Kigamboni bado wana kiu ya maji ‘matamu’

Dar es Salaam. Wakati Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) ikisema imefikisha maji eneo la Kigamboni, baadhi ya wananchi wamesema maji hayo hayafai kunywa, kwa kuwa yana chumvi.

Hata hivyo, Dawasa imesema ladha ya maji inategemea miamba yanakopatikana, lakini maji ya Kigamboni yamepimwa na yana viwango vinavyokubalika.

Kwa mujibu wa taarifa ya Dawasa, mradi unaosambaza maji Kigamboni umekamilika kwa asilimia 100 ukihusisha uendelezaji wa visima saba na ujenzi wa tangi la maji la lita milioni 15.

“Vilevile kilomita 120 za mabomba zimeshalazwa katika kata sita za Kisarawe II, Kibada, Kigamboni, Tungi, Mji Mwema na Vijibweni.

“Kwa sasa, mradi huo pia unahudumia baadhi ya maeneo katika Wilaya za Temeke (Kata ya Kurasini na Keko), Wilaya ya Ilala (Kivukoni, Kisutu, Mchafukoge, Gerezani na Kariakoo) na eneo la Magomeni unahudumia Kata za Tandale, Kigogo na Magomeni,” imesema taarifa.

Mradi huo ulizinduliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Novemba 3, 2022, akiagiza maji yasambazwe maeneo ya Temeke, Ilala, Kinondoni, Sinza na Ubungo ili kupunguza makali ya upungufu wa maji.

Pamoja na mradi huo, baadhi ya wananchi waliozungumza na Mwananchi, wanasema hawapendelei maji hayo, badala yake wanafuata visima vya watu binafsi vyenye maji yenye ladha nzuri kama yale ya juu ya ardhi.

Hali hiyo imewapa fursa baadhi ya watu kufanya biashara ya kuuza maji.

Juma Kigosi anayeishi Kibugumo, hutumia baiskeli kusambaza maji yanayotoka kisimani, lakini yanayodaiwa kuwa ladha nzuri kuliko ya Dawasco.

“Natoa maji eneo la Salanga kilomita tano kutoka hapa. Hayo maji yamechimbwa kwenye kisima na kwa bahati nzuri ni matamu.

“Bei inategemea na umbali, kuna sehemu nauza Sh500 hadi Sh600 kwa dumu. Biashara yenyewe ni kutegemea mahitaji ya watu nikipigiwa simu. Kama hapa nimepigiwa simu nipeleke dumu tatu mahali. Madumu mengine yakibaki yanasubiri wateja,” anasema.

“Maji ya Dawasa yapo ila ni ya chumvi, wapo wanaoyatumia kwa matumizi ya kila siku na wengine ndio wananunu haya matamu,” anasema.

Kutokana na mahitaji ya maji ‘matamu’, Kigosi anaendesha maisha kwa biashara hiyo, akiwa na familia ya mke na watoto watatu.

Hata hivyo, anasema kuna changamoto ambazo ni pamoja na mahitaji kupungua wakati wa msimu wa mvua.

“Unaweza kushinda kutwa nzima umepeleka safari moja tu. Lakini wakati jua linawaka, wapo wenye maduka wanayanunua kwa ajili ya kuwauzia wanaokunywa ya baridi,” anasema.

Ally Said, anayeuza maji eneo hilo anasema huuza wastani wa madumu 50 kwa siku, kila moja akiuza Sh700 na anakoyachukua hulipa Sh200 kwa dumu.

“Ninayachota Kishiwani na kuleta mjini kwa kutumia guta za injini, gharama ya kwenda na kurudi ni Sh13,000. Biashara yetu inategemea mawingu. Kama kuna jua kali nauza hata madumu 60 na kama kuna mvua nauza hata madumu 30,” anasema.

“Mahitaji ya maji ni makubwa huku Kigamboni, japo wauzaji ni wengi wakiwamo wenye baiskeli, mikokoteni, lakini bado mahitaji ni makubwa,” anasema.

Mwananchi limefika katika moja ya visima vinavyokimbiliwa na wafanyabiashara wa maji vikitajwa kuwa na maji matamu na kukuta foleni kubwa.

Kassim Shedafa, aliyekuwa akisubiri foleni yake ifike anasema: “Tunapenda kuchota maji hapa kwa kuwa ndiyo matamu na yanauzika, watu wengi hawatumii maji ya Dawasa.”

