Jaji Mkuu ataka utafiti kuhusu msongo wa mawazo kwa majaji

Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma akitoa hotuba ya ufunguzi wa kongamano maalumu la kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Majaji na Mahakimu Wanawake, jijini Dar es Salaam leo Machi 10, 2024.
Muktasari:
- Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, amewataka Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (Tawja) kufanya utafiti kuhusu hali ya msongo wa mawazo kwa majaji nchini.
Dar es Salaam. Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amekitaka Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (Tawja) kufanya utafiti kuhusiana na hali ya msongo wa mawazo kwa majaji nchini.
Profesa Juma ameeleza hayo leo Jumapili, Machi 10, 2024 wakati akifungua kongamano maalumu la kusherehekea Siku ya Kimataifa ya Majaji na Mahakimu Wanawake, yenye ujumbe “Mwanamke katika utoaji haki, tafakuri ya msongo wa mawazo na majukumu ya kijinisia”
Katika hotuba yake, Profesa Juma amesema majaji na mahakimu wako katika hali ya kupata msongo wa mawazo kutokana na majukumu na mazingira yao ya kazi.
Amesema kupita mada hiyo itakuwa nafasi muhimu kutafakari kwa kina namna msongo wa mawazo unavyoathiri nafasi na mchango wa mwanamke kushiriki kikamilifu katika mfumo wa utoaji haki.
Profesa Juma amesema mada hiyo imegusa eneo jipya ambalo halijawahi kufanyiwa utafiti nchini, hivyo ameitaka Tawja kulifanyia kazi kwa kufanya utafiti kujua visababishi, yakiwemo mazingira na namna yanayavyoweza kuathiri ufanisi wa utekelezaji majukumu yao ya kutoa haki na kwamba Mahakama iko tayari kuwasaidia.
Hata hivyo, amesema katika nchi nyingine tafiti kama hizo zimeshaanza kufanyika, huku akitoa mfano nchini Marekani kuwa alisoma makala iliyoelezea utafiti wa msongo wa mawazo uliofanyika kwa majaji nchini humo.
Amesema katika utafiti ingawa haukujikita kwa majaji wanawake, lakini unatoa picha ni kwa kiasi gani majaji wanawake wanavyokutana na msongo wa mawazo wakiwa maeneo ya kazi.
Profesa Juma amesema katika utafiti huo, majaji waliofanyiwa utafiti walitakiwa kuorodhesha visababishi 37 vinavyowasababishia msongo wa mawazo na kwamba sababu mbili zilizotajwa na wengi ni matokeo ya uamuzi wao.
“Wakati mwingine uamuzi unautoa wewe mwenyewe, unamaliza kusoma hukumu unajisikia vibaya, pengine ilikuwa ni kesi yenye ukatili mkubwa na pengine ushahidi ulioletwa haukuenda kama ambavyo ungependa ule ushahidi uende,” amesema Profesa Juma na kuongeza:
“Pengine ni namna gani uamuzi yake unaweza kuathiri wale wanaohusika. Kwa mfano unaweza kutoa amri baba ndiye achukue mtoto, mama anaondoka mikono mitupu. Au unapogawa mali za mirathi, ule uamuzi unaweza kuwa umeufanya kwa mujibu wa sheria, lakini unaweza kukusababishia msongo wa mawazo.”
Amesema sababu nyingine iliyotajwa ni aina ya migogoro inayopelekwa kwao akitoa mfano wadaawa wa familia moja wanapambana na wanataka jaji aegemee upande mmoja na kwamba akijaribu kuwa katikati wakati mwingine wanamkataa.
Profesa Juma amesema kuwa jaji anapoambiwa ajitoe katika kesi wakati yeye anajua kuwa anatenda haki, hiyo pia husababisha msongo wa mawazo.
