Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kikwete: Uchaguzi 2025 ni fursa kuonyesha demokrasia

Muktasari:

  • Rais mstaafu Jakaya Kikwete amesema Uchaguzi Mkuu wa 2025 ni fursa kwa Watanzania kuchagua viongozi wanaowataka, lakini pia kuendelea kuonyesha uwezo wa Tanzania katika chaguzi za haki, amani na za kuaminika, bila hofu wala upendeleo.

Dar es Salaam. Rais mstaafu, Jakaya Kikwete amesema hila, ulaghai na ujanja visitumike katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025.

Amesema uchaguzi huo wa kuwapata Rais, wabunge na madiwani ni fursa kwa Tanzania kuionyesha dunia kwamba ina uwezo wa kuendesha mambo yake kidemokrasia.

Kikwete amebainisha hayo leo Jumamosi Juni 20, 2025 kwenye kongamano la mawakili wa Serikali lililofanyika jijini Dar es Salaam, likihudhuriwa na wadau mbalimbali katika tasnia ya sheria. Kongamano hilo limeandaliwa na Chama cha Mawakili wa Serikali.

Kaulimbiu ya kongamano hilo inasema: “Demokrasia kwa vitendo, sheria na uwajibikaji wa uchaguzi mkuu wa 2025.” Ujumbe huo unalenga kuwakumbusha wadau wa uchaguzi huo wajibu wao na umuhimu wa kuzingatia sheria.

Kikwete aliyekuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo amepongeza kaulimbiu hiyo akosema imekuja wakati Taifa likielekea kwenye uchaguzi mkuu, akieleza namna demokrasia ya Tanzania ilivyopita katika nyakati tofauti.

Amesema uchaguzi wa mwaka huu ni fursa kwa Watanzania kuchagua viongozi wanaowataka, lakini pia kuendelea kuonyesha uwezo wa Tanzania katika chaguzi za haki, amani na za kuaminika, bila hofu wala upendeleo.

Vilevile, ni fursa ya kuyafanya mambo yao kuwa mazuri na kuwafanya Watanzania wenyewe waridhike kwamba uchaguzi umeendeshwa vizuri na wananchi wamepata nafasi ya kuchagua viongozi wanaowataka.

“Tukiepuka hila, ujanja, ulaghai, tutakuwa na uchaguzi ambao matokeo yake yatakuwa na sifa hiyo. Tukifanya vinginevyo, basi tutakuwa tumemaliza. Watatangazwa walioshinda na walioshindwa, lakini bado hata aliyeshinda mwenyewe anashangaa ameshindaje,” amesema na kuongeza:

“Kukikosekana uwazi, kuheshimu sheria, kuheshimu taratibu, tutafika huko na sifa hiyo haitakuwa sifa nzuri kwa demokrasia ya Tanzania, ambayo inahesabiwa kwamba ni mfano mzuri wa kubadilishana uongozi na mfano mzuri wa kuendesha mambo kidemokrasia.”

Kiongozi huyo wa Serikali ya awamu ya nne amesema mchakato wa uchaguzi utakaofanyika ndiyo njia pekee ya wananchi kukasimu mamlaka yao kwa viongozi kwa kuwaweka madarakani wanaowataka.

Amesema katika kipindi hiki cha uchaguzi, wanasiasa watakuja na kaulimbiu nyingi na mpaka sasa amesikia wanaosema: “Piga kura, linda kura” wengine wanasema “Oktoba Tunatiki” na wengine wanasema “No reforms, No election.” Amewataka wananchi kufanya uamuzi wa busara.

“Itakapofika wakati wa kupiga kura akili za kuambiwa changanya na zako. Wanasiasa watasema mengi, utakaposikia mengi, fanya uamuzi wa busara ili tupate viongozi watakaolipeleka mbele Taifa letu kwenye amani na utulivu,” amesema.

Kikwete amesema demokrasia ni mchakato mpana na kupiga kura ni sehemu ndogo japo ni muhimu.

Amesema kwa muda uliobaki kuelekea uchaguzi mkuu ni wakati wa Watanzania kuonyesha uzalendo na uwezo wa kusimamia mambo yao ya ndani.

“Kwa wakati tulionao sasa si wa kufanya mzaha, ni mambo ya msingi. Huu si wakati wa malumbano, huu si wakati wa kunyoosheana vidole, huu si wakati wa kujenga uhasama wala kupandikiza hofu na chuki isiyo na sababu miongoni mwa wananchi,” amesema.

Kwa mujibu wa Kikwete: “Huu ni wakati wa kuonyesha uzalendo wetu na kuthibitisha sisi wenyewe na kuithibitishia dunia kuwa, Tanzania na Watanzania tunaweza kuendesha mambo yetu ya ndani kwa amani, uhuru na haki.”


Wajibu wa kila mdau

Kikwete amesema kila mdau wa uchaguzi anapaswa kutimiza wajibu wake, akisema Serikali, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), vyama vya siasa na wananchi kwa ujumla wanapaswa kuhakikisha tofauti za kisiasa haziwi chanzo cha kuharibu umoja wa kitaifa ulioupiganiwa na kujengwa kwa miaka mingi.

“Tutakuwa na tofauti zetu za kisiasa, mwingine ataahidi asali, mwingine ataahidi maziwa, mwingine ataahidi kuibadili nchi ghafla ikawa kama New York (Marekani), mwingine ataahidi mambo mengi, lakini yote hayo yasifanyike katika mazingira ya kuvuruga amani yetu, mshikamano wetu,” amesema.

