Mahakama yataka uthibitisho mshtakiwa kufanyiwa upasuaji
Muktasari:
- Mahakama imeshindwa kuendelea na usikilizwaji wa kesi baada ya mshtakiwa Majuto Ndevu kutofika mahakamani akidaiwa kufanyiwa upasuaji.
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuagiza mshtakiwa Majuto Ndevu anayekabiliwa na kesi ya kukukutwa na meno ya tembo yenye thamani ya zaidi ya Sh108.9 milioni kuwa tarehe ijayo anapokuja mahakamani apeleke uthibitisho unaoonyesha alikuwa amelazwa hospitalini.
Hatua hiyo imekuja baada ya Wakili wa Serikali, Grace Mwanga kuieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa shauri lilikuja kwa ajili ya usikilizwaji lakini amepata taarifa mshtakiwa Ndevu amelazwa hospitalini.
"Taarifa imetolewa mshtakiwa Ndevu amelazwa na amefanyiwa upasuaji leo na kesho anatoka hospitali inanitia shaka, naiomba mahakama hii tarehe ijayo mshtakiwa alete vielelezo vinavyoonyesha amelazwa hospitali,” alisema Mwanga.
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Fernand Kihwonde alikubaliana na ombi hilo hivyo alimtaka mshtakiwa huyo tarehe ijayo apeleke vithibitisho vinavyoonyesha alikuwa amelazwa na kufanyiwa upasuaji.
"Mahakama hii ilitakiwa iendelee na ushahidi lakini mshtakiwa amefanyiwa upasuaji hivyo tarehe ijayo mashahidi mliofika askari mpelelezi wa kituo cha polisi Msimbazi, Mratibu wa Polisi, Benard Nyambalya na Madini Tumbo mhakikishe mnafika bila kukosa," alisema Kihwonde
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 22,2023 kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji.
Mbali na mshtakiwa Ndevu wengine ni Salehe Ngaumba, Zuberi Malengeta ambao wanakabiliwa na shtaka moja la uhujumu uchumi ya kesi namba 63/2023.
Inadaiwa kuwa Februari 14,2019 eneo la Kitinge Relini Kipunguni washtakiwa hao kwa pamoja walikuwa na meno ya tembo matatu yenye thamani ya Dola za Kimarekani 45,000 bila ya kuwa na kibali.