Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bodaboda wapatiwa mbinu kutambua abiria wanaobeba dawa za kulevya

Baadhi ya maofisa usafirishaji maarufu Bodaboda katika kata ya Rwamishenye wakiendelea na shughuli zao baada ya kupatiwa darasa la muda kutoka chuo cha Independent Driving School kilichopo Bukoba mkoa Kagera, la jinsi ya kuendesha vyombo vya moto ili kuepuka mitego ya abiria waosafirisha madawa ya kulevya.

Muktasari:

  • Kuna umuhimu kwa bodaboda kuhakikisha usalama wao na jamii kwa kuzuia usafirishaji wa vitu haramu au hatari kwa kuongeza uwajibikaji na uangalifu katika huduma zao.

Bukoba. Madereva wa bodaboda kanda ya Ziwa wamepatiwa mafunzo ya kutambua abiria wanaobeba dawa za kulevya, ili kuepuka kuhusika na uhalifu wa usafirishaji wa dawa hizo, ambalo linaweza kusababisha adhabu ya kifungo cha maisha jela.

Jitihada za kupambana na usafirishaji wa dawa za kulevya kupitia waendesha bodaboda zimeelezwa na Ofisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Kanda ya Ziwa, Jafari Mtepa.

Amesema bodaboda wanaweza kusaidia kwa kuwatambua mapema abiria wanaojihusisha na biashara hiyo haramu.

Mtepa amesema hayo leo Juni 11, 2025 alipokuwa akizungumza na Mwananchi Digital, kufuatia tukio la mwendesha bodaboda kukimbizwa na polisi akihisiwa kubeba abiria aliyedaiwa kuwa na dawa za kulevya katika eneo la Kata ya Rwamishenye, Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, mkoani Kagera.

 “Njia mojawapo ni kufuata sheria kamili ya kumtaka bodaboda kabla hajampakia mteja kuhakikisha amemuhoji na kujiridhisha shughuli anazofanya sambasamba na kukagua kifurushi au mzigo alioubeba kujua ndani kuna nini ili awe salama” amesema Mtepa.

 “Tunatahadhalisha bodaboda kuwa makini na vifurushi wanavyobeba kusafirisha kutoka kwa abiria wao maana adhabu ni kali, kwa mfano ukikutwa na dawa za kulevya kama heroini gramu 200 unafungwa kifungo cha maisha" ameeleza Mtepa.

Aidha, Mtepa ametaja maeneo maarufu kwa usafirishaji wa dawa hizo kwa njia ya pikipiki ni mipakani mwa nchi.

“Jiji la Mwanza maeneo ya Kisesa, Igogo na mpaka wa Tanzania na Kenya Silali kwa upande wa Mkoa Kagera ni pamoja na mipaka ya Uganda na Tanzania kama vile mpaka wa Mtukula” amesema Mtepa.

Mkazi wa Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, ambaye pia ni Katibu wa Umoja wa Maofisa Usafirishaji maarufu, bodaboda, Salvatory Mulangira, ameieleza Mwananchi Digital tukio la kukimbizwa na polisi baada ya kudaiwa kupakia abiria aliyebeba dawa za kulevya.

“Nilikutana na mteja akiwa amebeba mfuko wa vifaa vya ujenzi kama vile anatoka kazini bila kumuhoji nikampakia kwenye pikipiki, kumbe ndani alikuwa amebeba dawa za kulevya.

Baadaye tukafukuzwa na gari lenye nembo ya polisi kwa nyuma nikataka kusimama mteja akasema nikimbie la sivyo ataniachia mzigo huo wanikamate mimi na tulipofika kwenye daraja alitaka kuruka kwenye pikipiki akakamatwa, mimi nilifanikiwa kukimbia."

Naye, Mwenyekiti wa Umoja wa Maofisa Usafirishaji katika Stendi Kuu ya Ibura, Manispaa ya Bukoba, Johansen Christian amesema kundi kubwa la watu wanaojihusisha na usafirishaji wa dawa za kulevya linaundwa na vijana, akisisitiza kuwa elimu na uangalizi wa karibu vinahitajika ili kuzuia tatizo hilo kuendelea.

 Pia, Mkurugenzi Mtendaji wa Chuo cha udereva cha Independent, Medard Kaheka amesema wamefanya utafiti wa hivi karibuni kuhusu utoaji wa elimu kwa maofisa wa usafirishaji na kubaini kuwa bado kuna upungufu mkubwa wa uelewa, kuhusu athari na mbinu za kudhibiti usafirishaji wa dawa za kulevya.

 “Bodaboda hawana elimu juu ya vyombo wanavyoendesha hasa kuhusu usafirishaji wa dawa za kulevya, tumejiandaa kuwasaidia madereva wa Kagera kutoa elimu ya vyombo wanavyoendesha hadi jinsi wanavyoweza kuepuka na kuwaripoti wateja waliobeba dawa hizo haramu wakati wa kuwasafirisha," amesema Kiheka.