Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hukumu kesi ya Halima Mdee na wenzake inafumua Chadema hadi CCM

Muktasari:

  • Uamuzi wa kesi hiyo ulitolewa hivi karibuni na kuzua mjadala katika duru mbalimbali za kisiasa nchini.

Jaji Cyprian Mkeha amewapuliza Halima Mdee na wenzake upande mmoja, kisha akawang'ata sehemu nyingine. Utaratibu huohuo ameutumia dhidi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Unaweza kujenga picha hiyo endapo utaisoma hukumu ya shauri la Halima Mdee na wenzake 18 dhidi ya Bodi ya Wadhamini Chadema.

Ni kesi ya Halima na wabunge wenzake 18 wa viti maalumu, kupinga kuvuliwa uanachama wa Chadema, kama ilivyoamuliwa na Kamati Kuu ya chama hicho, Novemba 27, 2020. Kisha, wabunge hao kudai kutotendewa haki na Baraza Kuu la Chadema, Mei 11, 2022, walipohudhuria kutetea rufaa yao.

Kila kitu kilianza na matokeo ya Uchaguzi Mkuu 2020. Kipigo kikali ambacho Chadema walikipata kwenye uchaguzi, wakaambulia mbunge mmoja wa kuchaguliwa, jimbo la Nkasi Kaskazini na wabunge 19 viti maalumu. Chadema walipitisha uamuzi wa kutotambua matokeo hayo.

Katikati ya uamuzi wa Chadema, Novemba 24, 2020, Halima na wenzake 18, walikwenda bungeni na kula kiapo cha ubunge mbele ya aliyekuwa Spika, Job Ndugai. Uamuzi siyo tu ulikuwa kinyume na chama, bali pia uliibua tuhuma za kughushi saini za viongozi wa juu wa chama ili kuhalalisha uteuzi wao.

Walioapishwa, ukimuacha Halima ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), wengine ni Grace Tendega, Esther Matiko, Cecilia Pareso, Ester Bulaya, Jessica Kishoa na Hawa Mwaifunga.

Wamo pia Tunza Malapo, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Anatropia Theonest, Salome Makamba, Conchesta Rwamlaza, Agnesta Kaiza, Nusrat Hanje, Asia Mohamed, Felister Njau na Stela Fiyao.


Kung’ata na kupuliza

Ukipitia hoja kwa hoja, shahidi na shahidi, ushahidi hadi ushahidi, kesi nzima mbele ya Jaji Mkeha, ilibishaniwa kwenye maeneo matano:

Mosi, Kamati Kuu Chadema ilikuwa na mamlaka ya kikatiba, kusikiliza shauri la akina Halima kwa dharura? Je, Kamati Kuu iliwapa haki ya kusikilizwa?

Pili, Halima na wenzake walipewa haki ya kusikilizwa kwenye Baraza Kuu Chadema? Tatu, mchakato wa kuwavua uanachama ulikiuka sheria?

Nne, Baraza Kuu lilizingatia kanuni ya usawa? Tano, kama maombi ya kina Halima mahakamani yalikidhi matakwa ya kupewa haki.

Jaji Mkeha aliwapuliza akina Halima kwa uamuzi wake kwamba Baraza Kuu Chadema halikuwa na usawa na lilikiuka misingi ya haki asili , hapohapo akawang’ata aliporidhika kuwa Kamati Kuu Chadema ilikuwa na uhalali kuwavua uanachama.

Chadema walipulizwa kwa uamuzi kwamba Kamati Kuu Chadema ilikuwa na uhalali, vilevile ilikidhi matakwa ya Katiba ya chama na kanuni, kuwavua uanachama wabunge 19 wa viti maalumu.

Jaji akawang’ata Chadema kwa kuwaambia Baraza Kuu lilikosa usawa dhidi ya wabunge hao.

