Kigoma yaunganishwa kwenye umeme wa gridi ya taifa

Muktasari:
Mkoa wa Kigoma umeunganishwa kwenye umeme wa gridi ya taifa kwa mara ya kwanza, jambo ambalo linatarajiwa kuondoa adha ya kukatika kwa umeme mara kwa mara katika mkoa huo.
Dar es Salaam. Mkoa wa Kigoma umeunganishwa kwenye umeme wa gridi ya taifa kwa mara ya kwanza, jambo ambalo linatarajiwa kuondoa adha ya kukatika kwa umeme mara kwa mara katika mkoa huo.
Jana, mitambo ya umeme iliyokuwa ikitumia mafuta ya dizeli ilizimwa na sasa wateja 10,000 katika mkoa huo tayari wameshaunganishwa kwenye gridi ya umeme ya Taifa.
Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa ameandika katika ukurasa wake wa Instagram akisema majenereta ya Kasulu na Kibondo yaliigharimu serikali Sh22.4 bilioni kwa mwaka kutokana na gharama za mafuta na matengenezo.
“Kwa mara ya kwanza tangu kuzaliwa kwake, Mkoa wa Kigoma umeunganishwa na umeme wa Gridi ya Taifa na Tanesco jana imezima rasmi majenereta yaliyokuwa yanazalisha umeme kwa ajili ya Kigoma.
“Majenereta yaliyopo Kibondo na Kasulu pekee yaliigharimu Serikali shilingi Bilioni 22.4 kwa mwaka kutokana na gharama za mafuta na matengenezo. Na hapo bado gharama kubwa zaidi za majenereta ya Kigoma Mjini,” ameandika Msigwa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Septemba 19, 2022 na Kurugenzi ya Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma, Shirika la Umeme nchini (Tanesco), inaeleza kuwa pamoja na Kigoma pia maeneo ya Nyakanazi na Biharamulo na Ngara mkoani Kagera nayo yameunganishwa katika umeme wa Gridi ya Taifa.
Taarifa hiyo pia ilieleza kuwa Tanesco imekamilisha ujenzi wa njia za kusafirishioa umeme za msongo wa Kilovoti 220 kutoka Geita hadi Nyakanazi, Kilovoti 33 na Kilovoti 400 katika mkoa wa Geita na Kigoma pamoja na Kilovoti 33 kutoka Nyakanazi hadi Kakonko kwa lengo la kuunganisha Kakonko, Kibondo na Kasulu kwenye Gridi ya Taifa.
Pia imeeleza kuwa tayari imezindua kituo cha kupokea na kupoza umeme chenye Kilovoti 220/33 cha Nyakanazi na na inaendelea na mpango wa kukamilisha ujenzi wa njia ya kufikisha umeme wa msongo wa Kilovoti 33 wilayani Kasulu hadi Kigoma mjini kufikia mwanzoni mwa mwaka 2023.
“Kukamilika kwa ujenzi wa njia hizi za kupeleka umeme wa msongo wa Kilovoti 33 wa Gridi ya Taifa kumewezesha kuimarisha huduma ya upatikanaji umeme kwenye maeneo yalikuwa yanategemea umeme wa kuzalishwa kwa mashine nne zilizokuwa zikitumia mafuta ya dizeli” inaeleza taarifa hiyo.