Kina Mwabukusi wazuiwa kuandamana

Muktasari:
- Mwabukusi amesema baada ya kufikishwa ofisi ya kamanda wa Polisi mkoani humo walikabidhiwa barua ya kuzuia maandamano akiahidi kukata rufaa.
Mbeya. Mwanasheria wa kujitegemea na mwanaharakati, Boniface Mwabukusi amesema pamoja na kupokea barua ya jeshi la Polisi kuzuia maandamano waliyoandaa kufanyika Novemba 9, wanakusudia kukata rufaa kwa Waziri mwenye dhamana.
Mwabukusi na wenzake akiwamo mwanasiasa Dk Wilbroad Slaa na Mpaluka Nyagali maarufu kwa jina la Mdude, walitangaza mapema kufanya maandamano ya amani watakayozindulia jijini Mbeya yakilenga kupinga uwekezaji kwenye bandari.
Akizungumza na Mwananchi leo Novemba 3, Mwabukusi amesema wamepokea barua kutoka kwa kamanda wa jeshi la polisi mkoani humo, Benjamini Kuzaga kuzuia maandamano hayo.
Amesema pamoja na barua hiyo, lakini sheria inawaruhusu kukata rufaa kuanzia leo kwa waziri mwenye dhamana ili kufanikisha azma yao kwa mujibu wa sheria.
Kuhusu kukamatwa na kujojiwa na Jeshi la Polisi pamoja na waandishi wa habari wanne, mwanasheria huyo amesema baada ya kikao na waandishi walichukuliwa na askari polisi hadi ofisi ya Kamanda wa Polisi ambapo baada ya kufika walikabidhiwa barua hiyo na si mahojiano yoyote.
"Kwa kuwa sheria iko wazi tutakata rufaa kwa waziri mwenye dhamana kuhakikisha tunapata haki yetu, tulipofikishwa pale kwa RPC (Kamanda wa Polisi Mkoa) walisema wanataka kutupatia barua ya kuzuia maandamano na kujua ofisi zetu hatukuhojiwa chochote" amesema Mwabukusi.
Mmoja wa waandishi wa habari waliodaiwa kukamatwa, Ahadi Mtweve amesema baada ya kikao na Mwabukusi walizingirwa na askari kama watano ambao waliondoka nao hadi ofisi ya kamanda wa Polisi.
"Kwa hiyo hatukuhojiwa chochote badala yake tulipofika kamanda alimuagiza OCD kuwapa barua kina Mwabukusi kisha kuambiwa tuondoke" amesema Mtweve.
Alipotafutwa kamanda Kuzaga amesema yupo msibani akieleza atumiwe ujumbe na mwandishi alipofanya hivyo hakujibu chochote.
Katika hatua nyungine, vuguvugu la Sauti ya Watanzania (SyW), limetoa tamko lake leo likisema ukamatwaji wa wanaharakati huo ni unyanyasaji wa Jeshi la Polisi kwa wanaopinga Makubaliano ya uendeshaji wa bandari (IGA) kati ya Serikali ya Tanzania na ile ya Dubai.
“Maandamano ya kitaifa yalipangwa kuanzia Mbeya Alhamisi Novemba 9, 2023. Mambo mengine ambayo SyW inayopambania ni kuitaka Serikali kuacha tabia ya kuwazuia Watanzania wanaotaka kuandikwa kwa Katiba mpya na wanaopinga ukiukwaji wa haki za binadamu,” imesema sehemu ya tamko hilo.