Mwisho kabisa, Jaji Mkeha amebatilisha uamuzi wa Baraza Kuu Chadema, uliokazia hukumu ambayo Halima na wenzake walipewa na Kamati Kuu Chadema. Wakati huohuo, Jaji Mkeha ameridhika na kila hatua iliyochukuliwa na Kamati Kuu Chadema.

Bila kuzunguka, hukumu ya Jaji Mkeha imemaanisha kuwa wote wameshinda. Mawakili wa Chadema wameshinda kwa utetezi wao kuhusu uamuzi wa Kamati Kuu ya chama hicho. Mawakili wa wabunge 19 wamefaulu katika hoja ya Baraza Kuu kukosa usawa.


Hukumu kwenye mzani

Jambo moja ni uhakika, Jaji Mkeha ameamua kutumia umahiri wake wa kisheria kuunda mzani kwenye hukumu. Kila mmoja atoke mahakamani akijiona mshindi. Hata hivyo, hukumu yake inafumua kasoro za kisheria kwenye vyama vyote vya siasa nchini.

Jaji Mkeha ameyagusa makosa yaliyofanywa na Chadema kwa wajumbe wa Kamati Kuu, waliowafukuza wabunge 19, kuhudhuria mkutano wa Baraza Kuu, uliosikiliza rufaa na kutoa uamuzi. Hilo lilikiuka moja ya misingi ya haki asili.

Moja ya misingi ya haki asili (natural justice) ni uamuzi au waamuzi wa shauri kutokuwa sehemu ya kesi. Imeandikwa kwa kilatini “Nemo judex in causa sua”, yaani haruhusiwi mtu yeyote kuwa hakimu wa kesi yake mwenyewe.

Wabunge 19 viti maalumu, walikata rufaa Baraza Kuu, wakipinga Kamati Kuu kuwavua uanachama. Kwa maana hiyo, Kamati Kuu ilishtakiwa Baraza Kuu kwa kutotenda haki.

Kisha, wajumbe wa Kamati Kuu wakahudhuria Baraza Kuu, wakasikiliza rufaa na kushiriki uamuzi. Wajumbe Kamati Kuu walikuwa mahakimu wa kesi yao.

Jaji Mkeha, alipokuwa anajenga hoja kuhusu usahihi wa Kamati Kuu Chadema kuwavua uanachama wabunge 19, alifanya marejeo katika kitabu cha “Halsbury's Laws of England” toleo la 19, ukurasa wa 201.

Jaji Mkeha amenukuu kwa kirefu uhalali na ubatili wa taasisi kufukuza wanachama wake.

Kwa kifupi, nukuu hiyo inasema kuwa jamii yoyote yenye mwafaka wa mkataba wa maandishi, mwanachama wake hatafukuzwa uanachama mpaka hatua zake ziwe kwa nia njema, kwa masilahi ya hiyo jamii na kwa kufuata kanuni zilizowekwa.

Ikiwa mwanachama atafukuzwa uanachama kwa nia njema na baada ya kupewa nafasi ya kusikilizwa, uamuzi huo haupaswi kuingiliwa na mahakama yoyote.

Baraza Kuu Chadema lipo kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho. Wajumbe wake wameainishwa kikatiba. Taratibu zinaeleza kuwa mtu akiona hajatendewa haki na mkutano wa chini, anakata rufaa juu.

Katiba ya Chadema haisemi wajumbe wa Kamati Kuu wasiingie Baraza Kuu panapokuwa na rufaa.

Chadema wenyewe, kwa nia njema, wakizingatia masilahi ya chama chao na kwa kufuata taratibu zilizoainishwa kikatiba, waliamua kuwafukuza wanachama wao. Jaji Mkeha, alikosoa kilichofanyika kwa maelezo kwamba haki ya asili ilikiukwa.

