Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wataalamu wa masoko sasa hakuna haja ya kwenda London, Nairobi

Muktasari:

  • Ni baada ya Chama cha Wataalamu wa Masoko Tanzania (TMSA) kuingia makubaliano rasmi na Chuo cha Masoko cha Uingereza (CIM) kwa lengo la kutoa kozi za taaluma ya masoko zinazotambulika kimataifa.

Dar es Salaam. Chama cha Wataalamu wa Masoko Tanzania (TMSA) kimeingia makubaliano rasmi na Chuo cha Masoko cha Uingereza (CIM) kwa lengo la kutoa kozi za taaluma ya masoko zinazotambulika kimataifa, hatua inayolenga kuinua ubora wa wataalamu wa fani hiyo nchini.

Akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo, Mkurugenzi wa TMSA, Profesa Emmanuel Chao alisema hatua hiyo inaondoa hitaji kwa wataalamu wa masoko kusafiri hadi Uingereza au Kenya ili kupata mafunzo ya ubobezi.

"Kuanzia sasa, kupitia ushirikiano huu, kozi zitakazotolewa na TMSA zitakuwa na hadhi ya kimataifa kwani zitatambuliwa na CIM ambao wana uzoefu wa zaidi ya miaka 100 katika kutoa mafunzo ya masoko," alisema Profesa Chao.

Alifafanua kuwa makubaliano hayo yatahusu pia uandaaji wa mitaala, ambapo wataalamu wa pande zote mbili watashirikiana kuhakikisha kozi zinazotolewa zinakidhi viwango vya kimataifa.

"Dunia ya sasa imebadilika sana. Mapinduzi ya kidijitali yameleta changamoto mpya katika sekta ya masoko. Ili tuendelee kuwa na ushindani, tunahitaji mafunzo ya kisasa yanayowapa wataalamu ujuzi wa kukabiliana na mazingira mapya ya kidijitali," alisema Profesa Chao.

Akizungumza kuhusu makubaliano hayo, Mtaalamu wa Masoko na Mauzo Kanda ya Afrika Mashariki, Moreen Njeri alisema hatua hiyo ni ya kihistoria kwa kuwa inaleta elimu ya ubobezi karibu na wataalamu wa ndani.

“Hapo awali ili kupata cheti cha CIM ilikuwa ni lazima kusafiri kwenda Uingereza au Kenya, lakini sasa Watanzania wataweza kupata mafunzo hayo hapahapa nchini, jambo litakalopunguza gharama na kuongeza wigo wa ushiriki,” alisema Njeri.

Kwa upande wake, Ofisa Masoko wa Bodi ya Chai Tanzania, Suleiman Chillo alisema ushirikiano huo utasaidia kuongeza uwezo wa wataalamu wa ndani kutangaza bidhaa za Tanzania katika masoko ya kimataifa.

“Tutakuwa na ujuzi sahihi wa kuvipeleka bidhaa zetu nje ya nchi, jambo ambalo litachangia kuongeza mauzo na mapato ya Taifa,” alisema Chillo.

Kwa hatua hii, Tanzania inajiweka kwenye ramani ya nchi zinazowekeza katika kukuza taaluma ya masoko kitaifa na kimataifa, kwa lengo la kuongeza ufanisi na ushindani katika soko la dunia.