Mapya yaibuka mtandao wa dawa za kulevya

Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo
Muktasari:
- Mtanzania ashikiliwa akituhumiwa kupatikana na kilo 3.8 za skanka nchini Burundi
Dar es Salaam. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imemkamata Shaban Adam (54), mkazi jijini hapa akituhumiwa kutengeneza dawa feki za kulevya aina ya heroini.
DCEA imesema uchunguzi umebaini zimetengenezwa kwa kutumia dawatiba zenye asili ya kulevya na kemikali bashirifu zilizokwisha muda wake wa matumizi hivyo kuwa sumu kwa mtumiaji.
Kutokana na hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Mohamed Janabi amesema kuna ongezeko la vifo vya ghafla vinavyotokana na matumizi ya dawa za kulevya, zikiwamo zinazotengenezwa kwa dawatiba.
Profesa Janabi amesema matumizi ya mchanganyiko wa dawatiba na kemikali bashirifu yana athari kubwa kwa binadamu, ikiwa ni pamoja na kuharibu mfumo wa umeme kwenye moyo hali inayosababisha vifo vya ghafla.
Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema leo Julai 17, 2024 kuwa mtuhumiwa alikamatwa nyumbani kwake Manzese Kilimani Juni 11, 2024 akitengeneza dawa alizozitambulisha kwa jina la heroini kwa kutumia dawatiba zenye asili ya kulevya akichanganya na kemikali bashirifu.
Amesema baada ya mtuhumiwa kuhojiwa alikiri akieleza dawa hizo huzisafirisha kwa kutumia mabasi ya abiria kama vifurushi kwenda mikoa mbalimbali nchini.
Amesema mtuhumiwa alidai awali alikuwa akitengeneza dawa hizo katika nchi za Bara la Asia kwenye magenge ya wazalishaji wa dawa za kulevya na alitumika kama mbebaji, hivyo aliporejea nchini aliendelea na uhalifu huo.
“Tulipomhoji aliutaja mtandao wake tukafanikiwa kukamata zaidi ya lita 19,000 za kemikali bashirifu na mhusika anayezisambaza, mbaya zaidi tulibaini kemikali hizo zilikuwa zimekwisha muda wake wa matumizi,” amesema.
“Mara nyingi tulipokuwa tunakamata dawa za kulevya na kuzipeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali tunakuta kuna mchanganyiko wa dawatiba zenye asili ya kulevya na kemikali bashirifu, hizi dawa ndizo zinatibu saratani na maumivu makali,” amesema.
Lyimo amesema: “Hizi ndizo dawa zinauzwa huko mitaani na ndiyo maana kunaibuka vifo vya ghafla kutokana na mchanganyiko wake kuwa hatari mno kiafya. Hatari zaidi ni hizo dawa na kemikali zinazotumika kutengeneza dawa za kulevya zimekwisha muda wake wa matumizi.”
Athari zake kiafya
Profesa Janabi amesema dawatiba zenye asili ya kulevya zinapotumika bila maelekezo ya daktari zinaathiri mwili wa binadamu na kumsababishia madhara ya kiafya, ikiwemo magonjwa ya moyo, figo, saratani na vifo vya ghafla.
“Dawatiba wanazotumia sisi kule hospitali tunatumia kumlaza mgonjwa kabla ya kumpeleka chumba cha upasuaji, sasa dawa ya aina hii inavyotumika hovyo hata sisi wenyewe hatuelewi kinachotengenezwa ni nini huko mwilini,” amesema.
“Dawa hizi zinaingiliana na mfumo wa umeme wa moyo ndiyo maana siku hizi kuna matukio mengi ya vifo kwa vijana wanaotumia dawa hizi, utasikia wame-overdose, ukweli ni kwamba mfumo wa umeme moyo unakuwa umeingiliwa. Athari nyingine inaonekana kwenye figo pale MNH tunawaona wagonjwa 150 kila siku wa kusafisha figo,” amesema.
“Idadi kubwa ya wagonjwa tunaowaona ni wale ambao figo zao zimekufa kwa sababu ya shinikizo la damu, ugonjwa wa kisukari na kundi kubwa ni wale ambao figo zao zimekufa kwa sababu ya matumizi mabaya ya dawa, zikiwemo hizi za kulevya,” amesema.
Profesa Janabi amesema hadi Juni, 2024 watu 3,840 wamefika Muhimbili kwa tiba ya methadone, takwimu zikionyesha wastani wa watu 900 kila siku hufika hospitalini hapo kwa ajili ya kupata tiba hiyo.
Kanzidata ya ‘wauza unga’
Katika hatua nyingine DCEA imesema imekamilisha kuandaa kanzidata ya wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya.
Kamishna Jenerali Lyimo amesema uchunguzi dhidi ya watu hao umeanza na imebainika baadhi wapo nje ya nchi na wengine wapo nchini.
“Baadhi ya wafanyabiashara hawa wana biashara nyingine za halali lakini wanajihusisha na dawa za kulevya na kufanya utakatishaji fedha, mamlaka inatoa wito kwao kuachana na biashara hii kwani uchunguzi dhidi yao unaendelea,” amesema.
Amesema kwa muda mrefu wamekuwa wakiandaa kanzidata ya wanaojihusisha na biashara hiyo, akieleza wapo wanaofanya na wengine hawajihusishi moja kwa moja ila wanafadhili.
“Taarifa zote hizi tunazo sasa tunawasihi waache. Baada ya leo tukiwanasa kwenye uchunguzi wetu tutawashughulikia,” amesema.
Anaswa Burundi
Amesema pia wanamshikilia Mbaba Issa aliyekamatwa na kilo 3.8 za skanka katika Uwanja wa Ndege wa Melchior Ndadaye nchini Burundi.
Issa ambaye ni Mtanzania aliyekuwa akiishi Burundi, amesema alikamatwa akiwa ameficha dawa ndani ya begi la nguo tayari kwa safari ya kuelekea Dubai.