifunga mashine za Linac zinazotakiwa kutumika kwa miaka 10.

 “Zinatakiwa kutibu wagonjwa 30 kwa siku, lakini zinatibu wagonjwa 70, uwezo wake wa kuishi umepungua mpaka kufikia miaka sita kwa kuwa mashine inafanya kazi mara tatu ya inavyotakiwa.

 “Mzigo wa saratani upo nchi za kusini mwa jangwa la Sahara, Afrika takwimu zinaonyesha miaka sita kutoka sasa vifo vitokanavyo na saratani vitaongezeka kutoka 500,000 mpaka milioni moja. Rais Samia alipoenda Marekani ndipo akaja na programu hii,” amesema.

Ametaja saratani inayoongoza ni ya mlango wa kizazi kwa asilimia 25, matiti asilimia 10, tezi dume asilimia 9, mfumo wa chakula asilimia 6.5 na saratani nyinginezo.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Raphael Maganga amesema atahamasisha wawekezaji nchini kuungana na mpango huo, ili kuhakikisha afya za Watanzania zinaimarika.

Mkurugenzi wa Huduma za Tiba kutoka Wizara ya Afya, Profesa Paschal Ruggajo amesema Tanzania ina uhaba wa madaktari bingwa wa saratani, inakadiriwa kutakuwa na ongezeko la wagonjwa wa saratani duniani kutoka 500,000 hadi milioni moja ifikapo 2030.