Kinana aahidi kusimamia haki, masilahi ya wananchi

Muktasari:
- Kinana awaahidi wananchi wa Mkoa wa Mara kuwa atatekeleza majukumu yake kwa busara na kusimamia haki katika kufanya maamuzi kwa masilahi ya wananchi ili kuona wanapata maendeleo wanayohitaji.
Mara. Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM (Bara), Abdulrahman Kinana ameahidi kuendelea kutumia busara katika nafasi hiyo kwa kusimamia haki na kufanya maamuzi sahihi kwa masilahi ya wananchi.
Kauli hiyo aliitoa alipokuwa akijenga hoja yake aliyoieleza mbele ya kadamnasi kuwa bado Watanzania wana imani kubwa na chama hicho pamoja na viongozi wake, hivyo yeye kama mmoja wa viongozi wa ngazi ya juu hatawaangusha.
Amesema hayo akizungumza leo Aprili 13, 2024 baada ya kupokewa katika Kijiji cha Robanda-Ikoma Wilaya Serengeti, alikoenda kuanza ziara ya siku sita ya kusikiliza kero za wananchi na kufanya vikao vya ndani na viongozi wa chama hicho.
"Kwanza nawashukuru kwa mapokezi mazuri, nawashukuru wananchi wa Ikoma kwa kunipa heshima ya uchifu, uchifu unaenda na mambo mengi ikiwemo busara, kuwaongeza watu vizuri,"
"Nitumie fursa hii kuwahakikishia kwa nafasi niliyonayo nitaendelea kutumia busara katika kutenda haki kwa masilahi ya chama changu na kuona wananchi wanapata maendeleo wanayoyataka," amesema.
Baada ya kutua Kijiji cha Ikoma kilichopo kwenye Kata ya Mugumu, Kinana alipewa heshima ya uchifu na wananchi hao na kumuita jina la 'Ikoma Marasi.
Awali akizungumza wakati anampa hadi ya uchifu huo, Mzee maarufu wa Kijiji cha Ikoma, Kenyatta Mosoko ametoa tafsiri ya Chifu Marasi kuwa ni kiongozi mwenye hekima na busara.
"Ni Jina lenye heshima kubwa katika hili kabila letu, chifu wa kwanza wa kabila hili aliitwa Ikoma marais, Mwalimu Julius Nyerere alipokuwa kwenye harakati ya kutafuta uhuru alikuja kijiji hiki na kusimikwa uchifu, akapewa baraka za kwenda kufanya harakati za kusaka uhuru," amesema.
Mosoko amesema wana imani na kiongozi huyo huku akieleza wamewiwa kumpatia jina hilo ili katika majukumu yake azingatie sifa hizo katika kuwatumikia wananchi.