Kissenge atamani huduma ya intaneti ipatikane kila kijiji

Mkurugenzi wa Mipango na Uhandisi Tigo, Semvua Kiseenge
Muktasari:
- Amesema intaneti ina nafasi kubwa katika maendeleo ya nchi, hivyo inapaswa kuwafikia watu wote kwa ajili ya kufanikisha shughuli zao na si wengine hadi wasafiri kwenda sehemu inapopatikana huduma hiyo.
Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Mipango na Uhandisi Kampuni ya Huduma ya Mawasiliano ya Tigo, Semvua Kissenge amesema huduma ya mtandao wa intaneti inapaswa kufika maeneo yote ikiwemo vijijini ili wananchi wapate maendeleo ya haraka kama wenzao waliopo mijini.
Amesema intaneti ina nafasi kubwa katika maendeleo ya nchi, hivyo inapaswa kuwafikia watu wote kwa ajili ya kufanikisha shughuli zao na si wengine hadi wasafiri kwenda sehemu inapopatikana huduma hiyo.
Kissenge, ameyasema hayo jana Jumatano Julai 24, 2024 wakati akichangia mada kwenye mjadala wa Mwananchi Space ambao hufanyika kila Jumatano kupitia mtandao wa X, mada ya leo ikihoji, ‘Ipi nafasi ya huduma za intaneti katika maendeleo ya nchi.
Kutokana na hilo, Kissenge amesema wanashirikiana na Serikali kuhakikisha huduma hiyo inawafikia watu kila eneo kwa ajili ya ustawi wa maendeleo.
“Maendeleo si Dar tu au maeneo ya mijini, bali watu wote wanapaswa kupata intaneti ili kurahisisha huduma na kupata fursa kama wanazozipata watu wa mijini kwa ubora uleule,” amesema Kissenge.
Akichangia katika mjadala huo, Mhariri wa Uchumi wa Mwananchi, Ephrahim Bahemu ameitaja huduma hiyo kama sehemu ya maisha na maendeleo ya nchi kwa ujumla, kutokana na umuhimu wake katika nyanja za uchumi, siasa, biashara na kijamii.
Amesema nafasi ya intaneti katika maendeleo ya Taifa na kwa mtu mmoja mmoja, taasisi na jamii ni kubwa na hitaji la msingi la binadamu kwa sasa.
“zamani miaka ya 1990 kulikuwa na mtandao wa 2G ambao tumeenda nao hadi sasa tupo 5G huku wengine wakitazamia 6G, mapinduzi yote haya yanaongeza kasi ya mawasiliano na kuongeza ufanisi katika shughuli mbalimbali.
“Umuhimu wake unakuja pale inaporahisisha shughuli za kibiashara, kilimo, afya, taarifa za hali ya hewa, uchumi na hata siasa. Mtandao wa intaneti umeongeza ukuaji wa biashara kwa kufanya utafiti na kupata ujuzi kupitia mtandao,” amesema Bahemu.