Kibano kanuni za maudhui mtandaoni

Muktasari:
- Kanuni za maudhui mtandani za mwaka 2022 zimetangenezwa chini ya Sheria ya Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta 2010 (Epoca). Madhuni ya kanuni hizi ni kusimamia na kuendesha maudhini yanayotolewa kwenye mitandao ya kijamii na kwenye vyombo vya habari vya kimtandao.
Na James Marenga
Dar es Salaam. Kanuni za maudhui mtandani za mwaka 2022 zimetangenezwa chini ya Sheria ya Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta 2010 (Epoca). Madhuni ya kanuni hizi ni kusimamia na kuendesha maudhini yanayotolewa kwenye mitandao ya kijamii na kwenye vyombo vya habari vya kimtandao.
Kanuni hizi pia zinatoa utaratibu wa namna ya usajili wa watoa huduma za watumiaji wa maudhui mtadaoni vikiwemo vyombo vya habari mtandaoni kama radio na televisheni, mitando ya kijamii kama facebook, blogs, whatsapp na instagram.
Kanuni hizi za mtandaoni zilianza kutungwa tangu mwaka 2017 na zimeendelea kufanyiwa mabadiliko mwaka 2018, 2020, 2021 na 2022 chini ya sheria ya Epoca.
Sababu kubwa ya kufanyika mabadiliko haya pamoja na mambo mengine ni kuwa mawasiliano ya mtandaoni ambayo yanatumia maudhui hayo yamekuwa yakibadilika mara kwa mara sababu ya kukua kwa teknolojia ya habari, lakini hata hivyo mabadiliko haya ya kanuni yamekuwa kikwazo kikubwa kwa haki ya kuwasiliana na uhuru wa vyombo vya habari nchini.
Moja ya changamoto kubwa iliyoletwa na utungwaji wa kanuni hizi tangu mwaka 2017 ambazo zimekuwa zikibadilika mara kwa mara ni pamoja na kuwanyima fursa hasa vijana waliokuwa wamejiajiri kwenye mitandao ya kijamii kutakiwa kujisajili na kwa masharti magumu.
Katika usajili huo, sharti la kwanza ni lazima mwenye kuanzisha chombo cha habari mtandaoni awe amesajili kampuni kupitia Brela, lazima awe amejiandikisha kama mlipa kodi na amepewa cheti cha uhakiki kabla hajafuata taratibu za Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), ili apate leseni ya usajili na uendeshaji.
Changamoto nyingine kubwa inayotokana na mabadiliko hayo ya kanuni za utangazaji za mwaka 2022 pamoja na mambo mengine ni kuweka makatazo ya matumizi ya baadhi ya maudhui kwenye mawasiliano ya vyombo vya habari vya kieletroniki ambayo Serikali ina mtazamo kuwa haienedani na sheria, lakni kwa upande mwingine watetezi wa haki za kuwasiliana na uhuru wa habari wanadhani zinazuia uhuru wa mawasiliano.
Jambo la kwanza ambalo limeleta kadhia kwa watengenezaji wa maudhui mtandaoni anayetumia aidha youtube, whatsapp, twitter, online TV au radio ni takwa la kanuni la kushurutisha mtengeneza maudhui kuyaondoa mtandaoni kwa muda wa saa mbili tangu apewe taarifa na TCRA pindi watakapopokea malalamiko.
Kabla ya mabadiliko haya ya mwaka 2022 kanuni za mwaka 2018 zilikuwa zinampa mtenganeza maudhui mpaka saa 12 pale panapotokea malalamiko.
Kanuni hii ya kuondoa maudhui mtandaoni kwa muda mfupi inalalamikiwa na wadau wa maswala ya haki ya kupata taarifa, kwani haifuati misingi ya kisheria. Mamlaka imepewa uwezo mkubwa kulazimisha maudhui kuondolewa bila kufuata misingi ya sheria ya kuhoji uwepo wa maudhui hayo na kumtaka aliyeyatengeneza atoe utetezi.
Pia muda ulitolewa ni mfupi, maana wakati mwingine mtengeneza maudhui anaweza kuwa kwenye mazingira ambayo hakuna mtandao na anaweza kuchukuliwa hatua kuwa amekaidi amri.
Jambo lingine ni kuwa inawezekana maudhui yaliyotolewa yasiifurahishe Serikali kwa sababu yanaeleza ukweli wa mambo wasiyotaka yaandikwe, hii ni sababu nyingine itakayoshinikiza maudhui kuondolewa mtandaoni.
Sehemu nyingine yenye changamoto kwenye kanuni hili ni jedwali lililotengezwa linaloelezea maeneo 10 yanayozuiliwa kwenye utengezaji wa maudhui na baadhi ya mambo hayo yana nia ya kuzuia uhuru wa kutoa taarifa na kujinaisha watoa taarifa kwa kile kinachodaiwa kuwa ni taarifa za uongo.
Eneo majawapo la makatazo ni katazo namba 2 kwenye jedwali la tatu la kanuni hizo za 2022 la kuzuia kuchapisha maudhi ambayo yatamkashifu mtu au labda kiongozi hata kama kashfa hizo zitahusiana na habari ya kweli isipokuwa tu litamfanya huyo mtu au kiongozi adhurike linapaswa kutoandikwa.
Katazo kama hili linafifisha uhuru wa utoaji taarifa, maana habari nyingine zinaweza kuwa ni kwa maslahi ya umma au vitendo vinavyofanywa na hao wanaodaiwa kukashifiwa vinaweza kuwa ni kwa maslahi ya umma, lakini wakalindwa na sheria.
Kwa kanuni hizo kwa mfano zinaweka makatazo kwa wamiliki wa mitandao ya kijamii kama tiktok, facebook, snapchat, like, twitter wanakatazwa kutuma jambo lolote linalohusu, kuandaa, kuhamasisha maadamano hata yale ambayo yanaruhusiwa kikatiba na wakati mwingine yanavihusu vyama vya siasa ambavyo vinasimamiwa na sheria ya vyama vya siasa.
Maandamano hata ambayo yanatekelezwa kwa mujibu wa sheria ya kazi na mahusiano kazini ya mwaka 2004 nayo pia yakitangazwa na kuandaliwa kwa njia ya mitandao nalo ni kosa pia.
Changamoto ile kanuni ya 9 ambayo inamtaka mwenye leseni ya kuandaa maudhui anapolazimishwa kuweka wazi watoa taarifa wake na hata kama taaluma yake inamkataza kuweka wazi vyanzo vyake vya habari. Kanuni zinatoa maelekezo kuwa mamlaka ikitaka taarifa za mtoa huduma unapaswa kuzitoa na ukishidwa unachukuliwa hatua za kijinai.
Makatazo mengine ni kuandika au kutoa maudhui kwa njia ya video au sauti ambayo yataonekana kuingilia masuala ya uchumi wa nchi au kuufedhehesha hata kama maudhui hayo yana lengo la kueleza hali halisi kwa wananchi. Mfano mzuri ni masuala ya tozo ambayo baadhi ya wananchi wakiwemo watumishi wa umma walipoyaongelea mtandaoni yamewagharimu ajira zao na wengine kukamatwa na polisi.
James Marenga ni wakili wa kujitegemea