Tanzania yajipanga na ushuru mpya wa Trump

Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dk Yamungu Kayandabila
Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imechukua hatua ya kulinda ukuaji wa uchumi ikiwa ni siku mbili baada ya Rais Marekani, Donald Trump kutangaza hali ya dharura ya kiuchumi nchini mwake iliyokwenda sambamba kuwekwa kwa ushuru wa angalau asilimia 10 kwa kila bidhaa inayoingia nchini humo.
Katika tangazo lake Trump amesema kuanzia Aprili 5, ushuru huo utaanza kutozwa lengo la kulinda viwanda vya ndani, aliielezea uamuzi huo kama hatua ya kuelekea uhuru mkubwa wa kiuchumi kwa Marekani, akisisitiza ajenda yake ya "Marekani Kwanza."
Kutokana na hatua za Trump na sababu nyinginezo, kamati ya Sera ya fedha iliyokutana jana Aprili 3, 2025 na kufanya tathmini ya mwenendo wa uchumi na mwelekeo wake katika robo ya pili ya mwaka 2025 imeamua riba ya Benki Kuu (BoT) kuendelea kuwa asilimia 6.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Aprili 4, 2025, Naibu Gavana wa BoT, Dk Yamungu Kayandabila mwenendo wa uchumi wa Tanzania ni mzuri lakini, kutokutabirika kwa sera za biashara na migogoro ya kisiasa duniani inaweza kuathiri mwelekeo wa mfumuko wa bei na ukuaji wa uchumi katika kufikia malengo yake.
“Wote tuliona kilichotokea jana tariff (ushuru) zimeanza na hao ndiyo wakubwa wa duni, kunapokosekana utulivu katika biashara ikiwemo kubadilika kwa sera za kiuchumi na kibiashara husuani kwa mataifa yaliyoendelea huathiri ufanisi wa ukuaji wetu,” amesema Dk Kayandabila.
Amesema katika mazingira ya kiuchumi kama yaliyopo hivi sasa Benki Kuu nyingi humua kupunguza riba au kuacha kiwango hichohicho, hivyo uamuzi wa Kamati unalenga kuukinga uchumi dhidi ya athari zinazoweza kutokea kutokana na vikwazo vya kibiashara na migogoro ya kisiasa duniani.
“Suala la mtikisiko wa kiuchumi unaoweza kutokea kutokana na yanayoendelea duniani, Serikali imeunda timu na sisi ni wajumbe kwa ajili ya kufanyia kazi yote yanayoendelea,” amesema Dk Kayandabila anayesimamia uchumi na sera za fedha.
Katika robo ya kwanza ya mwaka 2025, hali ya ukwasi iliimarika, kutokana na ongezeko la matumizi ya Serikali pamoja na kupungua kwa fedha taslimu nje ya mfumo wa benki. Kutokana na mwenendo huu, benki zilipunguza mahitaji ya mikopo kutoka Benki Kuu.
Katika kipindi hicho ukuaji wa uchumi wa Tanzania unakadiriwa kufikia asilimia 5.5. ukuaji huo unatarajiwa kuendelea kukua kwa kasi ya kuridhisha katika robo ya pili ya mwaka 2025, ukifikia asilimia 6.1, Tanzania Bara na asilimia 6.5 kwa Zanzibar.
Aidha Dk Kayandabila amesema pamoja na changamoto hizo pamoja na changamoto zinazoweza kujitokeza ana imani kuwa ukuaji wa uchumi utakuwa kama ulivyotarajiwa kwa kuwa hautegemei shughuli moja ya kiuchumi.
“Sisi tuna vitu vingi vinavyochangia ukuaji wetu wa uchumi, tuna dhahabu, tuna korosho, tuna utalii, pamba, tumbaku na hata usafishaji. Hatutarajii uingizaji wa bidhaa kupanda kwa kiwango kikubwa, kwa kiwango kikubwa tunatumia fedha nyingi kuagiza mafuta ambayo mwenendo wake unaonyesha bei yake itakuwa dola 60 hadi 70 kwa pipa moja,” amesema.
Katika mkutano huo Mwenyekiti wa umoja wa mabenki Tanzania (TBA), Theobald Sabi ameipongeza Serikali kwa usimamizi mzuri wa uchumi akisema takwimu zilizotolewa zinaonyesha ufanisi wa maeneo muhimu ya kiuchumi.
“Nashukuru pia kwa msaada wa karibu ambao BoT imekuwa ikitupatia ikiwa ni pamoja na mwaka jana wakati wa tatizo la ukwasi na mwaka huu mwanzoni,” amesema Sabi ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa benki ya NBC.
Hatua za Trump na athari zake
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade), mizania ya biashara kati ya Tanzania na Marekani imekuwa ikiegemeza zaidi Marekani katika miaka ya hivi karibuni, huku ripoti ya hivi karibuni kutoka BoT ikionyesha pengo linalopanuka la kibiashara.
Mwaka wa fedha wa 2023/24, Tanzania iliuza bidhaa zenye thamani ya Sh255.6 bilioni kwenda Marekani, huku bidhaa zilizoagizwa kutoka Marekani zikifikia Sh950.2 bilioni.
Bidhaa kuu zinazouzwa na Tanzania kwenda Marekani ni pamoja na kunde (maharagwe), kahawa, nguo, madini ya thamani, korosho, kakao, nta ya nyuki na ngozi. Marekani huuza kwa Tanzania vifaa vya maabara, mitambo, vifaa vya kielektroniki, na bidhaa za dawa.
Mchambuzi huru wa masuala ya uchumi, Oscar Mkude, alionya kuwa uamuzi wa Trump unaweza kuwa janga kwa biashara ya dunia, ambayo ilikuwa inaanza kurejea baada ya janga la Uviko-19.
