Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jaji Mkuu: Haki si kushinda kesi peke yake

Jaji Mkuu wa Tanzania,Profesa Ibrahim Juma,akizungumza katika kikao cha Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu nchini, leo Jumatatu Februari 26,2024 mkoani Arusha.Picha na Janeth Mushi

Muktasari:

  • Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma azungumzia wanaotoka mahakamani kufuata kamera na video kusema haki imepotea.

Arusha. Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amesema ni muhimu elimu kutolewa kwa wananchi waelewe haki si kushinda kesi peke yake.

Amesema sheria ni mizani hivyo, aliyeshindwa pia anaweza akapata haki yake kwa kukata rufaa.

Profesa Juma amewataka majaji nchini kutokukatishwa tamaa na baadhi ya watu wanaotoka mahakamani na kudai hakuna haki wakati wameacha mizani mahakamani.

Amesema hayo leo Jumatatu Februari 26, 2024 jijini Arusha, katika ufunguzi wa kikao cha siku tatu cha majaji wafawidhi wa Mahakama Kuu Tanzania.

Amesema moja ya maeneo ya msisitizo wanayozingatia ni kusimamia shughuli za utoaji haki.

"Haki ni eneo pana sana, hivi karibuni tumekuwa tukiona mwananchi anatoka mahakamani ameshindwa, yeye haki anaiangalia kwa upande mmoja, lakini haki ni mizani na ukiiangalia ilivyo katikati kuna sheria, kuna pande mbili ambazo zinabishana zinaleta ushahidi halafu ile mizani inatoa haki," amesema Profesa Juma.

"Kwa hiyo tuendelee kuwaelimisha wananchi kwamba haki si ushindi, haki ni ushahidi ulioletwa mahakamani, sheria iliyotumika katika kutoa uamuzi, na mizani ambayo imetoa haki hii. Tumezoea siku hizi kuona wanatoka mahakamani wanatafuta kamera na video na kusema haki imepotea bila kuangalia mizani ambayo ilikuwa mahakamani. Ninaomba sana msikatishwe tamaa na wale ambao wanatoka mahakamani na kudai hamna haki wakati wameacha mizani mahakamani."

Profesa Juma amesema ni muhimu kusimamia kuimarisha, kujenga na kudumisha imani ya wananchi kwa Mahakama.

Pia, amesema ushirikiano na wadau ni lazima viongozi wawasikilize wananchi na kutumia changamoto zinazowakabili kufanya maboresho na mabadiliko.

Amesisitiza pia matumizi ya Tehama ili kuharakisha utoaji huduma.

Awali, Jaji Kiongozi, Mustapher Siyani amesema tangu kufanyika kikao kama hicho mwaka 2022 muda wa wastani unaotumika tangu shauri kufunguliwa mpaka kumalizika umepungua kutoka siku 321 hadi 262, mlundikano wa idadi ya mashauri ukipungua kutoka asilimia tano mpaka mbili, yaani kesi 896 hadi 262.

"Hali ya Mahakama za chini nayo imezidi kuwa bora ambako muda wa wastani ambao mashauri yanatumia katika Mahakama za Hakimu Mkazi umepungua kutoka siku 159 hadi siku 120 na Mahakama za Mwanzo muda huo umeongezeka kutoka siku 29 mpaka siku 30," amesema.

Jaji Siyani amesema idadi ya kesi za mlundikano katika Mahakama hizo imepungua kutoka mashauri 878 mpaka 455 katika Mahakama za Hakimu Mkazi na kutoka mashauri 915 mpaka 706 katika Mahakama za Wilaya na Mahakama za Mwanzo kutoka 19 mpaka sifuri.