Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jina la Rais Samia linavyotumiwa turufu ya wabunge kurudi mjengoni

Muktasari:

  • Watakiana kheri kila mmoja akimwombea mwenzake kurudi katika Bunge la 13 na kuwaambia wapigakura bado wananguvu na upendo wa kuwatumikia.

Dodoma. Zikiwa zimebakia siku 11 Rais Samia Suluhu Hassan kulifunga Bunge la Tanzania, wabunge wameanza kuaga na kutumia mjadala wa bajeti kuu kwa kutakiana mema katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.

Hata hivyo, leo Jumanne Juni 17, 2025 wengi wameonekana kutumia jina la Rais Samia kutaka kurejea mjengoni kutokana na namna wanavyomsifia na kuzitaja kazi nyingi zilizofanywa na Serikali katika majimbo yao kwa miaka minne ya kipindi cha utawala wake.

Juni 27, 2025 Rais Samia atalihutubia Bunge na kulifunga ili kutoa fursa ya kwenda kwenye uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na urais huku vyama vingine navyo vikiwa vimeshatangaza wagombea wao huku Samia akipewa nafasi kwa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Salamu za kutakiana kheri zimetawala wakati wabunge wakichangia bajeti kuu ya Serikali ya 2025/26 itakayohitimishwa kwa kupigiwa kura Juni 24, 2025 siku nne kabla ya kuvunjwa kwa Bunge.

Baadhi ya wabunge wanasifu mafanikio ya Serikali huku kila mmoja akilitaja jina la Rais Samia kama ni turufu kwao itakayowarejesha katika Bunge la 13 litakalozinduliwa Novemba kama uchaguzi utakwenda kama ulivyopangwa.

Mbunge wa Arusha Mjini, (CCM), Mrisho Gambo amemwagia nyingi kwa Rais Samia huku akitaja miradi mikubwa aliyosema inakwenda kumbeba katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu na kumrudisha kwa kishindo.

Picha na Edwin Mjwahuzi

Gambo ametaja baadhi ya miradi ambayo imejengwa katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia ni ujenzi wa Uwanja wa Afcon, malipo ya fidia kwa wananchi wa ya Mushono waliokuwa na mgogoro na Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ) na sasa wameanza kulipa Sh2 bilioni.

“Tunasema Rais Samia mitano tena, kwani tulipoleta hoja zenye masilahi alitusikia na kufanyia kazi, maduka ya ubadirishaji wa fedha na watu waliokuwa wamechukuliwa fedha zao zimerudishwa na wengine wanaendelea kurudishiwa, kuna barabara nyingi ikiwamo ujenzi wa barabara ya kwa Murombo, Kisongo, Orasiti,” amesema Gambo.

Mchango wa Gambo ulimuibua Naibu Spika, Mussa Zungu akisema kila mbunge atakayeorodhesha miradi iliyofanywa na Serikali angemuongezea muda kwa kuwa hiki ni kipindi cha kueleza mafanikio yaliyofanya na Serikali.

Mbunge wa Makete (CCM), Festo Sanga amesema kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa Serikali, kuna vifo 1,400 vya waendesha bodaboda, huku akishauri Wizara ya Fedha na Wizara ya Mambo ya Ndani kuangalia jinsi gani wanaweza kuunganisha bima ya afya na leseni.

“Ili bodaboda wanapopata leseni ndani yake hapo hapo kuwe na bima ya afya kwa sababu ni moja, vijana wanapata ajali lakini wengi wanapata changamoto  kwenye matibabu kwa kuwa bodaboda zao ni mali ya matajiri wao,” amesema Sanga.

Hata hivyo, Sanga amewaomba wananchi wa jimbo lake kumrudisha tena bungeni akisema, hiki ni kipindi chake cha kwanza, hivyo anaamini akirudi atafanya makubwa zaidi chini ya Rais Samia.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Neema Lugangira ameshauri Serikali kutanua wigo wa walipa kodi hasa kutoka sekta isiyo rasmi ili waweze kuchangia ukuaji wa pato la Taifa.

