Prime
Kilichowaponza vigogo wawili kusimamishwa kazi Dawasa

Muktasari:
- Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, ametoa agizo hilo baada ya ripoti ya uchunguzi iliyoonyesha miundombinu duni na usimamizi mbovu wa uzalishaji na usambazaji maji Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Uamuzi wa kusimamishwa kazi kwa watendaji wawili wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), akiwemo Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu, Kiula Kingu umechochewa na sababu mbalimbali, ikiwemo ufuatiliaji duni wa miundombinu ya maji.
Kiula pamoja na Shaban Mkwanywe, mkurugenzi wa uzalishaji na usambazaji maji wa Dawasa, walisimamishwa kwa maelekezo ya Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kupisha uchunguzi wa utendaji usioridhisha na kusababisha huduma ya maji kutopatikana kila wakati katika eneo wanalolisimamia.
Hatua hiyo ilianzia kwenye ripoti iliyowasilishwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mwajuma Waziri aliyoitoa mbele ya Waziri Aweso, wajumbe wa bodi, menejimenti na kamati ya siasa ya CCM mkoa wa Dar es Salaam.
Ripoti hiyo ilitokana na ziara ya siku mbili ya Mwajuma aliyoifanya katika maeneo mbalimbali ya mitambo ya kuzalisha maji ya Ruvu Juu, Ruvu Chini pamoja na bomba kuu linalosafirisha maji kutoka kwenye vyanzo hadi kwenye matenki.
Ziara hiyo ilifanyika ikiwa ni takribani wiki moja tangu gazeti hili liripoti kwa kina hali duni ya upatikanaji wa maji katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.
Kadhia hiyo ilimfanya Naibu Waziri wa Maji, Kundo Mathew kufanya ziara Machi 20, 2024 maeneo mbalimbali kujionea hali hiyo akieleza ameagizwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na baadaye Serikali kuchimba kuanza visima kwenye maeneo yaliyotajwa kukithiri tatizo la maji.
Jana Waziri Aweso naye alifanya ziara Dawasa na kabla ya kupokea ripoti hiyo ya katibu mkuu, alitembelea tenki la Chuo Kikuu Ardhi, Luguruni, Mshikamano na Tegeta A. Timu nyingine ikiongozwa na wajumbe wa bodi ilikwenda maeneo ya Kigamboni.
Baada ya kurejeandipo Katibu mkuu Mwajuma aliwasilisha ripoti ya kile alichokibaini kwenye ziara yake, ambacho kilishabihiana na walichoshuhudia wenyewe jana.
"Nilianza Ruvu Juu sehemu ambayo kwa siku inapaswa kuzalisha lita milioni 180, nilikuta baadhi ya pampu hazifanyi kazi na maji mengi yakimwagika chini na nilijiuliza tunapataje lita milioni 180," alihoji.
Alisema pia alikagua bomba kuu linalosafirisha maji hadi kwenye matenki, akabaini kuna sehemu kulipaswa kufungwa 'flow mitter' zinazoonyesha kiwango cha maji, lakini zimetolewa na baadhi ya watu wameanzisha makazi.
"Inaonekana hakuna anayechukua hatua ya kufuatilia maeneo hayo na baadhi ya chemba maji mengi yanapotea, hali hiyo si kwenye bomba kuu tu, hata huku mijini chemba hizo watu wamezigeuza visima," alisema.
Katibu mkuu huyo alisema walifika baadhi ya maeneo watu wameanzisha mashamba ya umwagiliaji wakitumia maji ya taasisi hiyo na baada ya kuwaona wakifanya shughuli hizo, walikimbia.
"Eneo la Sinza Mugabe kuna chemba watu hadi wamegeuza kisima, yaani sehemu ya kuchota maji kwa matumizi yao binafsi na hakuna hatua zilizochulia," alisema
Alisema uwekezaji wa Serikali na hali ya mitambo ilivyo katika eneo la Ruvu Chini, wanatakiwa kuzalisha lita milioni 260 za maji kwa siku, lakini pampu zake nyingine hazifanyi kazi.
"Serikali imefanya uwekezaji unaotakiwa kuzalisha lita milioni 590 kwa siku, lakini ukiangalia taarifa ya miezi sita ya vyanzo vyote, ikiwemo Kigamboni kwa siku tunazalisha lita milioni 320, maana yake tunadaiwa lita milioni 270 kufikia 590," alisema.
Katika lita hizo milioni 320 wanazozalisha, alisema kwa siku wanauza lita milioni 210 kulingana na taarifa ya miezi sita iliyopita, maana yake wanapoteza lita milioni 110.
"Tukipiga mahesabu kiwango cha lita milioni 279 wanachodaiwa na kuongeza lita milioni 110 wanazopoteza, kama zingekuwa zinapatikana tungeweza kuhudumia idadi ya wananchi milioni sita," alisema.
Katibu mkuu huyo alisema kwenye hitimisho kuwa wamebaini tatizo lililopo ni uzalishaji wa maji kutokana na ubovu wa mitambo.
