Geita kupata Mahakama Kuu, mashauri kuendeshwa kidijitali

Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibarahim Juma
Muktasari:
Faida ya kufunguliwa Mahakama Kuu Geita itanufaisha pia Mahakama Kuu Mwanza ambayo hivi sasa imeelemewa na mashauri mengi kwa sababu ndiyo inahudumia pia Mkoa wa Geita.
Geita. Adha ya wakazi wa Mkoa wa Geita wenye shauri Mahakama Kuu kulazimika kusafiri hadi jijini Mwanza kufuata huduma itafkia tamati siku chache zijazo mpango wa kuwa kituo cha Mahakama Kuu mkoani humo utakapokamilika.
Akzungumza leo Oktoba 12, 2023 wakati wa mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama unofanyika mjini Geita, Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amesema mchakato wa kuwa na Mahakama Kuu Geita uko katika hatua za mwisho ikiwemo ya kupanga Majaji kutoka watakaotoka miongoni mwa Majaji walioteuliwa hivi karibuni.
Jaji Profesa Juma ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Tume ya Mahakama amesema Mahakama Kuu ya Geita itakuwa ya kipekee na ya mfano kwa Mahakama nyingine nchini kwa sababu utendaji na shughuli zake zote zitafanyika kidigitali badala ya utaratibu uliozoeleka wa makaratasi.
‘’Mahakama Kuu Geita itakuwa ya mfano na shule kwa Mahakama nyingine nchini kujifunza namna ya kuendesha mashauri yote kwa njia ya mtandao,’’ amesema Jaji Profesa Juma
Ingawa hajataja tarehe maalum ya Mahakama Kuu Geita kuanza, Kiongozi huyo mkuu wa mhimili wa Mahakama amesema tayari jengo litakalotumika limepatikana na kinachosubiriwa ni Majaji wapya kumaliza mafunzo elekezi na kupangiwa vituo ambapo miongoni mwao wamo watakaopangiwa kituo cha Geita.
Faida ya kufunguliwa Mahakama Kuu Geita itanufaisha pia Mahakama Kuu Mwanza ambayo hivi sasa imeelemewa na mashauri mengi kwa sababu ndiyo inahudumia pia Mkoa wa Geita.
Mahakama zinazotembea
Katika jitihada za kusogeza huduma kwa umma, hasa suala la mashauri kusikilizwa na kuamuliwa kwa wakakati, Jaji Mkuu amesema mchakato wa kuanzisha Mahakama zinazotembea katika mikoa ya Tabora na Morogoro unakamilishwa.
“Uongozi wa Mahakama unafanya kila jitihada kuhakikisha huduma zinasogezwa karibu na wananchi kutimiza lengo la haki kutolewa kwa muda muafaka,’’ amesema Jaji Mkuu
Amewataka watumshi wa Mahakama kusoma ripoti ya Tume ya Rais ya Haki Jinai ili kuboresha utendaji wao katika kutoa haki kwa wakati.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela ameupongeza uongozi wa Mahakama kwa kutekeleza mchakato wa kufungua Mahakama Kuu mkoani humo huku akiahidi kuwa uongozi wa Serikali mkoani humo umejipanga kutekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba na makazi ya Majaji.
Akitoa taarifa ya utendaji wa Kamati za Maadili za mkoa na wilaya za mkoa huo, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Geita, Dk Omari Sukari ametaja tuhuma za uzembe kwa baadhi ya mahakimu na watumishi wa Mahakama ni miongoni mwa malalamiko yanayowasilishwa mbele ya kamati hiyo.
‘’Malalamiko mengine ni ukiukwaji wa kanuni na maadili ya utumishi, mwenendo mbaya usiolingana na hadhi ya mahakimu, lugha zisizofaa na ucheleweshwaji wa hukumu na mwenendo wa mashauri katika Mahakama za mwanzo,’’ amesema Dk Sukari
Kukosekana kwa magereza kwenye baadhi ya wilaya za Mkoa wa Geita, baadhi ya Mahakama kukosa vitendeakazi na vifaa vya Tehama kwa waendesha Mashtaka ni changamoto nyingine zinazotajwa kuikabili idara ya Mahakama mkoani Geita.