Ameitaka Tume ya Uchaguzi iendelee kufanya kazi zake kwa weledi, uhuru na uwazi, huku wananchi na vyama vya siasa viamini hivyo.

Amesema hilo likifanyika, kutakuwa na utulivu, aliyeshinda anakuwa kashinda na aliyeshindwa anasema ameshindwa.

Vilevile, amesema Jeshi la Polisi na vyombo vya usalama vifanye kazi zao kwa weledi na kuheshimu haki za kisiasa za raia na kuhakikisha kunakuwa na ulinzi na usalama wakati wote.

“Vyama vya siasa vishindane kwa hoja, siyo kwa kejeli, vitisho, matusi na siyo kwa ugomvi au kwa mifarakano. Baba wa Taifa (Mwalimu Julius Nyerere) aliwahi kusema uchaguzi ni vita vya hoja, siyo vita ya mapanga na risasi,” amesema na kuongeza:

“Isiwe baada ya uchaguzi watu kwa vyama vya siasa hawaelewani, watu wanakaa nyumba moja lakini baada ya uchaguzi hawaelewani… vyama vya siasa visiwe ni msingi wa kufarakanisha watu.”

Kikwete amesema vyombo vilivyopewa mamlaka ya kusikiliza malalamiko baada ya uchaguzi vitekeleze wajibu huo kwa kuzingatia sheria na kwa uharaka wa utoaji wa haki. Pia, wananchi waelimishwe na kuhamasishwa kushiriki uchaguzi kwa kupiga au kupigiwa kura.


Mabadiliko ya sheria

Akizungumzia mabadiliko katika sheria za uchaguzi, Kikwete amesema amekuwa akifuatilia mijadala inayoendelea mitandaoni kuhusu sheria za uchaguzi, lakini wakati mwingine kumekuwa na upotoshaji unaofanywa kwa masilahi ya vikundi vya watu.

“Hivi ni kweli sheria zetu zinazohusu uchaguzi ni mbaya sana kiasi kwamba haziwezi kusimamia uchaguzi mwaka huu? Hivi ni kweli, hakuna maboresho yoyote yaliyofanyika? Mambo mengine yanaleta maswali mengi,” amesema.

Amesema mchakato wa kuboresha sheria hizo umekuwa ukifanyika tangu zamani, kwani yapo mabadiliko yaliyofanyika katika kipindi chake, yapo yaliyofanyika kabla na yapo yaliyofanyika katika awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Kikwete amesema marekebisho yanatokana na kujibu changamoto fulani kwenye uchaguzi.

Amesema Sheria ya Uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani imefanyiwa marekebisho katika eneo la wasimamizi wa uchaguzi ambao sasa si lazima wakurugenzi kuwa wasimamizi wa uchaguzi kama ilivyokuwa zamani.

“Walikuwa wanasema nikulipe mshahara halafu nisishinde uchaguzi. Ilikuwa inaonekana kama ni kikwazo… kwa hiyo limeshughulikiwa. Kupitia marekebisho hayo, zimewekwa sifa za mtu anayeweza kuwa msimamizi au msimamizi msaidizi.

“Masharti hayo, zamani hayakuwapo. Ilikuwa ukiwa mkurugenzi, moja kwa moja ni msimamizi wa uchaguzi na msimamizi alikuwa ana uwezo wa kumchagua msaidizi wake. Hii ni hatua muhimu ya kuongeza uwazi,” amesema.

Kikwete amesema sheria sasa imefuta mgombea kupita bila kupingwa, akieleza awali kuna hila zilikuwa zinafanyika, mtu anaambiwa umekosea kujaza fomu, hivyo anaenguliwa.

Mambo mengine mazuri kwenye sheria hiyo amesema ni pamoja na uamuzi wa kuwaruhusu wafungwa na mahabusu kupiga kura na mtu kuruhusiwa kupiga kura ya Rais akiwa nje ya kituo chake cha kupigia kura.


Elimu kwa wananchi

Awali, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini alisema wakati Rais Samia akizindua Chama cha Mawakili wa SerikaliSeptemba 29, 2022 alitoa maelekezo kwa wizara kukilea kwani ni kama jeshi la kalamu katika kulinda rasilimali za nchi.

“Tukio hili la leo linatafsiri kiu ya Rais Samia kuona wataalamu hawa wanatumia taaluma zao kuimarisha ustawi wa Taifa letu, kwani mada zinazoenda kujadiliwa zimekuja kwa wakati sahihi na zina tija kwa Taifa, kwani elimu hii itasaidia kuonyesha umma namna ilivyojipanga kuwa na uchaguzi huru na wa haki,” amesema.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johari Hamza amesema kongamano hilo lina lengo la kukuza uelewa wa wananchi kuhusu uchaguzi mkuu ujao kwa njia ya kutoa elimu hasa kwenye sheria mbalimbali.

Hamza ambaye ni mlezi wa chama hicho, amesema mabadiliko ya sheria za uchaguzi yaliyofanyika mwaka 2024, hasa kutungwa kwa sheria mbili muhimu; Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani na Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi, yalikuwa muhimu katika kuchochea demokrasia.

“Wito wa kufanya mabadiliko haya ulitoka kwa vyama vya siasa na wadau mbalimbali kwamba kwa kuwa tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu, tufanye mabadiliko. Kwa kuwa Serikali ni sikivu, ilianza kufanya hayo mabadiliko,” amesema.