Kikokotoo chaguswa bajeti ya 2024/25

Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba akionyesha begi la Bajeti Kuu ya Serika kwa mwaka wa fedha 2024 / 2025 baada ya kuwasili kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma leo Juni 13, 2024. Picha na Edwin Mjwahuzi
Tume ya kuboresha Taasisi za Haki Jinai
Muktasari:
- Kwa kipindi kirefu, kumekuwa na kilio kutoka kwa wastaafu kuhusu kikokotoo, hali iliyowafanya wafanyakazi kuungana na wastaafu hao kudai maslahi eneo hilo.
Dar es Salaam. Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza kuongezwa malipo ya mkupuo kutoka asilimia 33 iliyopo sasa hadi asilimia 40 kwa watumishi wastaafu.
Ikumbukwe mabadiliko ya kikokotoo yalishusha kundi la wafanyakazi waliokuwa wakipokea mkupuo wa asilimia 50 mpaka asilimia 33, huku kundi waliokuwa wakipokea asilimia 25 walipandishwa mpaka asilimia 33.
Akizungumza leo Alhamisi, Juni 13, 2024 wakati akiwasilisha bungeni mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2024/25, Dk Nchemba amesema maslahi hayo yameliangalia kundi kubwa la watumishi wanaofanya kazi nzuri kwa Taifa.
Watumishi hao ni pamoja na walimu, kada ya afya, polisi, magereza, uhamiaji, zimamoto na makundi mengine yalioko Serikali kuu na Serikali za mitaa.
“Rais ameelekeza kuongezewa zaidi kundi lililokuwa likipokea asilimia 25 hapo awali na kupandishwa kwenda asilimia 33, sasa itakuwa asilimia 35 kuanzia mwaka mpya wa fedha.
“Watumishi takriban 17 walioathirika na mabadiliko haya watazingatiwa katika mabadiliko haya. Serikali itaendelea kuangalia maslahi ya wastaafu kwa kuzingatia tathmini ya uhai na uendelevu wa mifuko,” amesema Dk Nchemba.
Ahueni hiyo ya kikokotoo imetangazwa baada ya kuwapo kwa mjadala mkali maeneo mbalimbali kutoka kwa watumishi na wanasiasa ndani na nje ya Bunge wakitaka kibadilishwe, kwani kinawaumiza wastaafu.
Waziri huyo wa fedha amesema Serikali imeendelea kuhakikisha malimbikizo ya kimshahara na yasiyo ya kimshahara ya watumishi wa umma yanalipwa kwa wakati.
Amesema kwa kipindi cha miaka mitatu, jumla ya Sh98.63 bilioni zimelipwa kama malimbikizo mbalimbali ya watumishi wa umma.
Amesema katika kipindi hicho, Serikali imelipa jumla ya Sh160.04 bilioni kugharamia upandishwaji wa vyeo kwa watumishi wa umma wapatao 126,814 katika kada mbalimbali.
Wakati Waziri Mwigulu anawasilisha bajeti hiyo, Rais Samia ameonekana akifuatilia moja kwa moja akiwa Ikulu ya Chamwino, Dodoma.