Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kiama kwa waharibifu wa mazingira, vyanzo vya maji

Muktasari:

  • Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameweka jiwe la msingi ujenzi wa bwawa la Kidunda, mkoani Morogoro, atoa maagizo kwa mamlaka kutunza mazingira na vyanzo vya maji

Morogoro. Tatizo la uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji linaloendelea nchini, limeifanya Serikali kutoa maagizo saba kwa mamlaka za wilaya, mikoa na za maji ikiwamo kutungwa sheria ndogo za kusimamia vyanzo vyote vya maji na kuwachukulia hatua kali watakaokaidi.

Maelekezo mengine ni kila Mtanzania popote alipo kutambua ajenda kubwa na muhimu kwa sasa ni utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji, hivyo izungumzwe kwenye vikao vyote vya uamuzi.

Wakulima na wafugaji wametakiwa kutumia na kuvitunza vyanzo hivyo na kuacha kupeleka mifugo kwenye mashamba ya watu.

Maagizo hayo yametolewa leo Jumatano, Machi 5, 2025 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipoweka jiwe la msingi la ujenzi wa Bwawa la Kidunda, mkoani Morogoro ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 28. Likikamilika litahudumia mikoa ya Pwani, Tanga, Dar es Salaam na Morogoro.

Amesema kumekuwa na uharibifu wa vyanzo vya maji na mazingira, akieleza pasipo hatua za haraka na za makusudi kuchukuliwa hali itakuwa mbaya.

Amesema bwawa hilo limekuwa kwenye historia ndefu ya nchi tangu awamu ya uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliyetamani kulijenga lakini haikuwezekana.

"Bunge na wabunge wake wamelizungumza sana hili kwa kuiagiza Serikali kutenga fedha hasa baada ya mwaka 2022 kulipotokea ukame.

"Mradi huo, utaweza kudumu endapo tu vyanzo vyote vinavyotiririsha maji vitatunzwa, la sivyo tukiharibu bwawa hili halitakuwa na maana licha ya mabilioni ya fedha tuliyowekeza na leo tuna kilio cha upatikanaji wa maji vijijini. Tunapaswa kuvilinda na kuwachukilia hatua wananchi wote wanaoviharibu," amesema.


Maagizo saba

Majaliwa ametoa maagizo mosi; kila Mtanzania popote alipo, ajenga tabia ya utunzaji mazingira na vyanzo vya maji iwe ajenda ya kudumu na izungumzwe maeneo yote ya ngazi za uamuzi kuanzia kata hadi mikoa.

Pili; mamlaka zote zifanye kazi kubainisha vyanzo vya maji kwa kushirikiana na wananchi wa maeneo hayo, ivilinde na kutunga sheria ndogo za kuvilinda ili yeyote atakayekwenda kinyume hatua zichukuliwe.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa Bwawa la Kidunda litakalokuwa na uwezo wa kuhifadhi maji lita bilioni 190.

"Mamlaka za mikoa na maji kuendelea kutoa elimu juu ya umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji, ikiwamo kuvitaja kabisa kwa sababu mmekwisha kuvibainisha. Tunatambua kuna wakulima, wafugaji lakini tuna jukumu la kulinda vyanzo vya maji wakati shughuli za kilimo na ufugaji zinaendelea," amesema.

Amesema Serikali inatambua na kuthamini ufugaji lakini mzuri, ni ule unaozingatia taratibu pasipo kuwasumbua wengine, ikiwamo kuingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima.

"Hili halikubaliki. Fuga kulingana na uwezo wa eneo la malisho. Tunawapenda wafugaji lakini lazima tufuate taratibu," amesema.

Agizo la nne amesema: "Mamlaka za mabonde msikae ofisini, wekeni mipango ya kuyajua maeneo yenu, uwezo wake wa kutiririsha maji wakati wote, shirikisheni wananchi namna bora ya uhifadhi. Tudhibiti uchochoro wa kuchukua maji. Hatuzuii watu kuchukua maji lakini utaratibu ufuatwe."

Amesema vibali vya matumizi ya maji viendelee kutolewa kwa kuzingatia mahitaji ya watu wengine na yanakwenda kwa wahusika.

Tano; ametaka mamlaka za maji kutambua uwezo wa wananchi na vijiji vinavyotunza maji na kuwapatia motisha.

Muonekano wa ujenzi wa Bwawa la Kidunda litakalokuwa na uwezo wa kuhifadhi maji lita bilioni 190.

Sita; mamlaka za maji zimetakiwa kuhakikisha wananchi wanaoishi karibu na vyanzo vya maji wanapata huduma.

