Jafo: Wanaume Kanda ya Ziwa jitokezeni mfanyiwe tohara

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, Seleman Jafo akizungumza wakati wa uzinduzi wa magari ya huduma tembezi ya tohara kwa wanaume Jijini Dodoma.
Muktasari:
Baadhi ya wanaume wanaoishi mikoa ya Kanda ya Ziwa nchini Tanzania wameombwa kujitokeza kwa wingi kufanyiwa tohara ili kuepuka magonjwa.
Dodoma. Baadhi ya wanaume wanaoishi mikoa ya Kanda ya Ziwa nchini Tanzania wameombwa kujitokeza kwa wingi kufanyiwa tohara ili kuepuka magonjwa.
Wito huo umetolewa leo Alhamisi Machi 4, 2021 na Waziri wa Tamisemi, Seleman Jafo katika uzinduzi wa magari ya huduma tembezi ya tohara kwa wanaume yaliyotolewa na shirika la IntraHealth afya plus na yatatumika katika mikoa minne nchini.
Jafo ameitaja mikoa ya Simiyu, Mwanza, Shinyanga na Mara kuwa na kiwango cha chini kwa wanaume waliofanyiwa tohara ikilinganishwa na mikoa mingine.
Amebainisha kuwa ni muhimu vijiji katika mikoa hiyo kuwa na mashindano ya idadi ya watu waliofanyiwa tohara, akisisitiza kuwa kuna faida kubwa kwa wanaume waliotahiriwa ikiwemo kujikinga kwa asilimia 60 na maambukizi ya Ukimwi.
"Najua ni jambo gumu kidogo kuukubali ukweli lakini kama walivyosema wataalamu wetu waliofanyiwa tohara wana asilimia fulani ya kujikinga na maambukizi, hivyo tujitokeze bila aibu," amesema Jafo.