Shahidi aeleza alivyowapeleka polisi usiku kufanya upekuzi nyumbani kwa Boni Yai

Muktasari:
- Boni Yai na Malisa wanakabiliwa na kesi ya jinai katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, mkoa wa Dar es Salaam, Kisutu, wakidaiwa kutoa taarifa za uwongo mitandaoni, wakilihusisha Jeshi la Polisi na mauaji ya raia wawili Dar es Salaam na Arusha.
Dar es Salaam. Shahidi ya tano wa upande wa mashtaka katika kesi ya jinai inayowakabili meya wa zamani wa Kinondoni na Ubungo, Boniface Jacob na mwanaharakati Godlisten Malisa, ameieleza mahakama namna alivyoshiriki katika upekuzi nyumbani kwa Jacob.
Shahidi huyo, ambaye ni askari Polisi mwenye namba F. 29 D/ SSGT Lugano, kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, ametoa ushahidi wake leo, Aprili 15, 2025 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisitu, katika kesi ya Jinai inayomkabili Jacob na Malisa.
Katika kesi hiyo, Jacob, maarufu kama Boni Yai, mkazi wa Mbezi Msakuzi, Dar es Salaam, mfanyabiashara na mwanasiasa aliyewahi kuwa meya wa Manispaa ya Ubungo na Malisa, mkazi wa Moshi mkoani Kilimanjaro, wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka matatu ya kutoa taarifa za uwongo mitandaoni.
Wanadaiwa kuchapisha taarifa za uwongo katika mitandao yao ya kijamii ya X (zamani Twitter) na Instagram, kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015, wakilihusisha Jeshi la Polisi na mauaji ya raia.
Katika taarifa hizo wanadaiwa kulihusisha Jeshi la Polisi na mauaji ya raia akiwemo mkazi wa Dar es Salaam, Robert Mushi maarufu kama Babu G na aliyekuwa dereva wa magari ya watalii, Wilaya ya Karatu mkoani Arusha, Omari Msemo.

Pamoja na mambo mengine Jacob aliandika kuwa, kuwa licha ya ndugu kutoa taarifa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam lakini kila siku Polisi walikuwa wakisema kuwa halijapata taarifa wala fununu zozote na kuwataka ndugu waendelee kuwa wavumilivu wakiendelea kumtafuta.
Hata hivyo ndugu walidokeza na msiri mmoja akiwataka waende Hospitali ya Polisi Kilwa Road mkachungulie vyumba vya kuhifadhi maiti ambako walikwenda wakamkuta ndugu yao akiwa ameua na wahusika wa hospitali walidai kuwa mailiti ilipelekwa tangu Aprili 10, 2024 na askari wa Jeshi la Polisi.
Hivyo, Boni Yai katika andiko lake alihoji; “ Maiti ina siku 12 Hospitali ya Polisi Kilwa Road haijui bila Jeshi la Polisi kujua ipo hapo? Polisi walioipeleka maiti ni wa nchi gani?
Kesi hiyo ya jinai namba 11805/2024, inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Ushindi Swallo, leo Jumanne, Aprili 15, 2025, imeendelea ambapo shahidi huyo ambaye ni dereva wa Jeshi la Polisi ametoa ushahidi wake jinsi alivyopewa maelekezo na bosi wake ya kuwapeleka askari nyumbani kwa Boniface Jacob, eneo Mbezi Msakuzi.
Akiongozwa kutoa ushahidi wake na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Clemence Kato, Lugano alidai kuwa Aprili 25, 2024 saa 3 usiku alikuwa ofisi akiendelea na majukumu yake ya kazi.
"Siku hiyo, niliitwa na Mkuu wa Upelelezi Msaidizi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam aitwaye George ambapo pia aliwaita wenzangu ambao ni wakaguzi wawili wa Polisi Joram na Michael na kuniuliza kuwa gari ni zima? Na mimi nilimjibu ni zima" alidai Lugano na kuongeza.
"Baada ya kujibu kuwa gari ni zima, alinimuru niwapelekea afande Joram na Michael nyumbani kwa Jacob kwa ajili ya kwenda kufanya upekuzi na mimi nilifanya hivyo," alidai.
Alidai kuwa waliongozana kwenda nyumbani kwa Jacob, akiwa yeye, Joram na Michael pamoja na mshtakiwa ( Jacob).
" Tulifika nyumbani kwa Jacob, saa 4 usiku na tuligonga geti na kufunguliwa na kabla ya kuanza upekuzi, afande Jarom na afande Michael walimuita jirani yake Jacob aitwaye George Steven ili aje ashuhudie upekuzi huo na alipofika zoezi la upekuzi lilianza," alidai Lugano ambaye jukumu lake siku hiyo lilikuwa ni dereva.
Alidai katika upekuzi huo, walikuta simu mbili na laptop moja na baada ya upelelezi, hati ya ukamataji mali ilijazwa na kisha mshtakiwa pamoja askari hao walirudishwa Kituo Kikuu cha Polisi (Central).
Hata hivyo, shahidi huyo alimtambua mshtakiwa mahakamani hapo na baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake, alihojiwa maswali ya dodoso na wakili wa utetezi Peter Kibatala na sehemu ya maswali hayo ilikuwa kama ifuatavyo.
Wakili: Hivi shahidi, kuna tija yoyote kutunga ushahidi?
Shahidi: Hapana
Wakili: Ulivyotoa ushahidi wako, unafahamu kama unapimwa na mahakama na umma uliopo hapa?