Hapohapo katika hukumu ya Jaji Mkeha, jina la John Mnyika au kwa cheo chake cha Katibu Mkuu Chadema, ametajwa mara nyingi. Kauli yake aliyoitoa Novemba 25, 2020, akiwaita wabunge 19 kama waasi na wasaliti wa chama, imerejewa mara kadhaa kwenye hukumu.

Kauli hiyo ya Mnyika ambayo iliwasilishwa mahakamani na kusajiliwa kama kiambatanishi HJM-01, ilikwenda pamoja na kuwaalika wanachama wa Chadema na umma kwa jumla, kutoa maoni, ni adhabu gani Kamati Kuu iwape wabunge 19 waliokula kiapo cha ubunge kinyume na matakwa ya chama?

Mnyika aliyetoa matamshi hayo hadharani, alikuwa katibu wa kikao cha Kamati Kuu, kilichoketi na kuwafukuza uanachama wabunge 19, ambao alishatangulia kuwaita wasaliti na waasi wa chama.

Kama Jaji Mkeha ametengua uamuzi wa Baraza Kuu Chadema kwa hoja kuwa watu waliokuwa sehemu ya kesi, walishiriki kikao na kuchangia uamuzi, kwa nini hakuona kuhusu Mnyika kuwaita wasaliti wabunge 19, kisha akahudhuria kikao cha Kamati Kuu na kushiriki uamuzi?

Jaji Mkeha aliona haki asili ilikiukwa kwa wajumbe wa Kamati Kuu kuingia Baraza Kuu, ila Mnyika aliyenadi makosa na mashtaka ya wabunge 19, kuhudhuria kikao kilichopaswa kusikiliza shauri na kutoa uamuzi, akiwa mmoja wa waamuzi, hilo hakuona kama ni tatizo.


Twende nukta kwa nukta

Rejea mwanzo kabisa wa mgogoro. Nani aliwashtaki Halima na wenzake 18? Walishtakiwa wapi? kina nani wasikiliza shauri? Utagundua kuwa walioshtaki ndiyo waliosikiliza shauri na kutoa hukumu.

Kamati Kuu Chadema ilikutana baada ya Uchaguzi Mkuu 2020 na kuamua kwa kauli moja kutotambua matokeo yote. Wanachama 19 wanajitokeza kwenda bungeni kula kiapo cha ubunge, kinyume na matakwa ya chama.

Katibu Mkuu wa chama, ambaye ndiye katibu wa Kamati Kuu na anayeitisha vikao vyote vya chama, anatokeza kulalamika na kuwashambulia wabunge 19 kwa uasi na usaliti.

Kamati Kuu inaitishwa, inaketi. Uamuzi unatolewa. Dhahiri, Kamati Kuu Chadema ilikuwa hakimu wa kesi yake yenyewe.

Hili si la Chadema peke yake. Vyama vyote vina mifumo inayofanana. Mwaka 2016, CCM walifukuza uanachama wanachama wao bila kuwasikiliza wala kuzingatia chochote kuhusu haki asili.

Ni sakata la Sophia Simba na wenzake. Walioshtaki CCM ndiyo walioketi kusikiliza shauri na kufanya uamuzi.

Mifumo ya vyama ni ileile, inaelekeza kuwa ukiona hujatendewa haki na kikao cha chini, panda ngazi ya juu. Bahati mbaya, wajumbe wa vikao vidogo kitaifa, hubeba sifa za moja kwa moja kuhudhuria vile vikubwa.

Mjumbe wa Kamati Kuu CCM, anafuzu ujumbe wa Halmashauri Kuu Taifa (Nec), vivyo hivyo Mkutano Mkuu.

Tangu hukumu ya Jaji Mkeha iliyotoka Desemba 14, 2023, wanasheria wamekuwa wakijenga hoja kuwa Chadema walijisahau.

Wajumbe wa Kamati Kuu wangepaswa kutoka nje ya kikao ili kuruhusu waliobaki washughulike na rufaa ya akina Halima.

