Katibu mwenezi Chadema, wanachama 500 wahamia CCM

Muktasari:
Katibu huyo amedai kuchoshwa na manyanyaso , kutothaminiwa na uongozi wa juu
Shinyanga. Katibu mwenezi wa Chadema, Kata ya Masekelo Manispaa ya Shinyanga, Jastan Mwasiga amekihama chama hicho na kujiunga na CCM.
Kiongozi huyo na wanachama wengine zaidi ya 500 wa chama hicho wamekihama chama hicho leo Agosti 27, 2018 kwa kile walichodai kunyimwa uhuru na viongozi wa chama hicho ngazi ya juu.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Mwasiga amesema ameamua kuhama kwa sababu chama hicho kinamnyima uhuru, kina masimango na unyanyasaji.
“Nimeamua kuhama mimi na baadhi ya wanachama wenzagu kwa kuwa viongozi wa Chadema ngazi ya juu wamekuwa wakitutumia kama daraja la kuvukia, hatuthaminiwi licha ya kuwa tumesaidia kufanikisha kata hiyo kupata ushindi wa viongozi wa chama hicho kuanzia ngazi ya kitongoji hadi kata,” alisema Mwasiga.
Mwasiga aliwahakikishia wanachama wa CCM kuwa kwa sasa ngome ya Chadema katika kata hiyo iliyokuwa inashinda kila awamu ya uchaguzi inaenda kubomolewa kwa kuwa anajua mbinu zote za ushindi.
Mmoja wa wanachama waliohamia CCM, Hamza Hamis amesema ameamua kurudi chama hicho kwa kuwa kilikua cha wazazi wake na kinafaa tofauti na Chadema alikokimbilia bila kujua kama kuna matatizo na manyanyaso.
Akiwapokea wanachama hao, katibu mwenezi wa kata hiyo, Mashimba Kadama aliwataka wanachama hao kutojisahau na kwamba wasaidie kuongeza wanachama wengine ili wasaidie kurudisha kata iliyokuwa imepotea.
Katibu wa CCM kata ya Masekelo, Petro Kolimba alisema amefurahi wanachama hao kujiunga na CCM na kwamba kwa kipindi cha miezi sita zaidi ya wanachama 950 wamejiunga na chama hicho.