Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kigogo Chadema afunguka kushiriki mkutano wa demokrasia

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan amefungua mkutano maalumu wa siku tatu kuanzia leo Jumatatu Septemba 11-13, 2023 wa wadau wa demokrasia kutathimini utekelezaji wa mapendekezo ya kikosi kazi na hali ya siasa nchini Tanzania.

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimelegeza msimamo na kimeanza kushiriki shughuli zinazoandaliwa na Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania?

 Hili ni swali lililoibua mijadala mitandaoni baada ya Makamu mwenyekiti wa Chadema-Zanzibar, Said Issa Mohammed kuonekana katika mkutano maalumu wa baraza hilo.

Mkutano huo maalumu unaoshirikisha wadau wa demokrasia kutathimini utekelezaji wa mapendekezo ya Kikosi Kazi na hali ya siasa nchini, unafanyika jijini Dar es Salaam kuanzia leo Jumatatu, Septemba 11-13, 2023.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameufungua mkutano huo utakaokuwa na mada mbalimbali zitakazotolewa kwa siku tatu.

Ushiriki wa Mohammed, umeibua maswali na mijadala huku baadhi ya wanachama wa chama hicho wametaka achukuliwe hatua kali kwa kuwa amekwenda kinyume na msimamo wa chama hicho wa kutohudhuria vikao hivyo kwa kile wanachodai haina tija.

Tangu mwaka 2020 ulipomalizika Uchaguzi Mkuu, Chadema iliweka msimamo wa kutoshiriki shughuli zozote zinazoratibiwa na Baraza la Vyama vya Siasa Nchini.

Mwananchi Digital, limemtafuta Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema ambaye amesema, alikuwa kwenye kikosi kazi cha Zanzibar huenda kaenda mwa mwaliko huo labda...,"ni vyema mkamuuliza amekwenda kwa mwaliko upi hasa."

Mara baada ya majibu hayo, Mwananchi Digital limekutana na Mohamed katika ukumbi wa Julius Nyerere kunapofanyikia mkutano huo kujua ushiriki wake.

"Msimamo wa Chadema bado upo palepale haujabadilika, mimi hapa sijaja kama mwakilishi wa Chadema, nimekuja kupita Kikosi Kazi cha Zanzibar ambako huko tunashiriki," amesema

"Kwa hiyo isionekane mimi nimekuja hapa kukiwakilisha chama hapana."

Kikosi kazi cha Zanzibar chenye wajumbe 11 akiwemo Mohammed, kiliundwa na Rais Hussein Ali Mwinyi ambacho alikizindua Oktoba 2022.

Wajumbe wa kikosi kazi hicho wanatoka vyama vya siasa, asasi za kiraia, taasisi za kidini na wasomi na mwenyekiti wake ni Dk Ali Uki na makamu wenyekiti ni Balozi Amina Salum Ali.