Amesema siku moja alimuuliza jaji mmoja mwanamke kuwa huwa anaona anashambuliwa sana kwenye mitandao ya kijamii, ili kujua namna anajisikia na kuhimili kutokana na hali hiyo, kwani wakati mwingine anapokuwa amefanya kazi yake kwa haki, lakini anaposhambuliwa humkatisha tamaa.
“Sisi wengine tumeshazoea, usipoandikwa wiki nzima kusemwa vibaya huwa hatujisikii vizuri kwa sababu nimeshazoea kuishi na kushambuliwa,” amesema Profesa Juma na kuongeza:
“Kuna wakati nilitaka nitengeneze mito ya kulalia na kuigawa bure, ile mito imeandikwa Ibrahim Hamisi Juma ili wale wanaonishambulia wawe wanalala usiku wanataja Ibrahim Hamis Juma. Ni njia moja ya kupambana na msongo wa mawazo.”
Profesa Juma amebainisha kuwa sababu nyingine iliyotajwa katika utafiti huo wa Marekani ni mawakili wasiojiandaa, akisema kuna wakili anaweza kufika mbele ya Jaji kuendesha kesi huku akiwa hajajiandaa, hivyo jaji hulazimika kumsaidia, kwani vinginevyo haki inaweza kupotea.
Amesema mawakili wa namna hiyo wengine ni wale ambao wanaandika sana kwenye mitandao ya kijamii, lakini wanapofika mbele ya jaji hizo wanazokuwa wameziandika mitandaoni inakuwa tofauti.
“Zile hoja wanazozijenga kwenye mitandao huwa wanashindwa kuzijenga wakiwa mbele ya jaji. Wengine tunawasaidia. Ongea hapa, fanya hivi fanya hivi. Wakipenda naweza kuwataja siku moja, au nitakapoandika kitabu changu nitawataja maana naweka kumbukumbu,” amesema Profesa Juma.
Hivyo amesema katika mazingira hayo, jaji anajikuta anafanya kazi ya ziada na kumsabishia kuchoka na kupata msongo wa mawazo.
Awali, Mwenyekiti wa Tawja, Jaji Barke Sehel amesema lengo la kongamano hilo ni kusherekea na kutambua mchango wa jaji mwanamke katika utawala wa sheria na utoaji haki na kutakari changamoto wazokutana nazo.
Amesema katika kongamano hilo watajadili vikwazo na changamoto wanazokutana nazo majaji na mahakimu wanawake na kusikia safari ya baadhi ya wanachama wao namna walivyoweza kuweka mizania ya kazi zao za ofisini na nje ya ofisi.
Jaji Sehel amesema wanawake wanakabiliwa na vikwazo na changamoto za kipekee zitokanazo na mila na desturi ambazo hazikumuandaa mwanamke kuwa kiongozi.
“Kwa ujumla jamii inategemea mwanamke mwajiriwa atekeleze majukumu yake ya msingi kwa kiwango sawa na mwanaume, wakati mazingira ya kazi ya mwanamke ni tofauti na ya mwanaume,” amesema na kuongeza;
“Kutokana na mwingiliano wa majukumu ya kifamilia na ya kikazi kunaweza kumsababishia mwanamke aliye kwenye nyanja ya utoaji haki kupata msongo wa mawazo. ndio maana tumekuja na kaulimbiu hii.”
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mary Mrio amesema kupitia kongamano hilo watapata wasaa wa kujadili mada zinazolenga utoaji wa haki.
Hakimu Mkazi Mahakama ya Mwanzo Mwanjelwa, mkoani Mbeya, Hafsa Shelimo amesema kupitia kongamano hilo watakutanishwa na wataalamu wa masuala ya msongo wa mawazo na kwamba hiyo itawaweka sawa katika kutekelea majukumu yao.
Siku ya kimataifa ya majaji na mahakimu wanawake ilitokana na Azimio ya Baraza la Umoja wa Mataifa la Aprili 28, 2021. Hii ni mara ya pili kwa maadhimisho jayp kufanyika nchini Tanzania.