"Nchi zinazotegemea mauzo ya nje kwenda Marekani zitakumbwa na athari kubwa za kiuchumi, hali ambayo itasababisha mfumuko wa bei na athari hizi katika biashara duniani," alisema.
Sekta za viwanda na ajira katika nchi hizo huenda zikakumbwa na misukosuko mikubwa, ikiwa ni pamoja na kupotea kwa ajira na kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi, aliongeza Mkude.
Mkude pia alieleza wasiwasi wake juu ya kumalizika kwa Mpango wa Ukuaji wa Kiuchumi wa Afrika na Fursa za Biashara (AGOA) ifikapo Septemba 2025. Ikiwa hautaongezwa muda wake, Tanzania na mataifa mengine ya Afrika yanaweza kukabiliwa na changamoto zaidi za kibiashara.
Hali hii, kwa mujibu wa Mkude, inaweza kuongeza mvutano katika mahusiano ya kimataifa na hata kusababisha migogoro ya kijiografia.
"Ukuaji wa uchumi wa dunia ulikuwa tayari haujawa imara, na kwa msukosuko huu mpya, hatari ya uchumi wa dunia kuingia kwenye mdororo mkubwa zaidi. Marekani ina nafasi muhimu katika uchumi wa dunia, hivyo kasi yake ya ukuaji inapopungua, athari zake huenea kote duniani," amesema.
Mkude pia amesisitiza kuwa mataifa yenye madeni makubwa yatakabiliwa na changamoto zaidi katika kulipa madeni yao. Ameshauri mataifa haya yajikite katika kupanua wigo wa uzalishaji wa bidhaa zenye thamani ya juu ambazo bado zinaweza kuvutia soko la Marekani.
Mchambuzi wa uchumi Profesa Abel Kinyondo amekiri kuwa ingawa ushuru huu utasababisha kuongezeka kwa gharama za bidhaa za bei nafuu kutoka nje hasa za kiteknolojia lakini unaweza kuwa na athari chanya kwa biashara ya dunia.
"Dunia imekuwa ikitegemea sana Marekani kwa bidhaa na utulivu wa uchumi. Kwa muda mrefu, hatua hizi za ushuru zinaweza kulazimisha mataifa kupunguza utegemezi huu, na hivyo kubadili mizania ya uchumi wa dunia na kuzalisha fursa mpya za biashara kwingineko," amesema.
Hata hivyo, mchambuzi wa masuala ya fedha, Christopher Makombe, ameonya kuwa Tanzania inaweza kukumbwa na kupungua kwa mahitaji ya malighafi zake, ikiwemo chuma na bidhaa za kilimo, kutokana na ushuru huu.
Hali hii inaweza kusababisha kuimarika kwa thamani ya dola ya Marekani hivyo kuifanya Tanzania iwe na ugumu zaidi wa kulipa madeni yaliyo katika dola. Kuongezeka kwa mfumuko wa bei nchini Marekani kunaweza pia kusababisha kupanda kwa viwango vya riba, jambo ambalo linaweza kufanya ulipaji wa madeni kuwa mgumu zaidi.
"Kampuni za Marekani huenda zikapunguza uwekezaji nje ya Marekani ili kuepuka ushuru huu, jambo ambalo linaweza kuathiri moja kwa moja miradi inayofadhiliwa na Marekani nchini Tanzania."
Licha ya changamoto hizi, Makombe anaona fursa kwa Tanzania. "Kampuni zinazohamisha mistari yao ya uzalishaji kutoka China ili kuepuka ushuru wa asilimia 54 wa Marekani zinaweza kuona Tanzania kama chaguo mbadala. Hata hivyo, ukosefu wa miundombinu bora na uwezo mdogo wa viwanda unafanya Tanzania isiwe na ushindani mkubwa kama mataifa ya Kusini-mashariki mwa Asia."
Maumivu kwa wengine
Tangazo la ushuru wa kimataifa wa Trump limeleta mshtuko mkubwa, Mataifa kama China, Canada, Mexico, na India yamekumbwa na viwango vya juu zaidi vya ushuru, huku China ikikabiliwa na ushuru wa asilimia 54 kwenye bidhaa zake zinazoingia Marekani.
Tangazo hilo lilisababisha msukosuko mkubwa katika masoko ya hisa, ambapo hisa za Marekani na Asia ziliporomoka lakini bei ya dhahabu imepanda kutokana na wawekezaji kutafuta mali salama zaidi, huku wachumi wakionya kuwa ushuru huu unaweza kusababisha mdororo wa uchumi wa dunia.
Mataifa mengine pia yameonyesha wasiwasi, huku Taiwan ikikosoa ushuru wa asilimia 32 uliowekwa kwa bidhaa zake, ikitaja kuwa "haukubaliki."
Hata hivyo, sekta ya vifaa vya teknolojia kama ‘semiconductors’ ya Taiwan imeondolewa kwenye ushuru huo. Korea Kusini nayo inakabiliwa na athari za ushuru huu, pamoja na hali ya sitofahamu ya kisiasa nchini humo.
Umoja wa Ulaya pia umeeleza wasiwasi wake kuhusu ushuru wa asilimia 20 uliowekwa na Marekani, ukisema kuwa ni pigo kubwa kwa uchumi wa dunia.
Japan, ambayo bidhaa zake zitatozwa ushuru wa asilimia 24, imeeleza masikitiko yake juu ya uamuzi huo, lakini bado haijatangaza hatua za kujibu.
Vivyo hivyo, New Zealand imekosoa ushuru huo, ikionya kuwa unaweza kusababisha kupanda kwa bei na mfumuko wa bei nchini Marekani. Hata hivyo, athari za kiuchumi za uamuzi huu kwa dunia nzima huenda zikahisiwa kwa miaka mingi ijayo.