Kagame, Museveni warejesha uhusiano, Muhoozi ahusishwa

Rais wa Rwanda, Paul Kagame na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni
Muktasari:
Kufungwa kwa mpaka kuliharibu biashara ya pande mbili iliyotawaliwa na mauzo ya nje kutoka Uganda kwenda Rwanda.
Kigali. Serikali ya Rwanda imesema itaufungua tena mpaka wake wa kituo kikuu cha mpakani cha Gatuna na Uganda wiki ijayo baada ya kufungwa kwa miaka mitatu.
Ufunguzi huo ni mafanikio muhimu katika kurudisha uhusiano mwema kati ya majirani hao. Hatua hiyo imekuja baada ya mtoto wa Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, Muhoozi Kainerugaba kufanya ziara jijini Kigali mwishoni mwa wiki iliyopita.
Awali, yeye na Rais wa Rwanda, Paul Kagame waliahidi kurejesha uhusiano baina ya mataifa hayo mawili.
Mpaka huo ulifungwa ghafla Februari 2019, huku mvutano wa kisiasa kati ya Rwanda na Uganda ukiongezeka. Mataifa hayo mawili ya Afrika Mashariki yamekuwa yakishutumiana kwa ujasusi, utekaji nyara na uvamizi kwenye maeneo ya mipaka.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Rwanda ilisema katika taarifa yake iliyoripotiwa na Shirika la AFP kwamba, kituo kikuu cha mpakani cha Gatuna maarufu kama Katuna nchini Uganda, kitafunguliwa Januari 31.
“Serikali ya Rwanda inajitolea katika juhudi zinazoendelea za kutatua masuala ambayo hayajakamilika kati ya Rwanda na Uganda na inaamini kuwa, tangazo la leo (jana) litachangia kwa njia chanya katika kuharakisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili,” inasema taarifa hiyo.
Hatua hiyo ilisifiwa na Umoja wa Afrika kama “hatua chanya” kuelekea kurejesha uhusiano wa kawaida kwa nchi hizo mbili.
Hata hivyo, hakuna taarifa rasmi ya mara moja kutoka Serikali ya Uganda kuhusiana na uamuzi huo wa Rwanda.
Lakini, Mjumbe wa Serikali ya Uganda katika Umoja wa Mataifa, Adonia Ayebare ambaye pia ni msaidizi wa Rais Museveni anayetegemewa zaidi katika sera ya mambo ya nje, aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa: “Hii ina maana kubwa kwa watu wa nchi zote mbili. Imefanya vyema kwa hatua hii muhimu ya kurejesha uhusiano imara kati ya nchi hizo mbili.”
Kufungwa kwa mpaka kuliharibu biashara ya pande mbili iliyotawaliwa na mauzo ya nje kutoka Uganda kwenda kwa jirani yake.
“Tunaweza kuona Serikali hizo mbili zinajaribu kutengeneza mwelekeo mpya baada ya mzozo wa muda mrefu na vizuizi vichache vya barabarani vimeondolewa,” mchambuzi wa usalama wa Uganda, Fred Egesa alisema.
Kainerugaba, ambaye pia ni Kamanda wa Majeshi ya nchi kavu wa Uganda, anadaiwa kuandaliwa kama mrithi wa baba yake (Museveni-77), ambaye amelitawala taifa hili tangu mwaka 1986.
Museveni na Kagame walikuwa washirika wa karibu katika miaka ya 1980 na 1990 wakati wa vita vya kugombea madaraka katika nchi zao, lakini uhusiano uligeuka kuwa na uhasama mkubwa baada ya kila mmoja kuchukua madaraka.
Rwanda ilifunga ghafla mpaka wake na Uganda kwa kuishutumu nchi hiyo kuwateka nyara raia wake na kuwaunga mkono waasi wanaotaka kumpindua Rais Kagame.
Uganda nayo iliishutumu Rwanda kwa kufanya ujasusi na kuwaua wanaume wawili wakati wa kuvamia eneo la Uganda mwaka 2019, madai ambayo Rwanda ilikanusha.
Tangazo la Ijumaa linafuatia uamuzi wa Rais Museveni alioutoa Jumanne iliyopita wa kufuta nafasi ya mkuu wa upelelezi mwenye nguvu nchini humo, Meja Jenerali Abel Kandiho na kuteua mwingine.
Maofisa wa Rwanda katika miaka ya hivi karibuni walimshutumu Kandiho, ambaye amehamishwa kuwa mjumbe wa usalama nchini Sudan Kusini, kwa kufanya kazi na wapinzani, kuwateka nyara raia wa Rwanda waliopo nchini Uganda.
“Kwa madhumuni ya maelewano kati ya nchi hizo mbili ilikuwa muhimu Kandiho kutumwa mahali pengine,” mchambuzi Egesa alisema.
Desemba mwaka jana, Marekani ilimwekea vikwazo Kandiho, aliyekuwa kamanda mkuu wa ujasusi wa kijeshi aliyehofiwa tangu Januari 2017, ikimtuhumiwa yeye na ofisi yake kuhusika na ukiukaji wa haki za binadamu ikiwa kuteka watu na kuwanyanyasa kingono na kutesa kwa shoti ya umeme.
Mazungumzo ya kujaribu kupunguza mvutano kati ya Kagame na Museveni hapo awali yaliandaliwa na Rais wa Angola, Joao Lourenco na kiongozi wa Kongo, Felix Tshisekedi na mkutano wa mwisho kama huo ulifanyika Februari 2020.
Hakuna mkutano ambao umefanyika kati ya viongozi hao wawili kwa sababu ya janga la Uviko-19. Uhusiano kati ya nchi hizo mbili pia ulidorora baada ya uchunguzi mwaka jana kubaini kuwa, Rwanda ilitumia programu ya kijasusi ya Israel ya Pegasus kudukua simu za waziri mkuu na waziri wa mambo ya nje wa Uganda.
Kigali ilitupilia mbali madai hayo na kusema ni kama sehemu ya ‘kampeni chafu.’ na kuyapuuza madai hayo ya majirani zake hao.
Kabla ya kufungwa kwa mpaka huo, mauzo ya Uganda kwenda Rwanda, hasa saruji na chakula yalifikia zaidi ya Dola za 211 milioni za Marekani mwaka 2018, kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia (WB), huku Rwanda ikisafirisha bidhaa zenye thamani ya Dola 13 milioni za Marekani kwenda Uganda.
Biashara ilishuka mwaka 2019, huku hali hiyo ikichochewa zaidi na mlipuko wa ugonjwa wa Uviko-19 ambao umesababisha madhara makubwa ya kibiashara kwa nchi za mataifa ya Afrika.