Jinamizi la ajali Mbwewe, kiini hiki hapa

Muktasari:

  • Jinamizi la ajali linalowatesa wananchi wa Mbwewe linalotokea katika barabara kuu ya Pwani-Tanga, wananchi wanasema ni mwendokasi wa magari, wembamba wa barabara na kukosekana kwa vidhibiti mwendo.

Pwani. “Tumechoka kuzika wapendwa wetu,” hii ni kauli ya wananchi wa Kata ya Mbwewe, Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani wakielezea madhila ya ajali za kila mara katika eneo hilo na kutaja sababu tatu kuwa ndio kiini cha tatizo hilo.

Jinamizi hilo linalowatesa wananchi hao linatokea katika barabara kuu ya Pwani-Tanga, huku wananchi wakitaja kiini cha ajali hizo kuwa ni mwendokasi wa magari, wembamba wa barabara na kukosekana kwa vidhibiti mwendo.

Jinamizi la ajali Mbwewe, kiini hiki hapa

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Pius Lutuma, Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroad), Baraka Mwambage na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Halima Okash, kila mmoja amezungumzia kile anachokifahamu kuhusu ajali hizo.

Wakizungumza na Mwananchi Digital kwa nyakati tofauti juzi na jana, wananchi wa Kitongoji cha Mbwewe Voda katika kijiji cha Mpaji, wanasema miongoni mwa maeneo ambako ajali hutokea ni kijijini hapo na wananchi wengi wamepoteza maisha.

Miongoni mwa waliofariki dunia ni wanafunzi waliogongwa na magari wakati wakivuka barabara. Jambo hili mara kadhaa limeibua hasira za wananchi na kuamua kufunga barabara wakishinikiza mamlaka kujenga matuta.

Mkazi wa kitongoji hicho, Mrisho Seif anasema chanzo cha ajali ni mwendo kasi wa madereva, kutoheshimiwa alama za barabarani kwa baadhi ya madereva na kukosekana matuta sehemu hatarishi za makazi.

Anatolea mfano eneo la Mbwewe Voda, akisema kipo kivuko cha waenda kwa miguu na kibao cha spidi 50, lakini magari hasa madogo yanapita mwendo kasi wa zaidi ya spidi 50, hali inayosababisha ajali.

Kwa mujibu wa mwananchi huyo, ameshuhudia vifo vya wanafunzi watano kwa siku tofauti na watu wazima wamegongwa na magari wakati wakivuka aidha kwenda shuleni au upande wa pili wa kijiji kupata huduma za kijamii.

“Changamoto inayosababisha ajali nyingi kwenye eneo letu la Mbwewe, barabara  imenyooka sana, hivyo madereva wanatembea kwa mwendo kasi, pia licha ya kuwepo alama za barabarani hawaziheshimu,” anasema Mrisho.

Mwananchi huyo akaongeza kusema; “Madereva (baadhi) wanapita kama hakuna alama yoyote hapo barabarani, hivyo ni vizuri Serikali kuangalia uwezekano wa kuweka tuta kwenye sehemu hatari, ili kuepusha ajali hizi.”

Kwa upande wake, Halima Salim naye pia anashauri kuwekwa matuta katika sehemu zote hatarishi kwa sababu ameshuhudia ajali za watu kugongwa na kufariki dunia na matukio yake yanahusisha gari za Serikali kama ilivyotokea Aprili mosi, mwaka huu.

Katika ajali hiyo, gari la Serikali ambalo ni la Mahakama ya Lushoto linadaiwa kumgonga mwanafunzi wa Shule ya Msingi Amani Voda, Hamis Mchechelwa na kufariki papo hapo na kufanya idadi ya wanafunzi waliokufa kwa kugongwa na magari kufikia 11.


Waathirika wa ajali wafunguka

Mkazi wa Mbwewe Voda, Idrisa Seif anasema  aliwahi kugongwa na gari ila kwa bahati nzuri alinusurika kifo.

Anasema chanzo cha ajali alikuwa akivuka barabara na gari lilikuja na kasi na kumgonga, ila alipatiwa matibabu na kupona.

Anasema katika ajali hizo mtu akipona hapati fidia yoyote, hasa kwenye gari za Serikali kwa sababu wanapofuatilia wanaambiwa hazina bima, hivyo mwananchi hata kama amepata ulemavu hawezi kupata stahiki yoyote.

Mwajuma Ngude (56) anasema mtoto wake wa miaka 18 alifariki dunia kwa kugongwa na gari katika eneo hilo la Mbwewe Voda na alikuwa anatarajiwa kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza mwaka huu.

“Mwanangu wakati anapata ajali mwaka jana na kufariki duniani hapo hapo alikuwa ameshamaliza elimu ya msingi na kuchaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari, ila ndoto zake zilikatishwa na ajali ile,” anasema Mwajuma.

Akisimulia kwa uchungu, Mwajuma anasema kuna umuhimu wa mamlaka husika kusimamia na kuchukua hatua kwa wavunjifu wa sheria, kwa sababu baadhi ya madereva wanavunja sheria kwa makusudi kwa kuendesha kwa kasi magari yao maeneo yasiyoruhusiwa kupita kwa mwendo huo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mpaji, Abasi Matua anakiri kushuhudia ajali tano kwenye kitongoji hicho cha Mbwewe Voda.

