Ilala kinara matukio ya ubakaji, kutelekeza familia na vipigo

Muktasari:
- Ubakaji ni miongoni mwa makosa matatu ya kikatili yaliyoshamiri Wilaya ya Ilala huku vyombo vya usalama vikieleza jitihada zinazochukuliwa ikiwemo kutoa elimu na kushirikiana na jamii kudhibiti vitendo hivyo
Dar es Salaam. Ubakaji ni makosa kinara ya ukatili yanayoongoza katika Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam kwa kipindi cha mwaka 2023 hadi 2024 huku ikifuatiwa na matukio ya ulawiti, kutelekeza familia na kipigo.
Tatizo hilo linadhibitishwa na takwimu za Jeshi la Polisi Mkoa wa Ilala, zinazoonyesha katika kipindi hicho jumla ya matukio 215 ya ubakaji yalijitokeza kati ya hayo 198 yalijitokeza mwaka 2023 na 77 kwa mwaka 2024.
Jeshi hilo limesema pamoja na kwamba takwimu hizo zinaonyesha kupungua kwa makosa ya ukatili lakini limebaini jamii imekuwa na uoga katika kufichua vitendo vya ukatili hususan wanaume wanaogopa kuripoti kwenye madawati wakihisi wataonekanaje wanapokwenda kufanya hivyo.
Matukio ya ubakaji na ulawiti yaliyoripotiwa kwenye vitu vya jeshi la Polisi nchini Tanzania yameongezeka kutoka 23 kwa siku mwaka 2022 hadi 31 mwaka 2023.
Kwa mujibu wa takwimu hizo zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBC) zimeonyesha makosa ya ulawiti yameongezeka zaidi ya mara mbili mwaka 2023 hadi kufikia matukio 2,488 ikilinganishwa na kesi 1,205 zilizoripotiwa mwaka 2020.
Idadi hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 57 ikilinganishwa na 2022.
Hata hivyo, Mzee Jackline Alfonce, Mkazi wa Barakuda amesema makosa ya ukatili yanafanyika kwa kiwango kikubwa lakini mengi yanamalizwa kifamilia.
"Kuanzisha madawati ni jambo moja lakini jamii yenyewe inakasumba ya kutokwenda kwakuwa wanaotendeana ukatili ukifuatilia ni ndugu hivyo hawataki kufikishana mbali, wakijua kuna leo na kesho," amesema Alfonce.
Akizungumza leo Alhamisi, Desemba 5, 2024 baada ya kufanya matembezi ya kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili, Kamanda wa Polisi Ilala, Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Yustino Mgonja amesema bado wanaendelea na jitihada ya kutoa elimu kwa jamii katika kupinga vitendo hivyo.
"Makosa ya kulawiti mwaka 2023 yalikuwa 87 mwaka huu yapo 51, kutelekeza familia 2023 yalikuwa 57 mwaka huu 23 lakini upande wa kipigo mwaka 2023 yalikuwa 79 na 2024 yapo 30," amesema Kamanda Mgonja.
Pia, Kamanda Mgonja amesema katika kipindi cha mwaka huu kesi zenye mafanikio dhidi ya ukatili wa kijinsia na watoto zilizopelekwa mahakamani zilikuwa 25 na jumla ya watuhumiwa 25 walitiwa mbaroni na kutumikia adhabu mbalimbali.
"Katika mkoa wa Kipolisi Ilala eneo lilokuwa na makosa mengi ya ukatili ni Ukonga, na yalishamiri kwa sababu nyumba nyingi ziko karibukaribu sana lakini kwa sasa tumeimarisha ulinzi kwa kushirikiana na serikali za mitaa na tumeanzisha kituo," amesema.
Katika matembezi hayo yaliyohusisha wanafunzi wa shule ya msingi yalianzia Tabata Shule hadi Barakuda mgeni rasmi alikuwa afisa elimu Msingi na Awali wa Jiji la Dar es Salaam, Magreth Macha.
Akizungumza baada ya Polisi kusoma taarifa yao, Magreth amesema bado jamii inapaswa kupewa elimu ili ishiriki kikamilifu katika kudhibiti viashiria na matukio ya ukatili ambayo kwa kiasi kikubwa athari zimekuwa kubwa kwa watoto.
"Mtoto akifanyiwa ukatili kisaikolojia hawezi kuwa sawa hivyo hata darasani hawezi kufanya vizuri, na ukiangalia matukio mengi yanafanywa na jamii inayowazunguka," amesema.
Awali, Mkuu wa Mtandao wa Kipolisi Ilala, Kamshina Msaidizi Mwandamizi, Hasna Ramadhani amesema mtandao huo ulianzishwa baada ya kushamiri makosa ya udhalilishaji.
"Wote wanaofanyiwa makosa ya ukatili wanatakiwa kuja kuripoti ili wapatiwe huduma na makosa mengi yanayofanyika kwakuwa yanaingia kwenye jinai tunahikisha yanafikishwa mahakamani na kuona haki inatendeka," amesema.