KESI YA LISSU: ‘Chadema itagharamia gharama za mejeruhi wote’

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Pwani, Boniface Jacob maarufu Boni Yai, amesema wanachama na makada waliojeruhiwa wakiwa viunga vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, watagharamiwa matibabu yao.
Baadhi ya viongozi na wanachama wa Chadema wamedaiwa kukutwa na kadhia hiyo walipokwenda kufuatilia kesi ya uhaini na ya kuchapisha taarifa za uongo mitandaoni inayomkabili mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu.
Boni Yai na wajumbe wengine wa Kamati Kuu ya Chadema akiwemo Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu wamekutana na waandishi wa habari mchana wa leo Alhamisi, Aprili 24, 2025 makao makuu ya chama hicho, Mikocheni, Dar es Salaam.
Boni Yai amedai kwenye hekaheka baina ya wafuasi na viongozi wao dhidi ya Polisi wamekutana na kadhia hiyo ya kujeruhiwa na wamepelekwa hospitalini kwa matibabu.
Miongoni mwao ni Makamu wa Chadema Zanzibar, Said Mzee Said na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Ali Ibrahim Juma.
“Wale wote waliojeruhiwa kwa kwenda Kisutu kufuatilia kesi ya mwenyekiti wetu Lissu wote Chadema itagharamia matibabu yao. Kwa taarifa wako kama nane na wengine hatujui walipo,” amedai Boni Yai.