Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kikwete asimulia Msuya alivyoshiriki mageuzi ya kiuchumi Tanzania

Muktasari:

  • Msuya, ambaye alizaliwa mwaka 1931 katika Kijiji cha Chomvu, Usangi, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, alifariki dunia  Mei 7, 2025, kutokana na ugonjwa wa moyo, akiwa hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam. Ammezikwa leo, Mei 13, 2025, katika makaburi ya familia yaliyopo nyumbani kwake.

Mwanga. Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete ameeleza namna aliyekuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, Cleopa Msuya alivyosimama kidete na kuchangia kwa kiasi kikubwa mageuzi ya kiuchumi nchini.

Kikwete ametoa simulizi hiyo leo, Mei 13, 2025, wakati wa ibada ya mazishi ya hayati Cleopa Msuya iliyofanyika katika Usharika wa Usangi, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro.

Msuya, ambaye alizaliwa mwaka 1931 katika Kijiji cha Chomvu, Usangi, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, alifariki dunia Mei 7, 2025, kutokana na ugonjwa wa moyo, akiwa hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam. Amezikwa leo, Mei 13, 2025, katika makaburi ya familia yaliyopo nyumbani kwake.

Kikwete amesema hayati Msuya, akiwa katika uongozi wakati wa utawala wa Rais wa Awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi, alihusika kwa kiasi kikubwa kuleta mageuzi ya kiuchumi nchini, katika kipindi kigumu, ambapo taifa lilikuwa linakabiliwa na changamoto kubwa za kiuchumi.

Wakati huo, masharti kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) yalikuwa yanahimiza utekelezwaji wa mageuzi hayo kwa kasi, hali iliyohitaji uongozi imara na maamuzi magumu ya kisera, kinyume na sera ya ujamaa ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Kwa mujibu wa Kikwete, wakati huo chama kilikuwa kimeshika hatamu, na hivyo sera na mipango yote ya Serikali ililazimika kupitishwa na CCM kabla ya kutekelezwa.

Amesema licha ya Msuya na Rais Mwinyi kuwasilisha hoja muhimu ndani ya chama, walikumbana na upinzani mkali, na waziri huyo alishambuliwa kwa maneno moja kwa moja, ambapo mmoja wa wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM alimwita  Mr IMF kutokana na msimamo wake wa kutetea masharti hayo. Wakati huo, Mwenyekiti wa CCM Taifa alikuwa Mwalimu Julius Nyerere.

Kikwete alieleza kuwa ilifika wakati Rais Mwinyi alilazimika kusema wazi ndani ya chama kuwa alikuwa amezungukwa na mikuki kulia na kusho, mbele hakuendeki na nyuma hakuendeki, na ndipo Mwenyekiti wa CCM wakati huo, Mwalimu Nyerere, alitoa ruksa kwa mchakato huo kuendelea.

 "Msuya alijitolea kwa dhati, alikuwa mvumilivu sana. Ingawa aliambiwa maneno makali, alisimama kwa utulivu, akajenga hoja kwa kivitendo.

“Alisema, 'Hali yetu ni hii, toeni majawabu ya kutoka hapa, tunawasikiliza. Sisi tuko kwenye Serikali, lazima tutoke hapa. Wenzetu, mnaona haya hayatufai, lakini ni lipi linalotufaa?' Hapo ndipo Mzee Mwinyi alipoanza kutoa ruksa.

“Kulikuwa na uhaba wa mabasi, akasema mwenye lori afunge viti asafirishe abiria, ndipo zikaja Chai maharage. Akasema mwenye kuleta bidhaa kutoka nje aingize, hatutamuuliza fedha amepata wapi, bidhaa zikaanza kuingizwa,” amesema.

Kikwete amesema Msuya alikuwa mtu aliyejaliwa akili nyingi na hakuwa mtaalamu wa uchumi na fedha, lakini aliyafahamu mambo ya uchumi na fedha vizuri kama mchumi mbobevu, na ndiyo maana amewahi kuwa Waziri wa Fedha mara mbili kwa Mwalimu Nyerere (Rais wa kwanza) na mara moja kwa Mzee Mwinyi.

“Penye nia pana njia na hii ndiyo ya kwanza kujifunza kwamba ukijitahidi kujifunza utajua. "Na sifa hiyo ndiyo iliyomwezesha Mzee Msuya kusimamia uchumi kwa ufanisi katika vipindi vigumu vya kiuchumi. Kilikuwa ni kipindi kigumu sana.

"Vilikuwa vipindi vigumu, cha kwanza uhaba wa bidhaa, madukani kulikuwa hakuna vitu, ulikuwa unakwenda kwenye duka la kaya unagawiwa mchele, sukari huko ndiko tulikotoka lakini pia kulikuwa na uhaba mkubwa sana wa fedha za kigeni, kwa sababu uchumi ulikuwa umedumaa.

“Lakini pia kulikuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa huduma za kifedha na kijamii, hayo ndiyo mazingira tuliyokuwa nayo na kiujumla hali ya uchumi ilikuwa ngumu,” amesema Kikwete.

"Kiujumla alikuwa mtu mwenye akili nyingi, maarifa mengi, Mzee Msuya alikuwa mtu mvumilivu na mstahimilivu wakati huo kulikuwa na changamoto nyingi upande mmoja kuna lawama au manung'uniko ya wananchi, kwamba hali ya maisha ni ngumu na ni kweli ilikuwa ngumu."


