Kilimo mazao mseto kilivyosaidia kupambana na tembo

Muktasari:
- Wananchi washauriwa kutumia mbinu mchanganyiko kukabiliana na tembo kutokana na hulka ya mnyama huyo kubadili tabia.
Iringa. Kutokana na mnyama tembo kuwa na tabia ya kubadilika, wananchi waishio maeneo yenye wanyama hao wameshauriwa kulima mazao mseto ili kuepukana na uharibifu unaoweza kusababishwa nao.
Hilo linatokana na kilimo cha mazao mseto yasiyo rafiki kwa tembo kuonesha mafanikio kama mbinu mojawapo ya kupambana na wanyama wakali na waharibifu.
Akizungumza na viongozi kutoka Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Wizara ya Maliasili na Utalii, wakati wa kufanya tathmini na ufuatiliaji wa matokeo ya mbinu hizo leo Jumatatu, Juni 30, 2025, mkazi wa Kijiji cha Idodi, Nasri Makasi amesema mbinu walizofundishwa zimewasaidia kukabiliana na wanyama waharibifu.

Mbinu hizo amezitaja ikiwemo kupanda vitunguu na ufuta wa miiba kuzunguka mashamba yao imeonekana kufanya kazi kwani wamefanikiwa kuvuna kutokana na tembo kutokula mazao hayo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mafuruto, Meshack Sanya amesema katika eneo lao wametundika mizinga ya nyuki katika lango la tembo kuzunguka eneo lao la kilimo.
Ameongeza katika upande ambao wakulima wa kijiji hicho hawakuweka mizinga ya nyuki wengi wao wameambulia mavuno ya gunia moja kwa heka na wengine kutovuna chochote kutokana na mashamba yao kuvamiwa na tembo.
Aidha, wameiomba Serikali na wadau wa maendeleo kuendelea kuwafadhili upatikanaji wa mizinga ya kisasa ambayo wamesema wanashindwa kumudu gharama zake.
Sambamba na kuwasaidia mbegu za mazao yasiyo rafiki kwa tembo kama vile vitunguu, ufuta wa miiba ambayo wakilima wanapata mavuno pamoja na soko la uhakika na hivyo kuwanyanyua kiuchumi.
Akizungumza wakati wa tathmini hiyo, Meneja mradi wa kupambana na wanyama wakali na biashara haramu ya nyara, Theotimos Rwegasira amewashauri wananchi hao kutumia mbinu mchanganyiko ikiwemo matumizi ya mabomu baridi.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Shirika la Mpango wa Maendeleo Duniani (UNDP), Tulalula Bangu amesema uzio wa nyuki ni mojawapo ya mbinu zilizoonesha mafanikio makubwa katika kukabiliana na tembo.