Kauli ya Trump yatikisa utendaji NGOs Geita

Muktasari:
- Januari 2025 Rais wa Marekani, Donald Trump alisitisha zaidi ya asilimia 90 ya ufadhili wa kimataifa kupitia Shirika la USAID, uamuzi huo uliathiri zaidi ya miradi 5,200 duniani kote.
Geita. Zaidi ya miradi 10 ya afya na maendeleo iliyokuwa ikitekelezwa na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) mkoani Geita, imeathiriwa, ikiwa ni pamoja na kusimamishwa kwa huduma muhimu ya programu ya PERFAR ya kinga dhidi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).
Hii ni baada ya kusitishwa kwa ufadhili kutoka kwa wafadhili wa kimataifa.
Akisoma taarifa ya mwaka ya mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) mkoani Geita, Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Nelico, Alex Majogoro amesema kutokana na uamuzi wa Rais wa Marekani, Donald Trump kusitisha asilimia 90 ya ufadhili kupitia USAID, kumesababisha mashirika mengi kuyumba.
“Mbali na kusitishwa kwa programu ya PERFAR, miradi mingine iliyositishwa ni pamoja na kampeni za kupambana na Malaria pamoja na huduma za msingi za afya,” amesema Majogoro.
Amesema mashirika mengi yanategemea ufadhili kutoka kwa wafadhili wa kimataifa, hivyo kukosekana kwa fedha hizo kumesababisha kupungua kwa huduma za afya, kusimama kwa baadhi ya miradi ya maendeleo na kuleta pengo kubwa kwenye maeneo yaliyokuwa yanategemea misaada hiyo.
Amesema baadhi ya mashirika mkoani humo yamelazimika kupunguza wafanyakazi kwa zaidi ya asilimia 50, huku mengine yakilazimika kupunguza mishahara ya wafanyakazi ili kukabiliana na changamoto ya utegemezi wa ufadhili.
Changamoto nyingine ni ugumu wa kupata misamaha ya kodi, licha ya mashirika mengi kuwasilisha maombi ya kutambuliwa kama taasisi za hisani.
Kwa mujibu wa NaCONGO, mashirika mengi hasa yale machanga yameshindwa kutekeleza majukumu yake, huku mengine yakifunga ofisi kutokana na kukosa ufadhili.
Mwenyekiti wa NaCONGO mkoani humo, Paulina Alex amesema pamoja na changamoto hizo, lakini mashirika yasiyo ya kiserikali yamefanikiwa kutekeleza afua mbalimbali, ikiwemo ulinzi wa mtoto na haki za binadamu, mapambano dhidi ya mila potofu na ndoa za utotoni, mapambano dhidi ya dawa za kulevya, afya, elimu, mazingira, pamoja na kutoa msaada wa kisheria.
Amesema miradi zaidi ya 50 imetekelezwa mkoani Geita na vikundi zaidi ya 300 vya wanawake na vijana vimewezeshwa kiuchumi kupitia mikopo.
“Kupitia mashirika haya, vituo vya afya zaidi ya 10 vimekarabatiwa na kupatiwa vifaa. Wananchi 480 wamepatiwa msaada wa kisheria, lakini pia kwenye sekta ya ajira, mashirika haya 70 yaliyopo hapa mkoani kwetu yametoa ajira kwa watu 500,” amesema Alex.
Takwimu zinaonyesha mashirika yasiyo ya kiserikali yamewekeza Sh7.2 bilioni kwa mwaka 2024/25 katika sekta ya afya, elimu, kilimo, ustawi wa jamii, mazingira na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Geita, Deodatus Kayango, akifungua mkutano huo, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na mashirika hayo, akisema,“Serikali inatambua kazi kubwa inayofanywa na NGOs katika kuwaletea wananchi maendeleo.”
Amesema lengo la mkutano huo ni kukutana na mashirika yote yasiyo ya kiserikali ili kujadiliana kwa pamoja kuhusu masuala mbalimbali kwa ajili ya kuboresha huduma na kuimarisha ushirikiano katika kutekeleza miradi na huduma mbalimbali za kijamii.
Akizungumzia uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, mwakilishi huyo wa mkuu wa koa ameyataka mashirika yaliyopewa idhini ya kutoa elimu ya uraia kwa wananchi kuzingatia uzalendo.
“Tunaelekea kwenye uchaguzi. Mashirika yasiyo ya kiserikali yaliyopata idhini ya kutoa elimu, toeni elimu ya uraia kwa kuzingatia uzalendo. Elimu ya uraia ikitolewa vizuri, jamii itapata mwamko mzuri na kujitokeza kuchagua viongozi bora,” amesema Kayango.