Alama za Msuya

Akizungumzia alama za hayati Msuya, Rais Samia Suluhu Hassan amesema kiongozi huyo atakumbukwa kwa mchango wake wa kutafuta fedha kwa ajili ya kuunga mkono harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika, akiwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha.

Amesema mbali na jitihada zake za kutafuta fedha kwa ajili ya matumizi ya Serikali, Msuya alibeba jukumu zito la kutenga bajeti kwa ajili ya harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika.

Aidha, Rais Samia amesema kuwa Msuya alikuwa miongoni mwa viongozi waliosafiri hadi China kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa reli ya Tazara, mradi uliochangia kwa kiasi kikubwa katika harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika na ambao umeendelea kuwa na manufaa makubwa kwa taifa kiuchumi hadi leo.

"Hayati Cleopa Msuya atakumbukwa kwa mambo mengi sana, Mzee wetu atakumbukwa kwa kujitolea maisha yake yote kwa kuwatumikia Watanzania kuanzia mwaka 1956 alipoajiriwa kama ofisa Maendeleo ya Jamii na hadi kuwa waziri mkuu na makamu wa kwanza wa Rais na kufikia mwaka 2000 alipostaafu rasmi kwenye siasa na utumishi wa umma," amasema Rais Samia.

Amesema; "Mzee Msuya aliongoza mabadiliko ya mfumo wa kiuchumi ili kuruhusu uchumi wa soko na kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi na hii ilikuwa kipindi kigumu cha kukabiliana na upinzani na shinikizo kutoka ufadhili wa kimataifa, wanasiasa nchini, wafanyabiashara wazawa na wasio wazawa na wengine baadhi yao wakiunga mkono mageuzi na wengine wakiyapinga kwa sababu tofauti tofauti."

Rais Samia amesema, katika nyadhifa mbalimbali alizozishika, ikiwemo waziri wa fedha, alifanikiwa kuondoa baadhi ya shida kubwa zilizokuwa zinawakabili wananchi kwenye miundombinu na kupunguza mfumuko wa bei kwa kipindi cha uongozi wake kwa nyakati tofauti cha mwaka 1972-75, 1983-85 na 1985-90.

Amesema licha ya kustaafu kwake mambo ya siasa mwaka 2000, hayati Msuya aliendelea kutoa mchango kwa taifa kupitia ushauri wake kwa viongozi mbalimbali serikalini ambao umekuwa ni msaada mkubwa kwa taifa.

"Mimi mwenyewe nimefaidika naye, viongozi wengi tulikuwa tukienda kwake ili pamoja na kumjulia hali lakini ushauri na busara zake," amesema Rais Samia.


Aliondoa vurugu za ubunge

Pamoja na mambo mengine, Rais Samia amesema mwaka 2015 wakati anaingia kwenye masuala ya kampeni kwa mara ya kwanza na kupangiwa mikoa ya kaskazini, alikutana na vurugu za ubunge katika Jimbo la Mwanga ambapo kwa kiasi kikubwa Mzee Msuya alimsaidia.

"Mwaka 2010 nilipata bahati kwa mara ya kwanza kumuona Mzee Msuya uso kwa uso na hii ilikuwa mwezi Agosti mwaka 2015, wakati wa kampeni ambapo ilikuwa mara ya kwanza kuingia katika kampeni na kwa wakati ule nilianza na mkoa mgumu kaskazini mwa Tanzania, nilianza Same milimani kule upareni nikateremka huku.

"Nilipokuja Mwanga, mwanga ulikuwa hauwaki kabisa, ni vurugu za kugombania ubunge baina ya Maghembe na wenzake na ilinibidi kupanda juu huku kumfuata Mzee Msuya, aje atupe maelekezo tufanyeje. Baada ya kupata ushauri wa Mzee Msuya nikashuka tena Mwanga ofisi za chama na kamati ya siasa.

"Nilipambana pale hadi saa sita usiku, ndipo nilipata mwafaka, ndio ilikuwa mara yangu ya kwanza kumuona Mzee Msuya kukaa naye ana kwa ana na aliyonieleza yalinisaidia kupata mwafaka," amesema Rais Samia.


 Misukosuko ya shilingi

"Hapa nakumbuka mwaka 1985-90 pale wakati shilingi yetu ikitaka kushuka thamani, huku wanaCCM tukisukumwa kuandamana tukatoka maofisini kule Zanzibar usiku, kwa mara ya kwanza niliimba jina Msuya, kabla ya hapo nilikuwa namsoma kwenye somo la siasa.

"Tulikuwa tukiimba Msuya usikubali shilingi yetu ishushwe thamani, tukaandamana mpaka ofisi za CCM Kisiwandui, lakini baada ya muda mfupi shilingi ikashuka thamani na wakati ule ilikuwa Dola moja ya Marekani ni Sh 5 za Tanzania, wakati ule nauli ya daladala zetu ilikuwa ni Sh5 na ndio maana dola tukaita daladala na mpaka leo yanaitwa daladala kwa sababu nauli ilikuwa shilingi 5," amesema Rais Samia.

Viongozi wengine ambao wameungana na Rais Samia katika mazishi hayo ni Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, Makamu wa Rais Dk Philip Mpango, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla na Rais Mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Kikwete.