Lugangira amesema heshima ya Mtanzania iwe katika ulipaji wa kodi ili kujenga nidhamu ya kujitegemea kwa mapato kwa kuwa ndipo kipimo cha kukua kwa uchumi.

“Napenda kurejea kuikumbusha Serikali kwamba, katika kila Sh10 inayozunguka kwenye uchumi wa Tanzania Sh6 ipo kwenye uchumi wa sekta isiyo rasmi, hivyo ni muhimu sana Serikali iweke jitihada thabiti kuhakikisha tunarasimisha biashara ambazo zipo kwenye sekta isiyo rasmi.

“Serikali ione namna ya kubadilisha sheria ili biashara zinazoanzishwa na vijana, wanawake na watu wenye ulemavu wapate likizo ya kulipa kodi kwa angalau miaka mitatu kwa sababu wawekezaji kutoka nje wanapata likizo ya kulipa kodi mpaka miaka mitano, hatua hii itatanua wigo wa walipa kodi,” amesema.

Amesema lazima Serikali ifunge mkanda ipunguze gharama zisizo za lazima katika bajeti yake na ifanye tathmini ya gharama zote ili iweze kuondoa gharama ambazo sio za lazima.

“Spika alishawahi kulisemea bungeni, utakuta magari ya Serikali yanaunguruma hata saa nne hadi tano Serikali inaingia gharama ya mafuta pasipo ulazima kwa hiyo niombe Serikali ikafanye tathmini ya gharama za uendeshaji ili kuziondoa,” amesema Lugangira.

Wabunge wengine waliotembea na turufu ya jina la Rais Samia ni Mbunge wa Makambako (CCM), Deo Sanga akisema katika maisha yake hajaona kiongozi mwenye upendo kwa wananchi kama Rais Samia na jinsi alivyowasaidia kuyafikia malengo yao.

Sanga amesema kuna miradi mingi ambayo haihesabiki, lakini shule zimejengwa na vituo vya afya kwa upendeleo mkubwa unaowafanya wananchi wa jimbo lake wasiwe na deni na kiongozi huyo mkuu wa nchi.

“Tunasubiri Oktoba ifike tufanye kazi moja ya kukurudisha Ikulu, hata hivyo niwatakie mema wabunge wote ili mrudi tena hapa, niwaambie wananchi wa Makambako kuwa bado nina nguvu na upendo wa kuwatumikia, naomba msiniache,” amesema Sanga.

Mbunge huyo amesisitiza wananchi wanapaswa kuwapuuza watu mbalimbali wanaopita na kudanganya kuwa Serikali haijafanya kitu akisema kundi hilo haliitakii mema nchi hii.

Mbunge wa Bahi (CCM), Keneth Nollo amesisitiza wananchi wa jimbo lake kumtazama akisema nguvu za kuwatumikia bado anazo na uwezo wa kufanya hivyo anaona, kwa hiyo  angetamani kuona anarudi kwa mara nyingine.

Nollo amesema kwa mambo makubwa ambayo yamefanywa na Serikali chini ya utawala wa Rais Samia ambaye alimwita ni shujaa, anaamini hakuna kitakachoshindikana.

Mbunge wa Viti Maalumu, Janejerry Ntate amewaaga wabunge wenzake huku akijinadi kuwa anaondoka lakini anaamini kuwa atarudi tena Novemba na kuendelea kuwatumikia Watanzania.

Ntate ni Mbunge wa Viti Maalumu kupitia kundi la uwakilishi wa watumishi ambao huwachagua wabunge kwa kipindi kimoja tu, amesema anawatakiwa mema wabunge wenzake lakini anajipanga kurudi kwa njia njingine bila kuitaka njia atakayotumia.

Mtindo wa kutakiana kheri ulianzia kwa mawaziri wakati wa kujibu maswali ya wabunge na waliposoma hotuba, kila mmoja alijinasibu kuomba arudishwe tena ili aendeleze kazi alizozianzisha jimboni.