Jinsi Shamim, mumewe waliyofungwa maisha

Muktasari:
- Wanandoa, Abdul Nsembo na mkewe, Shamimu Mwasha wamehukumiwa adhabu ya kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya makosa ya kusafirisha dawa za kulevya.
Dar es Salaam. Wanandoa, Abdul Nsembo na mkewe, Shamimu Mwasha wamehukumiwa adhabu ya kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya makosa ya kusafirisha dawa za kulevya.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Jaji Elinaza Luvanda wa Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, maarufu kama Mahakama ya Ufisadi, aliyekuwa akiisikiliza baada ya kuwatia hatiani kwa makosa yote mawili yaliyokuwa yakiwakabili.
Shamimu, anayemiliki blog ya 8020 na mumewe Nsembo, maarufu kama Abdulkadinda, mfanyabiashara walikuwa wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini gramu 439.70, wakidaiwa kutenda kosa hilo Mei Mosi 2019, eneo la Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.
Akisoma hukumu hiyo leo, Jaji Luvanda alisema kuwa baada ya kupitia ushahidi wa upande wa mashtaka kwa mashahidi wake wanane na utetezi wa washtakiwa wenyewe, ameridhika upande wa mashtaka umethibitisha mashtaka dhidi yao bila kuacha mashaka yoyote.
“Hivyo mahakama hii inawatia hatiani washtakiwa wote kwa makosa yote mawili kama ambavyo mnashtakiwa,” alisema Jaji Luvanda kuongeza:
“Kwa hiyo Mahakama hii inawahukumu adhabu ya kutumikia kifungo cha maisha jela. Haki ya kukata rufaa inaelezwa kwa upande wowote ambao utakuwa haujaridhika,” alisema Luvanda.
Kabla ya kutoa adhabu hiyo, upande wa mashtaka kupitia kwa Wakili wa Serikali Veronica Matipila, uliieleza Mahakama hiyo kuwa hawana kumbukumbu za nyuma za makosa ya washtakiwa.
Mawakili wa washtakwa hao wameiomba Mahakama hiyo iwapunguzie adhabu.
Wakili Juma Nassoro aliieleza mahakama hiyo kuwa mshtakiwa wa kwanza, Nsembo ni mkosaji wa mara ya kwanza na ana watoto watatu ambao wanamtegemea kwa ajili ya huduma na matunzo, na kwamba kama atapewa adhabu kali basi wataathirika zaidi.
Naye Wakili Ajra Mungula kwa niaba ya mshtakiwa wa pili, Shamimu ameileza Mahakama kuwa mshtakiwa ni mkosaji wa mara ya kwanza na kwamba naye ana watoto watatu ambao bado wanahitaji matunzo na malezi yake.
Akitoa adhabu, Jaji Luvanda alisema kwamba amesikiliza na kuzingatia hatua zote za utetezi, lakini amezingatia sheria.
Jaji Luvanda alisema kuwa kwa mujibu wa makosa waliyoshtakiwa nayo, sheria inalekeza kuwa wakitiwa hatiani adhabu yake ni kifungo cha maisha.
Hukumu hiyo imepokewa kwa hisia kali za uchungu kwa wanandoa hao pamoja na wanafamilia na ndugu zao wengine, kwani baadhi wameangua vilio, huku wakiwasukuma baadhi ya wanahabari hasa wapiga picha ili wasiwapige picha.
Ilivyokuwa
Wanandoa hao walikutwa na dawa za kulevya aina ya heroin Mei 2019 zenye uzito wa zaidi ya gramu 400 nyumbani kwao Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam.
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya (DCEA) ilieleza kuwa wanandoa hao walikamatwa baada ya kukamatwa kwa mtandao mkubwa wa dawa hizo.
Maofisa wa DCEA baada ya kupata taarifa walikwenda nyumbani kwa watuhumiwa hao na kufanya upekuzi na kubaini mfuko ukiwa na dawa hizo za kulevya na nyingine zilikutwa katika siti ya nyuma ya gari katika upekuzi uliofanyika kwa saa sita.