Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kicheko mradi wa Butimba ukianza majaribio usambazaji maji

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla (wanne kushoto) pamoja na viongozi  wengine mkoani humo wakishuhudia maji yakitoka baada ya kuzinduliwa majaribio ya  Mradi wa Maji Butimba jijini Mwanza.

Muktasari:

Utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa chanzo kipya cha maji Butimba ulianza mwezi Februari, 2021 na kwa mujibu wa mkataba unatarajiwa kukamilika Oktoba 31, 2023.

Mwanza. Wakazi wa mkoani Mwanza wataanza ‘kuchekelea’ baada ya mradi wa chanzo cha maji Butimba kuanza rasmi majaribio ya usambazaji maji kwa kuwashwa pampu moja kati ya tano yanayoashiria kukamilika kwa mradi huo.

Kabla ya chanzo hicho, Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mwanza (Mwauwasa) ilikuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 90 kwa siku katika chanzo cha Capripoint hivyo kuwepo upungufu wa lita milioni 75 kwa siku kwakuwa mahitaji ya maji jijini Mwanza ni lita za ujazo milioni 165 kwa siku.

Mradi wa maji Butimba unaotekelezwa kwa gharama ya Sh70 bilioni leo Septemba 15, 2023 umeanza majaribio ukitarajiwa kukamilika na kukabidhiwa rasmi Oktoba 31 mwaka huu ambao utazalisha lita za ujazo zaidi ya milioni 48 zitakazosambazwa kwa zaidi ya watu 450, 000 na kuboresha upatikanaji wa maji kwa wakazi wa jijini humo.

Akitoa taarifa ya mradi huo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mwauwasa, Nelly Msuya amesema chanzo hicho kipya kitapunguza tatizo la upungufu wa maji kutoka  lita za ujazo milioni 70 hadi  lita milioni 22 kwa siku hivyo kupunguza mgawo wa maji kwa wakazi wa Mwanza.

“Maeneo ya Jiji la Mwanza yatakayonufaika na mradi huu ni Nyegezi, Mkolani, Buhongwa, Lwahnima, Fumagila, Sahwa, Igoma, Kishili, Kisesa na Nyamhongolo; Mana yake ni kuwa maji ambayo yalikuwa yameelekezwa katika maeneo hayo kutoka mtambo wa Capripoint yatapelekwa katika maeneo mengine,”

“Baada ya masaa machache wananchi wa maeneo hayo watakuwa wamefikiwa na maji haya lakini tunaomba kuwakumbusha wananchi wetu kuwa bado tupo kwenye majaribio na hivyo tunawasihi kuchemsha maji ya kunywa katika kipindi hiki cha majaribio,”amesema Nelly

Amesema huduma itaendelea kuimarika kwa wakazi wa Nyegezi, Luchelele, Buhongwa, Buswelu na Butimba kadri pampu zitakavyokuwa zinawashwa na uzalishaji wa maji kuongezeka.

“Maji kutoka chanzo hiki yataingizwa katika mtandao mpya wa mabomba hivyo Mwauwasa imejipanga kufanya marekebisho ya mabomba ya zamani ili kupunguza upotevu na kuendelea kuondoa mabomba madogo madogo maarufu kama minyororo ili kupunguza athari za kuongezeka msukumo wa maji kutokana na maji yaliyoongezeka,”amesema

Pamoja na mradi huo, Nelly amesema ipo mingine ambayo hivi karibuni itaanza kutekelezwa na mamlaka hiyo ili kuleta matokeo ya haraka katika kupunguza changamoto ya maji akitaja miradi hiyo ni wa uboreshaji wa uongezaji wa mfumo wa usambazaji maji wenye thamani ya Sh4.3 bilioni akidai tayari wameanza kupokea mabomba ya kuutekeleza.

Mradi mwingine ni wakuboresha huduma za maji Kata ya Luchelele ambapo Sh885.5 milioni zimetengwa kulaza bomba la usambazaji maji lenye urefu wa kilomita 11.6, mradi wa kuboresha maji maeneo ya Nyamhongolo, iluhija na kisesa ambao utatumia Sh664.6 milioni kulaza mabomba ya usambazaji maji kwa umbali wa kilomita 3.5 pamoja na ufungaji pampu lenye uwezo wa kusukuma maji lita 170,000 kwa saa.

Amesema mamlaka hiyo ipo mbioni kuongeza matenki makubwa sita yatakayojengwa Nyamazobe lita milioni tano, Buhongwa lita milioni 10, Fumagila lita milioni 10, Bujora lita milioni tano na usagara lita milioni moja.

Amesema utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa chanzo kipya cha maji Butimba ulianza mwezi Februari, 2021 akidai kwa mujibu wa mkataba unatarajiwa kukamilika Oktoba 31, 2023.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla ameishukuru Serikali kwa kuhakikisha wananchi wanaondokana na kero ya maji huku akimtaka Mbunge wa Ilemela, Agelina Mabula kuitisha mkutano wa hadhara siku magari 11 yatakapopeleka mabomba kwaajili ya usambazaji maji wilayani humi ili waone na kutambua jitihada za Serikali.

Makalla pia amewataka wabunge wengine wa mkoa huo kuitisha mikutano hiyo kueleza mazuri yanayofanywa na Serikali ili wayajue na kuyatambua.

Naye Mbunge wa Ilemela, Angelina Mabula amesema kasi ya vitendo ioneshwe kwa miradi iliyosemwa ili kuondoa changamoto ya maji inayokabili jimbo lake kwa kiasi kikubwa huku Mbuge wa Nyamagana Stanslaus Mabula akimshukuru Rais Samia Suluhu Hassani kwa kutekeleza ahadi yake ya kuhakikisha mradi wa Butimba unakamilika ulioachwa hatua ya usainishaji mikataba na Hayati John Magufuli.