Jela miaka 30 kwa kubaka bintiye

Watu saba wafikishwa kortini wakidaiwa kujipatia Sh 428milioni mali ya Tanesco

Muktasari:

  • Mahakama ya Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya, imemhukumu Ayub Jackson Asudi (34), kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kumbaka mwanae wa kumzaa wa miaka (14), mwanafunzi wa darasa la sita.

Chunya. Mahakama ya Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya, imemhukumu Ayub Jackson Asudi (34), kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kumbaka mwanae wa kumzaa wa miaka (14), mwanafunzi wa darasa la sita.

 Asudi ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Mlima Njiwa, Kata ya Mbugani amehukumiwa jana Jumatano, Agosti 3, 2022 na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, James Mhanusi.

Akisoma huku hiyo, Hakimu Mhanusi alisema siku ya tukio, mtuhumiwa alimvuta mwanae chumbani kwake kisha kumvua nguo za ndani na kumwingila kimwili.

Alisema kitendo hicho kilimsababishia maumivu makali hali iliyosababisha kutokwa damu nyingi.

Hakimu huyo alisema mara baada ya mama yake kurejea alimweleza kitendo alichofanyiwa na baba yake hivyo walikwenda kutoa taarifa ofisi ya kijiji.

Alisema baada ya hapo walikwenda kituo cha Polisi Chunya na kupewa PF 3 waliyokwenda nayo hospitali kupata vipimo vya daktari vilivyoonesha mtoto kubakwa na kuonekana na michubuko sehemu za siri.

Hakimu Mhanusi alisema baada ya kuzisikiliza pande mbili Mahakama imeridhika na ushahidi wa upande wa mashitaka hivyo kumkuta mshitakiwa ana kesi ya kujibu ambapo alimpa nafasi ya kujitetea.

Alisema katika utetezi wake, mshitakiwa aliendelea kukana kosa na kwamba siku ya tukio hakuwepo nyunbani huku akitoa tiketi za basi pia ana watoto watano na wazazi wanaomtegemea hivyo anaomba kupunguziwa adhabu.

Mshtakiwa alidai kesi hiyo imetokana na wivu wa kimapenzi kwani awali mke wake aliwahi kumkuta anamhudumia vinywaji mwanamke aliyehisi ana mahusiano naye ambapo aliahidi kumkomesha.

Mhanusi baada ya kumhukumu kifungo hicho cha miaka 30 alisema, mshitakiwa ana haki ya kukata rufaa endapo hakuridhika na uamuzi.

Kwa upande wake, Ofisa Ustawi wa Jamii, Nashitabo Mwalende akizungumzia hukumu hiyo nje ya mahakama alisema Mahakama imetenda haki kwani kumekuwa na vitendo vingi vya ukatili dhidi ya watoto na adhabu za namna hiyo zitasaidi kupunguza vitendo hivyo.