Huyu ndiye Muhoozi Kainerugaba, mtoto wa Museveni

Luteni Jenerali Muhoozi Kainerugaba
Muktasari:
Kamanda wa Jeshi la Ardhini nchini Uganda (UPDF), Luteni Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ambaye ni mtoto wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni, jana Jumanne Machi 8, 2022 alitangaza kustaafu katika Jeshi hilo.
Dar es Salaam. Kamanda wa Jeshi la Ardhini nchini Uganda (UPDF), Luteni Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ambaye ni mtoto wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni, jana Jumanne Machi 8, 2022 alitangaza kustaafu katika Jeshi hilo.
Luteni Jenerali Kainerugaba alitangaza uamuzi huo kupitia ukurasa wake wa Twitter akisema ameamua kustaafu baada ya ya kuhudumu kwa miaka 28.
''Baada ya kuhudumu kwa miaka 28 katika jeshi letu, jeshi bora zaidi duniani, nafurahia kutangaza kwamba ninastaafu. Mimi na wanajeshi wangu tumefanikiwa pakubwa, ninawapenda na kuwaheshimu maofisa wote waliofanikiwa kila siku,” aliandika.
FAHAMU HISTORIA YA SAFARI YA MAISHA YA KAINERUGABA MPAKA ALIPOTANGAZA KUSTAAFU
Kuzaliwa
Kainerugaba alizaliwa Aprili 24, 1974 jijini Dar es Salaam nchini Tanzania.
Ni mtoto wa kwanza wa Rais wa Uganda, Yoweri Museveni na mkewe Janet Museveni.
Kainerugaba alilelewa na kukua katika familia ya Kikristo na mwaka 1999 alimuoa Charlotte Nankunda Kutesa.
Elimu
Alianza masomo kwa mara ya kwanza nchini Tanzania ambako ndiko alipozaliwa. Baadaye alihamishiwa Mount Kenya Academy iliyopo Nyeri nchini Kenya kabla ya kupelekwa nchini Sweden.
Baada ya baba yake kuwa Rais mwaka 1986, Kainerugaba aliliunga na Shule ya Wazazi Kampala na baadaye kujiunga na chuo cha King’s College kilichopo Budo na baadaye kuhitimu katika Chuo cha St Mary’s College Kisubi mwaka 1994.
Baadaye akajiunga na kozi ya ukamanda katika Chuo cha Kijeshi cha Misri. Pia aliwahi kusoma katika Shule ya Mafunzo ya Kivita vya Karama (KAWATS) nchini Uganda.
Mwaka 2007, Kainerugaba alidahiliwa katika Chuo cha Kamandi ya Jeshi la Merika na Chuo Kikuu cha Wafanyikazi huko Fort Leavenworth, Kansas, Missouri. Alikaa mwaka mmoja katika chuo hicho na alihitimu Juni 2008.
Baadaye Kainerugaba alifuzu mafunzo ya Usalama wa Kitaifa katika Chuo cha Kitaifa cha Ulinzi cha Afrika Kusini.
Kazi
Mwaka 1999 alijiunga na Jeshi la Uganda (UPDF) akiwa ofisa kadeti na kuhitimu shahada kutoka chuo cha mafuzo ya jeshi cha Royal Military Academy Sandhurst mwaka 2000.
Kainerugaba ni miongoni mwa wanajeshi wa Uganda walipanda vyeo haraka hadi kufikia ngazi za juu katika Jeshi hilo.
Mwaka 2003 alipandishwa cheo cha kuwa Meja na kuteuliwa kuwa Kamanda wa Kitengo cha Jeshi cha Motorised Infantry batallion, na mwanachama wa Baraza kuu la Ulinzi nchini Uganda.
Kainerugaba pia alihudhuria mafunzo ya ngazi za juu za usimamizi wa kitengo cha jeshi katika Chuo cha Kaisenyi Magharibi mwa Uganda 2005.
Mnamo mwaka 2006, Kainerugaba alisimamia mafunzo na mipango ya kitengo kipya cha jeshi katika eneo la Barlege, Kaunti ya Otuke wilayani Lira kaskazini mwa Uganda.
Alikuwa mganda wa kwanza kufuzu mafunzo ya kushambulia kwa kutumia parachute katika Jeshi la Uganda (UPDF) baada ya kumaliza mafunzo yake huko Marekani 2008, Julai. Mwaka huohuo akapandishwa cheo na kuwa Luteni Kanali na kuteuliwa kuwa kamanda wa kikosi maalumu chini ya UPDF.
Mwaka 2010 akateuliwa kuwa kamanda wa kikosi maalumu ambacho sasa kinajumuisha Kikosi cha Ulinzi wa Rais ambacho awali kilitenganishwa.
Septemba, 2011 akapandishwa cheo na kuwa kanali kabla ya kuwa Brigedia Jenerali Agosti 2012 na mwaka 2016 aliteuliwa kuwa Meja Jenerali.
Januari 2017, Muhoozi aliteuliwa kuwa mshauri wa Rais wa shughuli maalumu. Kupandishwa kwake cheo na kusogezwa Ikulu, kukaongeza maneno zaidi kwenye vyombo vya habari vya Uganda kwamba Kainerugaba ni kama anaandaliwa kuwa Rais ajaye wa Uganda kumrithi baba yake.
Mwaka 2020, Rais Museveni akamteua tena kuwa kamanda wa Kikosi Maalumu (SFC) kumrithi Meja Jenerali James Birungi. Akiendelea kuwa mshauri mwandamizi wa Rais kwenye shughuli maalumu.
Nyota ya Kainerugaba katika uongozi iliendelea kung’aa ambapo Juni 24, 2021 aliteuliwa kuwa Kamanda wa Jeshi la Ardhini nchini Uganda (UPDF), akichukua nafasi ya Luteni Jenerali Peter Elwelu ambaye aliteuliwa kuwa mkuu wa majeshi msaidizi.
Machi 8, 2022 Kainerugaba alitangaza kustaafu akiwa Kamanda wa Jeshi la Ardhini nchini Uganda (UPDF).