Kinana akerwa na viongozi wabovu

Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana kwenye Viwanja vya People’s Mjini Singida wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya chama hicho
Muktasari:
Kinana alisema hayo jana mjini Singida wakati akihutubia mamia ya wana CCM na wananchi ikiwa ni hitimisho la ziara ya siku nane mkoani humo.
Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana amesema bado kuna viongozi na watendaji ambao hawatekelezi majukumu yao lakini hawachukuliwi hatua zinazostahili na mamlaka za juu.
Kinana alisema hayo jana mjini Singida wakati akihutubia mamia ya wana CCM na wananchi ikiwa ni hitimisho la ziara ya siku nane mkoani humo.
Alisema bado kuna watendaji wachache katika Serikali ya CCM ambao wanashindwa kutekeleza majukumu yao badala yake wamebobea kwa rushwa na upendeleo.
Kinana alisema watendaji hao wanachukua muda mrefu kushughulikia matatizo ya wananchi bila sababu za msingi.
Alisema kuna watendaji ambao wakifanya vibaya katika utendaji wao wanahamishiwa katika idara nyingine kwa kisingizio cha utawala bora.
“Haiwezekani mtu anafanya makosa ya kiutendaji halafu anahamishiwa katika idara nyingine kwa kisingizio cha utawala bora, ni lazima hatua zichukuliwe kulingana na makosa wanayoyafanya,” alisema.
Akizungumzia uhai wa chama hicho, Kinana alisema wakati wapinzani wanapita katika mikoa mbalimbali wakitukana, wao wanapita kukagua miradi ya maendeleo.
“Hata kama wapinzani wakitutukana hawawezi kututoa katika ajenda yetu ya kuleta maendeleo kwa sababu katika uchaguzi wa mwaka 2015 tutaulizwa utekelezaji wa ilani ya chama na siyo aina ya matusi tuliyowatukana wapinzani,” alisema.