Anasema wananchi wake wamegongwa na magari na kufariki dunia, wakiwamo wanafunzi wa shule ya msingi iliyopo kwenye eneo hilo.

Anasema upande  wa mashariki wa eneo hilo kuna shule, hivyo wanafunzi hutoka upande wa magharibi, wanavuka kwenda shule na baadaye kurudi, ila wakikosa mtu wa  kuwavusha ndio inakuwa changamoto kwao na ajali kutokea.

“Ni mtoto wa tano huyu sasa kugongwa baada ya kushuhudia huyu mwingine aliyegongwa na kufariki jana, makubaliano sasa na wananchi wameomba wawekewe matuta kwenye eneo hili, ili iwe kama suluhisho,” anasema.

Kauli ya Jeshi la Polisi

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Pius Lutuma amesema wanaendelea kutoa elimu kwa madereva na watumiaji wengine wa barabara, kuhusu kuzingatia sheria za barabarani kwa sababu wapo wanaovunja sheria kwa makusudi.

Kamanda Lutuma amesema Jeshi la Polisi haliwezi kuweka askari kila sehemu barabarani, ila linasisitiza kila mmoja kuzingatia sheria na kuzifuata na kila mtumiaji wa barabara kuwa mstaarabu, lengo likiwa ni kupunguza ajali na vifo kwa wananchi.

“Huwezi kuweka askari kwa kila kipande na kona ya barabara kila sehemu, la msingi ni ustaarabu wa madereva na watumiaji wa barabara kuzingatia sheria bila kumuona polisi, kwani haipendezi watu kufuata sheria akiona polisi. Sio sahihi,” amesema.

Kwa upande wake, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Pwani, Edson Mwakihaba amesema katika barabara hiyo ya Pwani kwenda Tanga, alama nyingi za barabarani zimewekwa, ikiwemo eneo hilo la Mbwewe Voda na sehemu nyingne.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Pius Lutuma akizungumza na waandishi wa habari Novemba 14, 2023. Picha na Maktaba

Amesema changamoto iliyopo ni watumiaji wa barabara, wakiwamo madereva kushindwa kuzingatia sheria wakiwa barabarani na hivyo kusababisha ajali ambazo zimekuwa zikichangia kupoteza maisha ya watu karibu kila siku.

“Vibao vipo, alama zipo na michoro ya barabarani ipo, labda matuta ndio ya kufanyia kazi, lakini suala la usalama barabarani ni jukumu la wadau wote na lazima waangalie hili,” amesema bosi huyo wa Trafiki Pwani na kuongeza;-

“Changamoto iliyopo adhabu anayopewa dereva anayefanya tukio la mauaji bado haikidhi haja, mtu anaua anatozwa faini ya Sh70,000 mpaka Sh100,000 anaachiwa, hii inatakiwa kuangaliwa upya haisaidii,” amesema Kamanda Edson.


Tanroads kuhusu barabara

Meneja wa Tanroads Mkoa wa Pwani, Mwambage anasema mkoa huo una barabara kubwa 18 zenye urefu wa kilomita 1,300 na wapo kwenye mpango wa kuangalia ni jinsi gani zitafanyiwa matengenezo na marekebisho.

Kuhusu suala la matuta, meneja huyo wa Tanroads anasema sio suluhisho la ajali barabarani, hivyo wapo kwenye mpango wa kuangalia ni jinsi gani watasaidia kuthibiti ajali zinazoendelea kutokea sehemu mbali za mkoa huo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya Bagamoyo, Halima Okash amewataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi pindi kunapotokea ajali za barabarani, kwani kwa kufanya hivyo ni kosa kisheria na wanaweza kujikuta wanaishia gerezani.

Amesema Serikali inatafuta njia bora za kudhibiti ajali za mara kwa mara eneo hilo na kwamba wakati muarubaini ukitafutwa, sio jambo sahihi kwa wananchi kuvunja sheria kwa kufunga barabara kama ilivyotokea April mosi, 2024 kijijini hapo.

Kata ya Mbwewe ni moja ya maeneo ambayo yanatajwa kutokea ajali nyingi nchini ambazo husababisha vifo kwa wenyeji, wanafunzi pamoja na wasafiri wanaotumia barabara hiyo inayounganisha mkoa wa Pwani na Tanga.

Nyingi ya ajali ziliripotiwa kutokea mwaka jana kwa nyakati tofauti na kusababisha vifo kadhaa, wengi waliopoteza maisha ni wanafamilia waliokuwa wakisafiri kati ya Agosti na Desemba mwaka jana wakiwemo wanaokwenda msibani.

Agosti 2, 2023 kulitokea ajali iliyosababisha vifo vya watu watatu akiwemo Nora Msuya aliyekuwa Meneja wa Benki ya ABSA na watu wengine wawili waliokuwemo kwenye gari hilo, wote wakiwa ni wa familia moja.

Pia siku hiyo hiyo, mke wa diwani wa Kabuku, Nurudin Semnangwa alifariki dunia yeye, mtoto wake mdogo na dada wa kazi wakitokea Dar es Salaam kwenda Handeni, hivyo watu watatu walifariki dunia kwa wakati mmoja.

Pia Desemba 28, 2023 kulitokea ajali na kusababisha vifo vya watu wanne wa familia moja waliokuwa wakielekea kwenye msiba mkoani Kilimanjaro wakitokea Dar es Salaam ambapo kwa ajali hizo tatu watu 10 walifariki.