Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kesi ya Boni Yai na Malisa yachukua sura mpya, Serikali yakata rufaa Mahakama Kuu

Washtakiwa, Boniface Jacob (kulia) akiwa na Godlisten Malisa, wanaokabiliwa na mashtaka ya kuchapisha taarifa za uongo mtandao, wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kesi hiyo kuahirishwa.

Muktasari:

  • Boni Yai na Malisa wanakabiliwa na kesi ya jinai katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakidaiwa kutoa taarifa za uongo mitandaoni, wakilihusisha Jeshi la Polisi na mauaji ya raia wawili Dar es Salaam na Arusha. 

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetupilia mbali ombi la Serikali la kuruhusu kuwekewa ulinzi kwa mashahidi wanaotoa ushahidi katika kesi ya kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni inayowakabili meya wa zamani wa Kinondoni na Ubungo, Boniface Jacob na mwanaharakati Godlisten Malisa.

Uamuzi huo umetolewa leo Jumatatu, Mei 5, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo, anayesikiliza kesi hiyo.

Kutokana na hali hiyo, Serikali imeieleza Mahakama hiyo kuwa tayari imekata rufaa Mahakama Kuu, kupinga uamuzi uliotolewa na Mahakama hiyo.

Jacob, maarufu Boni Yai, mkazi wa  Mbezi Msakuzi, Dar es Salaam, mfanyabiashara na mwanasiasa na Malisa, mkazi wa Moshi, mkoani Kilimanjaro, wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka matatu ya kutoa taarifa za uongo mitandaoni.

Wanadaiwa kuchapisha taarifa za uongo katika mitandao yao ya kijamii ya X na Instagram, kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015, wakilihusisha Jeshi la Polisi na mauaji ya raia.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Clemence Kato akishirikiana na Cathbert Mbiling'i, amewasilisha taarifa hiyo ya kukata rufaa leo, Jumatatu Mei 5, 2025 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya usikilizwaji wa ushahidi wa upande wa mashitaka.

"Mheshimiwa hakimu, kesi hii imekuja kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji, lakini tunaomba kutoa taarifa kuwa, upande wa Jamhuri tuliwasilisha maombi madogo ya kuomba Mahakama iruhusu kuwawekea ulinzi mashahidi katika kesi hii, lakini uamuzi huo umekataliwa na Mahakama hii," amedai Wakili Kato na kuongeza.

"Kutokana na sababu hiyo, upande wa mashitaka tumekata rufaa Mahakama Kuu, kupinga uamuzi huo uliotolewa," amesema Kato.

Kato amesema maombi hayo ya kukata rufaa ya mwaka 2025 wameyasajili leo kwa njia ya mtandao.

 Kato baada ya kueleza hayo, Wakili wa utetezi, Peter Kibatala na Dickson Matata, walisema kuwa hilo ni jambo jipya kwao na walikuwa hawafahamu kama Serikali imewasilisha maombi madogo.

"Kama hawana mashahidi wawe wakweli waseme, sio mnafungua kesi na zina washinda kuziendesha," amedai Kibatala.

Kibatala alidai kuwa Mahakama ambayo upande wa mashitaka umeenda kukata rufaa kupinga uamuzi huo ni ambayo haina maisha kisheria, hivyo wanaomba Mahakama iwahimize upande wa mashitaka wapeleke mashahidi ili kesi hiyo iendelee.

Akijibu hoja ya Kibatala, Wakili Kato amedai kesi ikishaenda Mahakama ya juu, Mahakama ya chini inasimamisha shughuli zote mpaka uamuzi wa Mahakama ya juu utakapotolewa.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Swallo, amesema kuwa anafahamu mahakama za juu zimetoa amri ndogo na maamuzi mbalimbali.

"Kwa asili ya maombi yaliyowasilishwa na kwa masilahi ya haki, kesi hii haiwezi kuendelea na usikilizwaji, hivyo nasimamisha usikilizwaji wa kesi hii hadi uamuzi wa Mahakama Kuu utakapotolewa,” amesema.

Hakimu Swallo baada ya kueleza hayo, ameahirisha kesi hiyo hadi Juni 5, 2025 itakapoitwa kwa kutajwa na washtakiwa wapo nje kwa dhamana.


Maombi ya Serikali

Katika maombi hayo yaliyotupiliwa mbali na Mahakama ya Kisutu, Serikali iliwasilisha maombi madogo, ikiomba mahakama itoe amri ya kuzuia kutajwa utambulisho wa mashahidi na mahali wapo, katika kesi ya kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni inayomkabili Jacob na Malisa.

Kwa sababu za kiusalama, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP) aliwasilisha ombi hilo Mei 2, 2025 na kusikiliza upande mmoja na kutolewa uamuzi asubuhi ya Mei 5, 2025 na taarifa ya kukata rufaa kwa Serikali imetolewa mchana wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya usikilizwaji.

Katika maombi hayo, pia waliomba mashahidi waruhusiwe kutoa ushahidi wao kwa njia ya video na mahakama itoe amri ya kusikilizwa faragha kwa kesi hiyo.

Hata hivyo wakati kesi hiyo ikishwa kuendelea kutokana na rufaa iliyokatwa na upande wa mashitaka, tayari mashahidi watano wa upande wa Serikali wameshatoa ushahidi wao dhidi ya washtakiwa hao.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanakabiliwa na kesi ya jinai yenye mashitaka matatu yakiwamo kuchapisha taarifa za uongo kwenye mitandao ya kijamii.