Saba; ameagiza ukataji wa miti kwenye maeneo ya vyanzo vya maji usimamiwe, akieleza kazi hiyo si ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira pekee bali ni ya kila mmoja.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema wabunge kwa nyakati tofauti wameshika shilingi ya bajeti juu ya utekelezaji wa bwawa la Kidunda na limetolewa maelekezo mengi na viongozi, lakini tatizo lilikuwa fedha nyingi kuhitajika kutekeleza mradi.

Waziri Aweso amesema maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuwa wanapojenga mradi wa maji, kabla ya kuupeleka maeneo mengine wananchi wanaozunguka mradi wapate maji.

“Kukaa na waridi lazima unukie na wana Ngerengere lazima mnukie na niwaambie tu mtapata maji. Natoa maelekezo kwa Dawasa, ije Ngerengere iangalie inatoa wapi maji wananchi wapate,” ameagiza.

Awali, Waziri wa Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete amesema alipochaguliwa kwa mara kwanza kuwa mbunge wa Chalinze mwaka 2013 tatizo kubwa lilikuwa maji na mara zote alikuwa akilipigia kelele bungeni.

"Baada ya muda mrefu, Serikali ya awamu ya sita inakuja kushusha joto la maji tulilokuwa nalo. Tunashukuru sana Serikali kwa hili," amesema.

Mwakilishi wa mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya maji na mazingira, Stella Manyanya amesema suala la Kidunda limekuwa na sauti kubwa ndani na nje ya Bunge.


Taarifa ya mradi

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri amesema bwawa hilo litakuwa na uwezo wa kuhifadhi maji lita bilioni 190, lengo ni kuhakikisha Mto Ruvu unakuwa na maji wakati wote na kunufaisha mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es Salaam na uzalishaji wa megawati 20 zitakazoingizwa kwenye Gridi ya Taifa.

Amesema katika mradi huo itajengwa barabara kwa kiwango cha changarawe kilomita 75 kutoka Ngerengere hadi Kidunda.

Mkataba ulisainiwa Oktoba 31, 2022 na mradi ulianza rasmi Juni 18, 2023 ukitarajiwa kukamilika Juni 2026.

Mwajuma amesema mkataba huo uliingiwa baina ya Wizara ya Maji kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) na mkandarasi Ms Sinohydro Corporation Ltd ya China.

Mhandisi mshauri ni Ms Ghods Niroo Engineering Company ya Iran kwa ubia na Ms Advance Engineering Solution (T) limited ya Tanzania.

Amesema mradi huo unaogharimu Sh335.8 bilioni za ndani, umefikia asilimia 28 na unaendelea vizuri.

Amesema mpaka sasa mkandarasi amelipwa Sh85.4 bilioni ikijumuisha malipo ya awali na mhandisi mshauri amelipwa Sh698.6 milioni.

Mkandarasi anadai Sh35.7 bilioni kutokana na hati za malipo zilizoidhinishwa. Kwa upande wa mhandisi mshauri anadai Sh504.2 milioni kutokana na hati zilizoidhinishwa.

"Wizara imejipanga kufikisha maji katika vijiji vyote vinne vya Kata ya Mkulazi vya Usungura, Kidunda, Chanyumbu na Mkulanzi vinavyozunguka mradi huu," amesema.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amesema wakazi wa mkoa huo wanahitaji mambo mawili ili uendelee ambayo ni barabara na maji.

Amesema hadi kufikia Februari 2025 wastani wa upatikanaji wa maji ni takribani asilimia 70.

Malima amesema awali, vijiji vya karibu vinavyozunguka eneo hilo vilikuwa havitajwi kunufaika na mradi huo lakini baada ya kukutana na Dawasa na Serikali vinakwenda kunufaika.

Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Khamis Taletale maarufu Babu Tale amemwomba Waziri Mkuu kutoa maelekezo kwa Waziri Aweso ya jinsi gani wakazi wa jimbo hilo watapata maji kutokana na mradi huo.

"Ili mkazi wa Ngerengere apate maji baridi lazima akanunue Chalinze, sisi hapa wote kwenye jimbo hatuna uhakika wa kupata maji lakini wa Dar es Salaam tunakwenda kuwalisha maji. Tunakuomba sana Waziri Mkuu umuelekeze waziri ili nasi tupate maji," amesema.

"Kila nikizungumzia maji, unasikia wananchi wanakohoa, hivyo waziri mkuu naomba uwatoe adha ya maji wananchi hawa."

Pia, amesema baadhi ya wakazi walitoa eneo hilo ili kujengwa bwawa  hawajapata fedha walizoahidiwa, hivyo akaomba maelekezo ya Majaliwa ili walipwe.

Waziri Aweso amesema ameielekeza Dawasa kuhakikisha wanaostahili wanalipwa.