Kaya 62 zakosa makazi, 300 zazingirwa na maji Moshi

Baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko katika maeneo ya tambarare Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro. Picha na Omben Daniel
Muktasari:
- Kaya zaidi ya 62 zakosa makazi, huku 300 zikizingirwa na maji katika Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, kutokana na mafuriko kwa sababu ya mvua zinazoendelea kunyesha mkoani humo.
Moshi. Kaya zaidi ya 300 katika Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, zimezingirwa na maji, huku 62 zikiachwa bila makazi kutokana na mafuriko yaliyotokana na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani humo.
Mbali na makazi hayo kuharibiwa, mafuriko hayo pia yameathiri ekari zaidi ya 2,000 za mashamba ya mazao mbalimbali, miundombinu ya barabara pamoja na shule kadhaa kuharibiwa na mvua hizo.
Akizungumza leo Jumamosi Aprili 5, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu baada ya kutembelea baadhi ya maeneo yaliyoathirika na mafuriko hayo, amesema athari zilizotokana na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani humo ni kubwa.
"Leo tumetembelea maeneo ambayo yamepata mafuriko, athari ni kubwa, barabara zimeharibika, kaya 62 zimeingiliwa na maji hawana pa kukaa, tunajitahidi kuendelea kuwahamisha kuwapeleka maeneo ya shule za msingi na sekondari ili kuendelea kujisitiri wakati taratibu nyingine zikifuata," amesema Babu.
Ameongeza kuwa; "Lakini pia yapo maeneo ya Serikali ikiwemo miundombinu ya shule ambazo zimejengwa muda mrefu yameezuliwa kwa upepo mkali na mengine yameanguka, hivyo tumewahamisha wanafunzi kusoma kwenye madarasa mapya ambayo tumeyafanyia ukarabati."
Babu ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari katika kipindi hiki cha mvua ili kuepuka madhara ambayo yanaweza kujitokeza kutokanana mafuriko.

"Natoa wito kwenye mkoa, mvua zinaendelea kunyesha kwa wingi mkoani kwetu na tumegawanyika milimani na tambarare. Niwatake madereva wachukue tahadhari kubwa wanapoendesha magari maeneo ya milimani hasa ikizingatiwa kuna tatizo kubwa la misiba miwili iliyotokea hivi karibuni maeneo ya milimani kutokana na ajali," amesema Babu.
Ameongeza kuwa; "Wananchi walioko tambarare wachukue tahadhari kwani maji mengi yanatoka milimani, wahakikishe watoto wadogo na wanafunzi wanachukua tahadhari."
Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava amesema kata zilizoathirika zaidi na mafuriko hayo ni kata ya Kahe Magharibi, Kahe Mashariki, Mabogini, Arusha chini na Mfumuni.
"Tumepata changamoto kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha Wilaya ya Moshi na baadhi ya maeneo yamepata athari kubwa ambapo maji yamezingira makazi ya watu, na kwenye mashamba ya mpunga na mazao mengine," amesema Mnzava.
Ameongeza kuwa "Maeneo ya Tambarare ambayo ni kata za mabogini, Arusha Chini, Kahe Magharibi na Kahe Mashariki kote kumepata changamoto kutokana na jeografia ya eneo letu ambapo maji yote yanayotoka ukanda wa juu milimani yanaishia huku chini tambarare.
"Nitoe wito kwa wananchi wa Wilaya ya Moshi hususani wa kata hizi za tambarare, kuendelea kuchukua tahadhari kwa sababu mvua bado zinaendelea na serikali tunaendelea na jitihada za kupunguza athari hizo kwa kuchimba mitaro ili maji yaweze kupita kwenye mkondo wake na kwenda mtoni," amesema Mnzava.

Aidha amesema; "Kwa wale walioko maeneo hatarishi kama hapa daraja la miwaleni limekatika wachukue tahadhari, hivyo tunaendelea kutoa wito kwa wananchi wasije kulazimisha kupita kwa lazima kwa sababu wanataka kufika maeneo wanayotaka kwenda."
Amesema wanaendelea kufanya tathimini pamoja kuona maeneo mengine yaliyoathiriwa na mvua hizo na kuona mahitaji ya kibinadamu yanayohitajija ili kuona ni namna gani Serikali tunaweza kusaidia ikiwa ni oamoja na kuboresha miundombinu ya barabara ili kurudisha mawasiliano.
Kwa upande wake diwani wa Kata ya Kahe Magharibi, Aloyce Momburi amesema kumekuwa na changamoto ya maji ya mafuriko ambapo baadhi ya makazi yamezingirwa na maji na mawasiliano ya barabara kukatika.
"Maji haya yameingia siku ya pili leo, kuna Kitongoji cha Mauru, kisangesangeni B, maji ni mengi na nyumba zaidi ya 300 zimeingia maji, bado hatujaweza kuhamisha wale wananchi kwa sababu nao wanajitahidi kujisaidia kutoa maji kwenye makazi yao.

"Adha ni kubwa kwa sababu mawasiliano ni kitu cha msingi na katika maeneo yetu ya tambarare tanategemea kilimo na ufugaji kama shughuli kuu za kiuchumi na kwa leo mifugo haiwezi kutoka na watu hawawezi kutoka kwenda kwenye shughuli za kilimo na shughuli nyingine za kiuchumi, tunaiomba Serikali kuchukua jambo hili kwa uzito wake kwa maana limekuwa likipoteza nguvu kazi," amesema Momburi.
Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa wakala wa barabara za vijijini na mjini (Tarura) Mkoa wa Kilimanjaro, Cuthbert Kwayu amesema athari ni kubwa na kwamba timu itafika kufanya tathimini ili kuona namna ya kukarabati miundombinu iliyoathiriwa na nafuriko hayo na kurudisha mawasiliano katika hali ya kawaida.