Shahidi: Mimi sipimwi.
Wakili: Kwa hiyo unatoa ushahidi na mahakama haikupimi?
Shahidi: Yenyewe ndio inafahamu.
Wakili: Umemueleza Hakimu aina ya gari uliloendesha kwenda nyumbani kwa Boniface Jacob?
Shahidi: Hapana
Wakili: Umemuonyesha hakimu leseni yako ya udereva?
Shahidi: Ikihitajika nitaonyesha.
Wakili: Shahidi nakuuliza swali nijibu, leseni yako ya udereva umemuonyesha hakimu hapa mahakamani?
Shahidi: Sijaonyesha.
Wakili: Shahidi, kuna sehemu yoyote uliieleza kabla ya kumtoa Jacob polisi kumpeleka nyumbani kwake kufanya upekuezi, alipewa haki zake za msingi?
Shahidi: Mimi nilimkuta akiwa na afande Joram na Michael, kwa hiyi sijui kama alipewa haki zake za msingi.
Hakimu Swallo aliingilia kati na kumtaka shahidi huyo alijibu swali kulingana na jinsi anavyoulizwa.
Hakimu: Shahidi jibu swali, haya Kibatala muulize tena.
Shahidi: Mheshiwa hakimu, sisi askari tunapewa tu order.
Kibatala: Unajua mshtakiwa ana haki zake?
Shahidi: Haki zipi?
Wakili: Unataka nikuonyeshe hapa ili uzisome? Kwanza elimu yako umesoma mpaka wapi?
Shahidi: Kidato cha nne.
Wakili: Sasa jibu swali langu.
Shahidi: Sikuambiwa
Wakili: Unafahamu mantiki ya kisheria ya mshtakiwa kumfanyia upekuzi askari anayetaka kufanya upekuzi?
Shahidi: Nafahamu
Wakili: Ulimwambia hakimu, Joram na Michael kabla ya kufanya upekuzi walipekuliwa na Jacob.
Shahidi: Ngoja nikuelimishe.
Wakili: Unielemishe nini shahidi? Wewe jibu swali
Wakili: Shahidi, swali ambalo sitakiwi kukuuliza wewe ni girlfriend wako anakunywa wine kiasi gani.
Wakili: Hivyo maswali yangu wewe yajibu tu shahidi ili tusipoteze muda hapa.
Wakili: Tukumbushe jina la jirani aliyeshuhudia upekuzi nyumbani kwa Boniface Jacob.
Shahidi: George Steven
Wakili: Sasa mteja wangu anasema hana jirani anayeitwa jina hilo, bali anayejirani anayeitwa Frank Steven.
Shahidi: Sifahamu
Wakili: Je unafahamu Boniface Jacob ni Public Figure?
Shahidi: Labda familia yake!
Wakili: Jibu swali
Shahidi: Sifahamu.
Wakili: Je unafahamu Boniface Jacob alikuwa meya wa Manispaa ya Ubungo na Kinondoni na ameonekana mara 1,000 kwenye Tv?
Shahidi: Sifahamu.
Wakili: Je ulimwambia hakimu, hizo simu na Laptop zilizokamatwa zilikuwa aina gani na rangi gani?
Shahidi: Sikumwambia.
Wakili: Hizo simu ulimwambia hakimu, zimepatikana sehemu gani nyumbani kwa Boni?
Shahidi: Sikumwambia.
Wakili: Shahidi, ulimwambia hakimu nani aliyefungua mlango mlipokwenda nyumbani kwa Boniface Jacob?
Shahidi: Sijamwambia.
Wakili: Shahidi, ulimwambia hakimu Jacob alikaa upande sehemu gani katika gari wakati mnaenda nyumbani kwake kufanya upekuzi ili tujue ushahidi wako kama ni wa kweli au wa kutunga?
Shahidi: Sijamwambia.
Wakili: Ulimwambia hakimu Mbezi Msakuzi mlitoka saa ngapi baada ya upekuzi nyumbani kwa Boni?
Shahidi: Sijamwambia.
Shahidi huyo baada ya kumaliza kuhojiwa maswali ya dodoso, Hakimu Swallo aliutaka upande wa mashtaka kutoa idadi ya mashahidi waliobaki ili mahakama ijue namna ya kupanga tarehe ya kesi hiyo.
Wakili Kato alimueleza hakimu kuwa wamebaki mashahidi 10 wa upande wa mashtaka.
Baada ya kupewa taarifa hiyo, hakimu Swallo aliahirisha kesi hiyo na kuipanga kusikilizwa kwa siku tatu mfululizo kuanzia Mei 5, 2025 hadi Mei 7, 2025.
" Kesi hii naiahirisha hadi Mei 5 hadi Mei 7, 2025 itakapoendelea na ushahidi na nataka upande wa mashtaka mje na mashahidi watatu," alisema Hakimu Swallo.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walipandishwa kizimbani Mei 6, 2024 na kusomewa jumla ya mashtaka matatu, mawili kati ya hayo yanamkabili Jacob pekee yake, huku Malisa akikabiliwa na shtaka moja.
Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Machi 19 na Aprili 22, 2024 jijini Dar es Salaam.