Mambo mawili ya kuzingatia; mosi, wajumbe wa Kamati Kuu wangeondoka, maana yake Baraza Kuu lingeketi pasipo viongozi wote wa juu wa kitaifa na kanda.

Je, kusingeibuka manung’uniko mengine kisheria kwa viongozi wa kitaifa, kuadhibiwa na kundi la viongozi wa chini?

Pili, wajumbe wa Baraza Kuu ambao wangebaki kwenye kikao kusikiliza na kufanya uamuzi kuhusu shauri la wabunge 19, wangefanya kazi chini ya ushawishi kuwa kutengua uamuzi wa Kamati Kuu, maana yake ingekuwa kwenda kinyume na Mwenyekiti wa chama, Makamu wenyeviti, Katibu Mkuu, viongozi wote wa kitaifa na kanda. Mazingira hayo yanatenda haki?

Hiyo ndiyo sababu hukumu ya Jaji Mkeha inafumua mifumo ya vyama vyote, kuhusu jinsi ya kushughulikia mashauri ya nidhamu kwa wanachama wake. Kamati za kiutendaji, ziondolewe majukumu ya kusikiliza mashauri ya kinidhamu na kufanya uamuzi.

Mathalan, Chadema wangekuwa na kamati maalumu ya kusikiliza na kuamua kuhusu mashauri ya nidhamu, vilevile kungekuwa na kamati ya rufaa, kusingetokea mkanganyiko wa kisheria ambao umeubuliwa na hukumu ya Jaji Mkeha.

Kamati Kuu Chadema, badala ya kusikiliza na kuchakata shauri, wangewashtaki wabunge 19 wa viti maalumu kwenye baraza la nidhamu na uamuzi. Kesi ingetoka hapo ingekwenda baraza la rufaa. Uteuzi au uchaguzi wa wajumbe ungezingatia kutokuwa na muingiliano.

Hukumu ya Jaji Mkeha inaonyesha udhaifu mkubwa uliopo Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa. Vyama vya siasa vinasajiliwa pasipo kuhakiki na kujiridhisha kuwa katiba zao hazikiuki misingi ya kisheria.

Matokeo yake vyama vinafuata katiba ila mahakama inabatilisha uamuzi kwa sababu vimekiuka misingi kisheria.

Sheria ya Vyama vya Siasa, kifungu 6C (5), inaeleza kuwa mwanachama hatafukuzwa uanachama kwenye chama chake mpaka pale uamuzi utakapokidhi matakwa ya katiba ya chama husika.

Chadema walitimiza matakwa ya kikatiba, ila walikiuka misingi ya kisheria. Halafu, Katiba ya Chadema ilisajiliwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Ni wakati mwafaka pendekezo la kuwa na Baraza la Usuluhishi na Uamuzi wa mashauri ya vyama vya siasa, lizingatiwe. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), limekuwa likipigia kelele hili.

Kenya wana baraza tayari. Linaitwa Political Parties Disputes Tribunal (PPDT), lina wajibu wa kushughulikia mashauri yote ya vyama. Suala la wabunge 19 Chadema, lingefika baraza, kama mifumo ndani ya chama chao ingegonga mwamba.

Katika siasa za vyama, kuna nadharia inaitwa “Party brand ambassadors”, yaani wanachama wa chama kimoja, kutumika kwa masilahi ya chama kingine.

Ndivyo Chadema wanawaona Halima na wenzake. Kwamba wapo bungeni kwa tiketi ya Chadema lakini kwa masilahi ya CCM.

Tiba ya masuala hayo ni Katiba ya nchi kuweka misingi bora ya uendeshaji wa vyama vya siasa. Ofisi ya Msajili kupitia kwa umakini katiba za vyama na kujiridhisha kuwa hazisuguani na misingi ya kisheria.

Katiba ya nchi itambulishe uwepo wa Baraza la Usuluhishi na Uamuzi wa mashauri ya vyama vya siasa.