Kisukari chatajwa sababu kuu magonjwa ya figo
Muktasari:
- Ugonjwa wa kisukari umetajwa kuwa kisababishi kikubw katika kusababisha magonjwa ya figo duniani.
Dar es Salaam. Wakati dunia ikiadhimisha wiki ya ugonjwa wa kisukari, ugonjwa huo umetajwa kuwa kisababishi kikuu cha magonjwa ya figo duniani.
Akizungumza katika mkutano uliowakutanisha wanachama wa Chama cha Kisukari Tanzania pamoja na watu waishio na ugonjwa huo leo, Novemba 17, 2023 jijini hapa, Rais wa Chama cha Wataalamu wa Figo Tanzania na Daktari katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Onesmo Kisanga amesema kisukari umekuwa kinara katika kusababisha magonjwa ya figo kote ulimwenguni.
Dk Kisanga amesema takribani asilimia 44 ya wagonjwa wa figo wametokana na kupata kisukari, hivyo juhudi zaidi zinahitajika kuzuia ugonjwa huo ambao huja na madhara mengi katika mwili wa binadamu.
"Muhimu ni kuzuia kwa sababu ugonjwa wa kisukari una hatua tano ambapo katika hatua mbili za mwanzo inawezekana kudhibiti magonjwa ya figo na ikifika katika hatua ya nne na tano inakuwa vigumu kuzuia,” amesema Dk Kisanga.
Amesema lengo kuu la chama hicho ni kubadili mfumo wa maisha ya watu, ikiwemo kufanya vipimo mara kwa mara ili kutambua afya zao na kujua hatua za mapema za kuchukua pindi mtu atakapogundulika kuwa na kisukari.
"Tuna wagonjwa 200 wanaosafishwa damu kila siku, wagonjwa 40 mpaka 50 huja kliniki kila siku, wakati 20 wakilazwa kila siku kutokana na magonjwa ya figo. Pia tuna wagonjwa wengi walioko katika uangalizi maalumu," amesema Dk Kisanga.
Kwa upande wake, Dk Omary Ubuguyu, mkurugenzi msaidizi magonjwa yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya, amesema udhibiti wa kisukari na magonjwa mengine yasiyoambukiza unahitaji mfumo maalumu wa maisha ikiwemo kupata maelekezo kutoka kwa wataalamu ikiwemo kufahamishwa kuhusu dalili za magonjwa hayo na umuhimu wa kupima na kuzingatia mfumo bora wa maisha kama vile lishe na kufanya mazoezi.
Akizungumzia uhusiano uliopo kati ya kisukari na magonjwa ya macho, amesema ugonjwa huo huathiri mishipa ya damu katika mwili ikiwemo macho, hivyo ndipo magonjwa ya macho huanzia.
"Watu wengi huwa wanachelewa kwenda kupima kisukari, kwani si rahisi kutambua dalili zake, ndani ya miaka mitatu mpaka mitano utakuta mtu ameshaanza kuathirika katika viungo kama macho, figo na ubongo," amesema Dk Ubuguyu.
Ameeleza kati ya wagongwa 100, wagonjwa 30 hupata tatizo la macho baada ya mishipa iliyoko kwenye macho kuziba kutokana na kiwango kikubwa cha sukari mwilini.
Aidha, amesema mazoezi ni moja ya njia za kupunguza kiwango cha sukari mwilini, kwani husaidia kukuza misuli ambayo hunyonya kiwango cha sukari kwenye damu pale insulini inapokuwa imeshindwa kumeng'enya sukari.
Naye Dk Aniceth Muchunguzi ambaye anaishi na kisukari kwa zaidi ya miaka 10 sasa, amesema licha ya kugundulika kuwa na ugonjwa huo, haijamzuia kutimiza ndoto zake za kuwa daktari.
Dk Muchunguzi ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wanaoishi na kisukari Tanzania, amesema jamii haifahamu kuhusu uwepo wa ugonjwa huo kwa watoto na vijana.
"Ni changamoto sana, kwani hii inachangia watoto wengi na vijana kupoteza maisha kabla hata hawajagundulika, ni wakati wa jamii kufahamu mbali na aina ya pili ya kisukari ambayo wengi wanaifahamu, ipo aina ya kwanza ambayo huwapata watoto na vijana," amesema Dk Muchunguzi.
Amesema kisukari aina ya kwanza mara nyingi hutokea kutokana na kinga ya mwili kushambulia kongosho, hivyo kushindwa kutengeneza insulini ambayo ndiyo hudhibiti kiwango cha sukari mwilini.
Amesema dalili za kisukari aina ya kwanza hufanana na zile za aina ya pili ambapo huhusisha kupungua uzito, kupata kiu na kwenda haja ndogo mara kwa mara, hivyo ni muhimu kufika hospital pindi kijana au mtoto anapopata dalili kama hizo.
Amesema mpaka sasa duniani kuna waathirika zaidi ya milioni 10 ambao wamepata kisukari aina ya kwanza.
"Tunahitaji msaada mkubwa, kwani insulini ya bandia ambayo tunatumia vijana na watoto pamoja na vifaa tiba ni gharama sana, ikilinganishwa na wale wenye aina ya pili ya kisukari ambapo kwetu sisi mtu anaweza kutumia kati ya Sh2 milioni mpaka Sh 3 milioni kwa mwaka," amesema.