Kicheko kwa bodaboda kodi ikipungua

Muktasari:
- Ni kufuatia pendekezo la Serikali kupunguza ada ya usajili wa pikipiki za biashara kutoka Sh340,000 hadi Sh170,000.
Dar es Salaam. Idadi ya pikipiki zinazojihusisha na biashara ya kubeba abiria, maarufu kama bodaboda, huenda ikaongezeka maradufu kufuatia hatua ya Serikali kupunguza kwa asilimia 50 ada ya usajili wa vyombo hivyo vya moto.
Hatua hiyo ni matokeo ya pendekezo la marekebisho ya Kanuni za Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 2024.
Pendekezo hilo limetolewa leo, Juni 12, 2025, bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, wakati akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba akisoma Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025 / 2026, jijini Dodoma leo, Juni 12, 2025. Picha na Edwin Mjwahuzi
“Napendekeza kupunguza ada ya usajili wa pikipiki za biashara kutoka Sh340,000 hadi Sh170,000 kwa miaka mitatu. Ada husika italipwa wakati wa usajili wa awali pekee.
Amesema kuwa Serikali pia imefuta kodi ya mapato ya mwaka inayolipwa kwa utaratibu wa presumptive tax, na badala yake imeanzisha mfumo wa ulipaji wa mara moja wa ada pamoja na presumptive tax kwa kiasi cha Sh120,000 badala ya Sh290,000. Ada na kodi hiyo italipwa wakati wa usajili wa pikipiki.
“Pia, kufuta kodi ya mapato kwa mwaka inayolipwa kwa utaratibu wa presumptive tax na kuanzisha ulipaji wa mara moja wa ada na presumptive tax kwa kiasi cha Sh120,000 badala ya Sh290,000. Ada na kodi hii italipwa wakati wa usajili”amesema.
Waziri huyo pia amependekeza kupunguzwa kwa ada ya leseni ya uendeshaji wa pikipiki, bajaji na guta kutoka Sh70,000 hadi Sh30,000.