Idara ya usalama kufumuliwa

Mbunge wa Viti Maalumu, Salome Makamba akizungumza bungeni alipokuwa akichangia mjadala wa kupitisha miswada mitatu iliyowasilishwa bungeni na serikali jijini Dodoma jana. Miswada iliyowasilishwa ni muswada wa sheria ya Tume ya Mipango wa mwaka 2023, Muswada wa marekebisho ya sheria ya Idara ya Usalama wa Taifa, sura ya 406 na Muswada sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali yatokanayo na urekebu wa mwaka 2023. Picha na Edwin Mjwahuzi
Walichosema wabunge
Wabunge walichangia muswada huo kabla ya kuupitisha na kusubiri saini ya Rais, huku mbunge wa Bukene (CCM), Suleiman Zedi akisema marekebisho hayo yanakwenda kuongeza majukumu ya idara ya usalama, hasa kukusanya taarifa za kiintelejensia kwa ajili ya kufanya ulinzi kwa maeneo muhimu ya kiuchumi.
Mbunge wa kiteto (CCM), Edward Ole Leikaita alisema walikubaliana katika kamati kutokana na maendeleo duniani kuna umuhimu wa kufanya maboresho kwenye sheria hiyo.
“Sheria hii inapunguza kazi za waziri (Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Menejimenti ya utumishi wa Umma na Utawala Bora) ili kazi yake ibaki ya sera na bajeti. Kuripoti kwa Rais moja kwa moja ni muhimu sana,” alisema.
Salome Makamba (viti maalumu) alisema mambo mengi yaliyopelekwa bungeni yanafanyika na kutoa mfano wa kifungu cha sheria kinachotaka kuwawezesha maofisa usalama kumiliki silaha tayari wanazimiliki.
“Kuna kifungu cha kuwalinda wananchi, viongozi wanaotakiwa kuwalinda ni viongozi wa vyama vya siasa, ukiona unaona nia njema kabisa ukija kwenye uhalisia huwezi kutofautisha taasisi hii na uongozi ulioko madarakani na TISS,” alisema.
Pia, alihoji kuhusu kifungu kinachotoa kinga kwa maofisa usalama wa Taifa wataofanya majukumu yao kwa nia njema, lakini akahoji unatofautishaje nia njema.
Waziri ajibu
Akihitimisha hoja yake, Waziri Simbachawene aligusia hoja iliyokuwa imetolewa ya kinga, akisema inawekwa kwa maofisa wakati wanatekeleza majukumu yao kisheria tu.
“Sio wewe ni ofisa usalama unakwenda kugombana huko mtaani umeitumia silaha yako vibaya eti ukasema una kinga hapana, sheria itachukua mkondo wake,” alisema.
Alisema wanazungumzia kinga katika utekelezaji wa majukumu yao na kwamba pengine watu wanayapunguza majukumu ya TISS kwa kuwaona wanalinda usalama wa ndani ya nchi tu.
Alisema chombo hicho kinalinda Taifa dhidi ya maadui wa nje ya nchi, mipango ya maendeleo na kiuchumi na kwamba vita ipo zaidi ya kwenye uchumi.
“Wananchi walioko nje tunaona mijadala mbalimbali, hakika ni kwamba hawajapitia yale mambo mazuri ambayo kamati imesimamia, lakini wabunge wanayafahamu. Taratibu tunaweza kujikuta na wenzetu tuko pamoja kwa sababu hakuna jambo lolote lililfanywa kwa nia yoyote mbaya,” alisema.
Simbachawene alisema msingi mkubwa ni amani, mshikamano na umoja na kulinda nchi kama jukumu la Watanzania.
Alisema kinga imesemwa sana mtaani, lakini wanachomaanisha ni dhidi ya magaidi.
Simbachawene alisema anapopambana na magaidi ikatokea silaha yake imempata unasema haina kinga.
Kamati yauchambua
Akisoma maoni ya Kamati ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, mwenyekiti wake, Joseph Mhagama alisema Serikali ilikubaliana na maoni ya kamati kwa sehemu kubwa, ikiwamo Ibara ya 5 (ii) kuongeza aya mpya za (e), (f), (g), (h) na (i) kwa lengo la kuboresha majukumu yanayotekelezwa kwa sasa, hasa ulinzi binafsi wa viongozi wa ngazi za juu wa kitaifa na kimataifa.
Pia, ulinzi wa wagombea urais wa nchi, ulinzi wa vituo muhimu, mamlaka ya upekuzi wa kiusalama wa viongozi na udhibiti wa matishio ya kiusalama dhidi ya Jamhuri ya Muungano.
Alitoa mfano pendekezo la kuweka masharti yanayozuia mkurugenzi mkuu wa idara kuajiriwa au kuteuliwa katika nafasi yoyote ya utumishi serikalini baada ya kuitumikia nafasi hiyo.
“Kamati ilishauri katazo hilo liondolewe, kwani linakinzana na Masharti ya Ibara ya 9 ya Katiba Tanzania, 1977…Serikali ilikubaliana na mapendekezo ya kamati kwa kufuta ibara ya 7(d) ya muswada,” alisema Mhagama.
Pia, alisema ibara ya 12 inakusudia kufanya marekebisho kwa kuongeza kifungu kipya ili kuweka masharti yatakayomwezesha katibu mkuu kiongozi kuratibu na kuwa kiungo baina ya Rais na Idara katika utekelezaji wa masuala ya kisera na utumishi wa umma.
Kamati hiyo ilisema ibara ya 14 inakusudia kufanya marekebisho Kifungu cha 13 cha Sheria kwa kukifuta na kukiandika upya kinachoweka utaratibu wa kuapishwa kwa mkurugenzi mkuu, naibu wakurugenzi wakuu, wakurugenzi na maofisa.
Kwa mujibu wa kamati hiyo, kiapo hicho kitawafunga watumishi tajwa hata baada ya utumishi wao kukoma.
Pia, ibara ya 20 inakusudia kufanya marekebisho kwenye kifungu cha 19 kwa kufuta kifungu kidogo cha 1 na kukiandika upya.
Pia, katika kifungu kidogo cha 3 kwa kufuta maneno “Attorney General” badala yake kuweka maneno “Attorney General, Director of Public Prosection or Solicitor General as the Case may be” ili kuweka kinga dhidi ya maofisa wa idara katika makosa yanayoweza kutendeka wakati wa utekelezaji wa majukumu yao kwa uaminifu.
Eneo jingine ni katika ibara ya 5(e) kinachohusu utoaji wa ulinzi kwa viongozi, kamati hiyo ilipendekeza mpangilio wa orodha ya viongozi waliowekwa katika kifungu hicho kifuate itifaki sahihi kwenye mpangilio wa viongozi na kuwaongeza wanasheria wakuu wa Tanzania na Zanzibar ili kukubali mapendekezo hayo.