Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kesi ya meno ya tembo yakwama

Muktasari:

  • Kesi ya kukutwa na vipande 166 vya meno ya tembo, kucha 65 na meno 20 ya simba inayomkabili Abdallah Mohamed (58) na wenzake 13 imeshindwa kuendelea baada ya upande wa mashtaka kudai kuwa upelelezi haujakamilika.

Dar es Salaam. Kesi ya kukutwa na nyara za serikali inayomkabili Abdallah Mohamed (58) na wenzake 13 imeshindwa kuendelea baada ya upande wa mashtaka kudai kuwa upelelezi haujakamilika.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka la kumiliki vipande 166 vya meno ya tembo vyenye thamani ya zaidi ya Sh3.2 milioni na kucha 65 na meno 20 ya simba yenye thamani ya zaidi ya Sh57 milioni, mali ya nchi za Msumbiji na Tanzania, bila kuwa na kibali kutoka kwa mamlaka ya wanyama pori.

Wakili wa Serikali, Erick Kamala amedai hayo leo Septemba 5, 2023; mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Mary Mrio, kuwa shauri lilikuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi haujakamilka.

"Upelelezi haijakamilika, naiomba mahakama hii ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa," amedai Kamala.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Mrio ameahirisha shauri hilo hadi Septemba 19, 2023; kwa ajili ya kutajwa.

Mbali na Mohamed wengine ni kampuni ya AB Marine Products Limited, Roseline Achachi (43) Kennedy Mwambeta (41), Noel Kassaro (41), Tito Mwambe (34), Erasto Makinda (46), Peter Kikwala, Theresia Rukanga (40), Abubakari Pazia (37), Haipeng Guo (50), Yassir Hussein(50), Salum Kiloko (42) na Hamis Mbwana(34).

Katika shtaka la kuongoza uhalifu inadaiwa kuwa tarehe tofauti kati ya Januari 1, 2019 na Mei 27, 2023 katika uwanja wa ndege wa Pemba nchini Msumbiji na uwanja wa ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam washtakiwa hao walipanga njama ya uhalifu kwa kuuza, kununua, kuhamisha na kumiliki nyara za serikali.

Nyara hizo ni vipande 166 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh3,285,807,600 mali ya nchi za Msumbiji na Tanzania bila kuwa na kibali kutoka kwa mamlaka za wanyama pori katika nchi hizo.

Inadaiwa kuwa katika tarehe hizo hizo na maeneo hayo, washtakiwa walikutwa wakijishughulisha na biashara ya nyara za Serikali ambapo walikutwa na meno 20 na kucha 65 za simba mali ya Tanzania na Msumbiji.

Katika shtaka la nne na la tano washtakiwa wanaodaiwa kumiliki nyara za Serikali kinyume cha sheria ambapo katika tarehe hizo hizo na maeneo hayo walikutwa na vipande 166 vya pembe za ndovu vyenye uzito wa kilo 236.87.

Pia walikutwa na meno 20 ya simba pamoja na kucha 65 za simba bila ya kuwa na kibali kutoka mamlaka ya wanyama pori.

Washtakiwa hao pia wanadaiwa kughushi nyaraka mbalimbali ambapo inadaiwa kuwa Mei 27, 2023 walitengeneza nyaraka feki ya kuonyesha uhalali wa kusafirisha mizigo hiyo wakidai imetolewa na mamlaka husika nchini Msumbiji inayowaruhusu kusafirisha kamba kutoka Jamhuri ya Msumbiji kwenda Kaula Lumpur, Malaysia kupitia Dar es Salaam.

Katika mashtaka ya utakatishaji wa fedha, mshtakiwa Abdullah Omar na kampuni ya AB Marine Product Limited walijipatia nyumba katika eneo la Mabibo, Manispaa ya Ubungo, huku Mwambeta akidaiwa kujipatia gari aina ya Toyota Prado kupitia mapato ya makosa ya kughushi na kumiliki nyara za Serikali kinyume cha sheria.

Pia, inadaiwa kuwa Mwambeta katika tarehe tofauti, kati ya Oktoba 11, 2021 na Mei 27, 2023; katika eneo la Kunduchi Mtongani, Manispaa ya Kinondoni, alijipatia gari aina ya Toyota Land Rover kupitia mapato ya makosa ya kughushi, kumiliki na kuuza nyara za Serikali kinyume cha sheria.