Mwadawa Zikatimu, anayeishi eneo hilo anasema awali alitegemea maji ya Dawasa, lakini ameamua kuvuna ya mvua.

“Dawasa walisema watatuunganishia maji kutoka Kisarawe ambayo ni matamu, lakini hadi sasa wanatoa yaleyale ya kisima ambayo yana chumvi.

“Tumefungiwa mita kama hivi, kila mwezi wanakuja kusoma. Leo hii Aprili 10, 2024 lazima waje,” anasema.

Pamoja na kuwa na bomba la Dawasa, anasema amelifunga kwa kuwa hutumia maji ya mvua anayovuna.

“Huwa nakinga maji ya mvua kwenye paa la nyumba, najaza vyombo vyangu tunatumia,” anasema.

Mbali na maji ya mvua, Mwadawa alichimbiwa kisima na wafadhili wa Qatar Charity mbele ya nyumba yake.

“Januari 1, 2024 nikiwa nafanya usafi nilisikia simu inaita, nilipokea mtu akaniuliza upo nikamwambia nipo. Aliyepiga simu akasema sisi ni watu wa mradi tunataka tuje hapo tukuchimbie kisima. Wakasema nimeteuliwa, pamoja na maji ya Dawasa pia tunakuchimbia kisima, nikasema sawa,” anaeleza.

Anasema watu hao wakatimiza ahadi yao na kumchimbia kisima na kisha kukijenga ikiwa pamoja na kuweka pampu na tanki la kuhifadhia maji. 

“Kwa kuwa niliona Mwenyezi Mungu amenipa neema ambayo sikuitegemea, kuanzia Januari, Februari, Machi na Aprili mwaka huu, sijauza maji natumia mwenyewe,” anasema.

“Pamoja na maji haya, sijaacha ya Dawasa, maana siku kisima kikiharibika, ukija kuwafuata tena Dawasa mchakato wake utakuwa mrefu,” anasema. 


Ladha ya maji inategemea miamba

Akizungumza na Mwananchi kuhusu maji hayo, Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Kiula Kingu amesema ladha ya maji inategemea miamba, lakini maji ya Kigamboni yamepimwa na yana viwango sahihi.

“Maji ya kisima yanatoka kwenye miamba, kuna tabia za miamba tofauti, ndiyo maana wanakwambia kisima hiki kinatoa maji haya na hiki maji haya,” anasema.

“Pamoja na tofauti hizo, kuna viwango vimewekwa vinavyoeleza kwamba maji fulani yanafaa kwa matumizi. Kwa hiyo kuwa na ladha tofauti za maji, vyote vinawezekana ikawa kweli au uongo lakini inatokana na mtazamo wa mtu,” anasema.

Anasema watu wanaolalamikia ladha ya maji ya Dawasa ni kutokana na mtazamo na mawazo waliyonayo.

Kuna watu wako kule hawalalamikii hilo, kwa sababu wamezoea aina ya maji wanayopata, anayelalamika anafanya hivyo kwa sababu kuna maji mengine anayopata,” anasema.

Akizungumzia mradi wa maji wa Kigamboni, Kingu anasema ni kisima chenye urefu wa mita 600.

“Kabla ya kuchimba kisima tulikuwa tunavuta bomba baharini kuleta maji Kigamboni, lakini kwa sasa hatupeleki kwa sababu mahitaji ya maji yamekuwa makubwa upande huu kabla ya kuvuka,” anasema.

Akizungumzia ubora wa maji, Kingu anasema Dawasa husimamia usalama na ubora wa maji kutoka kwenye visima wanavyoviendesha.

“Baadhi ya visima hivyo ni vile ambavyo vilichukuliwa kutoka katika jumuiya za watumia maji ambavyo vipo katika maeneo ya Kigamboni, Temeke, Mbagala, na Kitunda,” anasema.

“Dawasa pia inatoa elimu na ushauri wa kitaalamu kuhusu uendeshaji na usimamizi wa visima na ubora wa maji kwa visima vinavyoendeshwa na watu binafsi,” anasema.


Usuli Ripoti ya CAG

Wakati Dawasa wakitekeleza uchimbaji wa visima Kigamboni, ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwaka 2021/22 imeonyesha ongezeko la gharama la Sh7.97 bilioni kutokana na ucheleweshaji wa miradi ya visima 20.

“Katika ukaguzi wa mwaka huu, nimebaini visima saba tu ndiyo vimekamilika na kutokuwa na uhakika kuhusu umaliziaji wa visima vingine 13 vyenye thamani ya Sh17.2 bilioni.”