Kamati Kuu Chadema kutoa muongozo mchakato wa Katiba Mpya

Muktasari:
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeitaka Serikali kueleza kwanini muswada wa kuendeleza mchakato wa Katiba haukuwasilishwa bungeni wakati wa kikao cha Bunge la Bajeti; na ni lini muswada huo utapelekwa bungeni.
Geita. Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika amesema Kamati Kuu ya chama hicho kinachotarajiwa kukutana hivi karibuni kitajadili, kutathmini na kutoa msimamo kuhusu mchakato wa Katiba Mpya.
Akizungumza wakati wa kongamano la Baraza la Wanawake wa chama hicho (Bawacha) Mkoa wa Geita leo Julai 6, 2023, Mnyika amesema kikoa hicho kitakachoongozwa na Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe ndicho kitatoa muelekeo wa Chadema kuhusu Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi.
Huku akisisitiza msimamo wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini wa Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi kupatikana kabla ya uchaguzi mkuu ujao, Mnyika amewataka wanachama, wafuasi na wapenzi wa Chadema kusubiri maelekezo ya chama baada ya kikao cha Kamati Kuu na kuyatekeleza.
“Msimamo wetu wa kutaka Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi kabla ya mwaka 2025 ni msimamo tutakaoendelea kuusimamia mpaka kieleweke; niwaombe wana Geita wote mtakapo pokea tamko la chama la nini tufanye kama Watanzania kuharakisha nchi yetu inapata Katiba Mpya mtekeleze na kusimamia jambo hili,”amesema Mnyika
Mtendaji Mkuu huyo wa Chadema amesema matumaini ya kukamilika kwa mchakato wa Katiba Mpya kabla ya uchaguzi mkuu unazidi kufifia kutokana na Serikali kutotenga fedha kutosha katika bajeti iliyopitishwa bungeni hivi karibuni.
Hofu nyingine ya chama hicho kwa mujibu wa Mnyika ni Serikali kutowasilisha bungeni muswada wa sheria wa kuanzisha na kuendeleza mchakato wa Katiba Mpya.
“’Chadema tunaitaka Serikali kutamka kwanini haikuwasilisha bungeni muswada wa sheria wa kuendeleza mchakato wa Katiba Mpya na ni lini muswada huo utafikishwa bungeni,’’ amesema Mnyika
Wakati kiongozi huyo wa Chadema akidai hivyo, tayari Serikali imetenga zaidi ya Sh9 bilioni kupitia Wizara ya Katiba na Sheria kwa ajili ya kuanza mchakato wa Katiba Mpya.
Kwa mujibu wa Waziri wa wizara hiyo iliyoidhinishiwa zaidi ya Sh383.6 bilioni kwa mwaka wa fedha wa 2023/24, Dk Damas Ndumbaro, Katiba Mpya ni miongoni mwa vipaumbele 30 vya wizara hiyo.
Miongoni mwa mambo muhimu katika kipengele cha Katiba Mpya ni elimu kwa umma na kampeni ya msaada wa kisheria kwa wananchi maarufu kama Mama Samia Legal Aid.
Akizungumzia nia ya kushika na kuongoza dola, Mweka Hazina wa Chadema Kanda ya Magharibi, Upendo Peneza amesema lengo hilo litatimia pindi kundi la wananawake ambao ndio kubwa kuliko yote nchini itaamua kuwa mstari wa mbele kugombea na kushinda nafasi mbalimbali za uongozi ndani na nje ya chama.
“Bawacha tutumie mchakato wa uchaguzi ndani ya chama kuchagua viongozi bora, wenye haiba nzuri na ushawishi wa kuleta ushindi kuanzia uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025. Tuchague watu wanaokipenda chama ambao pi siyo mzigo kwa chama,’’ amesema mbunge huyo wa zamani wa Viti Maalum
Katibu wa Bawacha Jimbo la Geita, Elizabeth Urasa amesema pamoja na mambo mengine, kongamano la wanawake, vijana na wazee wa chama hicho yanayofanyika sehemu mbalimbali nchini inalenga siyo tu kuwaunganisha, bali pia kuwajengea uwezo na mbinu zitakazosaidia ushindi katika chaguzi zijazo.