"Pili, tumejifundisha na kuona usimamizi na hapa kuna kutokuwajibika kwa watendaji, kuona wanajionea, lakini shida katika kufanya uamuzi," alisema.
Tatu, kuna shida katika kuwaunganishia wateja huduma, huku kukiwa na maombi mengi na mengine wameshapokea fedha, lakini huduma haijawafikia walengwa.
"Mwaka mzima walioomba kuunganishiwa huduma wapo 55,547 na waliolipia wanasubiri kuunganishiwa maji wapo 6,891," alisema.
Alisema kingine walichokibaini ni kuwa watumishi wa taasisi hiyo wamejiachia kiasi kwamba hawajui namna ya kutekeleza majukumu yao.
"Watendaji wamekuwa wakiongea uongo, kila mtumishi unayemuuliza kitu anakupa majibu tofauti, wakati mwingine hadi waliopewa kusimamia nafasi fulani," alisema.
Kibano cha Aweso
Baada ya katibu mkuu kuwasilisha taarifa yake, Aweso aliyeonekana kukerwa, alianza kwa kumuuliza Shaban kwamba katibu mkuu alipofanya ziara siku mbili katika kituo chake cha kazi alikuwa wapi?
Shaban: Sikwepo mkuu
Waziri Aweso: Anayesimamia kitengo cha shughuli za matengenezo ya mitambo ni nani?
Shaban: Ni mimi mheshimiwa
Waziri Aweso: Inakuwaje katibu mkuu anafanya ziara ya siku mbili katika eneo lako la kazi na hujashiriki.
Shaban: Mheshimiwa tulipewa maelekezo na mkuu kwamba katibu mkuu anataka watu wa operesheni tu.
Waziri Aweso: Mtendaji mkuu wa operesheni ni nani?
Shaban: Ni mimi na anapokuja kiongozi wangu mkuu katika ukaguzi natakiwa kuwepo.
Waziri Aweso: Ofisa Mtendaji Mkuu (Kiula Kingu) ulikuwepo?
Kingu: Sikwepo
Waziri Aweso: Mhandisi Shaban tumeenda wote Chuo cha Ardhi kuangalia ujazo wa maji kwenye tanki la kuhifadhi lita milioni 40, yalikwepo?
Shaban: Hayakuwepo.
Waziri Aweso: Tulienda kwenye flow mitter zinafanya kazi?
Shaban: Hazifanyi kazi.
Waziri Aweso: Unapokuja mtu ameandika kwenye daftari kiwango cha maji yanayozalishwa anakuwa ametoa wapi kama flow mitter hazisomi?
Shaban: Sielewi anakuwa ametoa wapi.
Waziri Aweso: Tumeenda Kibamba kuangalia tenki lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 10, tumeyaona?
Shaban: Hakuna maji kabisa, hayasomi.
Waziri Aweso: Hivi kama maji hakuna malalamiko hayatakuwepo?
Shaban: Yatakuwepo.
Waziri Aweso: Ili tupate maji kuna mambo ya msingi lazima yawepo, je maji yapo?
Shabani: Maji yapo.
Waziri Aweso: Je, umeme upo?
Shaban: Umeme upo.
Baada ya hapo, Waziri Aweso alimwomba mwenyekiti wa bodi hiyo, Jenerali mstaafu, Davis Mamunyange azungumze, naye alisema katika ziara waliyofanya maeneo machache waliyotembelea imewapa picha sahihi ya halisi ya huduma ya maji.
"Hali ya utoaji huduma ya maji kwa kweli ni mbaya na ziara aliyofanya katibu mkuu ilikuwa ya kushtukiza. Ziara hizo zinafaa zaidi kuliko zile rasmi watendaji wanakuwa wamejiandaa," alisema.
"Mimi sikutarajia na wajumbe wenzangu wa bodi tutakuta hali hiyo, imetushtua. Ni jambo ambalo hatukulitarajia na hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa," alisema Jenerali Mwamunyange.
Alisema kama bodi watakaa kikao na kufanyia kazi maagizo yaliyotolewa na waziri huyo kwa kuzingatia utaratibu wa bodi hiyo.
“Lazima uamuzi nichukue kwa sababu napokea malalamiko mengi kutoka Dar es Salaam na kama mnavyojua Dar es Salaam kama haina maji hatupati pa kuhemea.”
Ndipo akaiomba bodi ya Dawasa wakubali kumsimamisha Kaimu Ofisi Mtendaji Mkuu, Kingu pamoja na Mhandisi Shaban kupisha uchunguzi na kuwa wanapaswa kutoa maelezo kwa bodi kwa nini maji kwenye matenki hakuna, ilihali kwenye vyanzo yapo, umeme upo na pampu zinafanya kazi.
Alisema katika kipindi ambacho wamesimamishwa viongozi hao, Dawasa itakuwa chini ya Wizara ya Maji.